Hotuba ya Mheshimiwa Jakaya
Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati wa kufungua
Mkutano Mkuu wa Maofisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi Katika Ukumbi wa Bunge,
Dodoma, 12 Februari 2013
Mheshimiwa
Dkt. Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi;
Mheshimiwa
Rehema Nchimbi, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma;
Ndugu
Said Mwema, Inspekta Jenerali wa Polisi;
Makamishna
na Naibu Makamishna wa Jeshi la Polisi;
Ndugu
wajumbe;
Wageni
waalikwa;
Mabibi
na Mabwana;
Utangulizi
Nakushukuru
sana Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mkuu wa Jeshi la Polisi
nchini kwa kunialika kuja kushiriki katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Maofisa
Waandamizi wa Jeshi la Polisi wa mwaka 2013. Nakupongeza sana Inspekta Jenerali kwa
utaratibu huu mzuri mliojiwekea. Hii ni fursa nzuri kwenu kupima maendeleo
mliyopata katika utekelezaji wa majukumu yenu.
Mtajua mmefanikiwa kiasi gani na maeneo au mambo gani yamewatatiza. Kwa
kufanya hivyo mnaweza kujua jinsi gani mtaimarisha mafanikio yenu, na mtatatuaje
changamoto zinazowakabili ili mpate ufanisi mkubwa zaidi siku za usoni.
Natumia
neno “ufanisi mkubwa zaidi siku za usoni” kwa makusudi kabisa, kwani ni ukweli
ulio wazi kuwa kila kukicha Jeshi la Polisi limekuwa linapata mafanikio. Hata hivyo bado haitoshi lazima mlenge kupata
mafanikio makubwa zaidi katika kupambana na uhalifu. Nakupongeza kwa dhati kabisa Inspekta
Jenerali, Makamu wa Polisi, Maafisa na askari wote wa Jeshi la Polisi kwa kazi
kubwa na nzuri mnayoendelea kuifanya. Ni
ushahidi ulio wazi kuwa uhalifu unazidi kudhibitiwa na wahalifu wa aina
mbalimbali wanazidi kubanwa. Endeleeni
na mwendo huo huo.
Kauli
Mbiu ya Mwaka Huu
Mheshimiwa Waziri;
Inspekta Jenerali; na
Washiriki watu;
Nimevutiwa sana na Kauli Mbiu ya
mkutano wenu wa mwaka huu inayosema ‘Tujenge Uwezo wa Jamii na Polisi Kukabiliana
na Vurugu, kwa kuimarisha Utii wa Sheria bila Shuruti”. Kauli Mbiu hii
imebeba ujumbe muafaka katika mazingira tuliyonayo sasa katika nchi yetu. Hivi
sasa matukio ya vurugu yanaanza kuwa taarifa za kawaida. Kila kukicha au kila baada ya muda mfupi kuna
tukio la vurugu ya aina fulani mahali fulani na kwa sababu mbalimbali. Kauli mbiu hii, inatukumbusha ukweli huo na
umuhimu wa jamii na Polisi kushirikiana katika kukabiliana na vurugu
nchini. Aidha Kauli Mbiu yenu
inasisitiza nafasi ya utii wa sheria bila shuruti katika kuzuia vurugu
zisitokee au pale zinapotokea ziweze kumalizwa haraka bila ya madhara makubwa kwa
pande husika. Mimi naamini kama shabaha
za Kauli Mbiu hii zitatimia, vurugu hazitakuwepo nchini na Tanzania patakuwa
mahali salama kuishi kwa kila mtu.
Mheshimiwa Waziri;
Ndugu Inspekta Jenerali;
Makamanda Waandamizi;
Vurugu
ni changamoto mpya ya usalama wa raia, mali zao na nchi ambayo hatuna budi
kukabiliana nayo. Hatuna budi kukaa
kitako na kutafakari kwa makini kiini cha vurugu na jinsi ya kukabiliana nazo
kwa maana ya kuzuia zisitokee na zinapotokea zinamalizwa haraka bila ya kuwa na
athari kubwa au kupunguza madhara kwa watakaoathirika. Wapo wadau wengi ambao kila mmoja wao anao
wajibu wake anaopaswa kuutekeleza. Kila mdau anatakiwa kuutambua wajibu huo na
kuhakikisha kuwa anatimiza ipasavyo yale yanayomhusu. Ninyi katika Jeshi la Polisi mnajua vyema
wajibu wenu katika kudhibiti vurugu.
Bahati nzuri wajibu huo umetamkwa kisheria na una miongozo yake ambayo
imeandikwa na hufundishwa katika vyuo na hufanyiwa mazoezi vikosini.
Nawaomba
suala la kuzuia na kudhibiti vurugu mlipe kipaumbele cha juu. Najua siku za nyuma haikuwa lazima kufanya
hivyo kwa sababu halikuwa tatizo kubwa.
Siku hizi sivyo. Vurugu zinakuwa
nyingi na za aina nyingi hivyo kugeuka kuwa shughuli kubwa ya jeshi letu. Vurugu zinasababishwa na mambo mengi. Zipo zinazosababishwa na vyama vya siasa kwa
kufanya mikutano na maandamano yasiyoruhusiwa.
Wakati mwingine hata pale yaliporuhusiwa wahusika hufanya mambo
yasiyohusika ama wakati au baada ya mkutano.
Pia zipo vurugu zinazosababishwa na kauli za wanasiasa au wafuasi wa
vyama vya siasa. Vilevile zipo vurugu
zinazosababishwa na watu kugombea rasilimali kama vile ardhi kwa wakulima na
wafugaji na baina ya wananchi wasiokuwa na ardhi na wamiliki wa maeneo makubwa.
Lakini, zipo pia vurugu zinazosababishwa na kauli na vitendo vya baadhi ya
viongozi wa dini na waumini wao. Kama
yale yaliyotokea jana Buseresere, Geita.
Mheshimiwa Waziri;
Ndugu IGP;
Hatukuwa
na hali tuliyonayo sasa ya watu kutumia
njia ya vurugu kuelezea hisia zao au kujaribu kutatua matatizo
yanayowakabili. Maadam sasa yameanza kujitokeza
kwa nguvu hatuna budi kukabiliana kisawasawa na aina hii ya uhalifu. Hatuna budi
kujifunza namna bora ya kukabiliana na vurugu. Hatuwezi kusema yatapita,
lazima tukubali ukweli kuwa matukio haya yanaweza kuendelea kuwepo na hata kuongezeka
siku za usoni. Tunachotakiwa kufanya ni
kuhakikisha kuwa tunajijengea uwezo wa kudhibiti vurugu na kufanya athari zake
zinakuwa ndogo.
Katika kukabiliana na vurugu kwanza
kabisa ni muhimu kuelekeza nguvu zetu kwenye kuzuia zisitokee. Kwa ajili hiyo ni muhimu kuyatambua maeneo na
mazingira yanayoweza kuleta au kusababisha vurugu kutokea. Kuwatambua wahusika wakuu na kuwasiliana nao ili
kuelewana nao kuhusu namna ya kupata ufumbuzi wa tatizo lililopo ili kuzuia
madhara yasitokee. Natambua kuwa kazi
hiyo mmekuwa mnaifanya kwa mafanikio makubwa.
Na mara zote pale ushauri wenu ulipopuuzwa madhara yalitokea. Naomba muendelee na jitihada hizo. Zitaliepusha taifa katika hatari nyingi.
Mheshimiwa Waziri;
Ndugu IGP; na
Ndugu Makamanda;
Ninapoyasema
haya kwenu natambua vilevile kwamba jukumu hilo si lenu peke yenu. Shughuli za kuzuia vurugu zisitokee au
kutuliza zinapotokea na kupata ufumbuzi wa migogoro iliyozua vurugu inahusu wadau wengine
pia. Kwa mfano vurugu za wakulima na
wafugaji kugombea ardhi zitapatiwa ufumbuzi wa uhakika na mamlaka zinazohusika
na upangaji wa matumizi ya ardhi.
Wakitenga maeneo kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji inasaidia kutatua
migogoro iliyopo na kuzuia isitokee siku za usoni. Hali ni hiyo hiyo kwa migogoro mingine yote ambapo
wapo wadau ambao wanaweza kufanya isitokee na kuipatia ufumbuzi
inapotokea. Naomba ninyi kwa upande wa
polisi muwatambue watu hao na kushirikiana nao kwa karibu kwa ajili hiyo.
Napenda
kutumia nafasi hii kuwaasa viongozi na mamlaka husika kuwa wawe wepesi kutambua
maeneo yenye migogoro inayoweza kusababisha vurugu na kuyatafutia ufumbuzi
mapema masuala hayo. Aidha migogoro na
vurugu zinapotokea na wao wawe mstari wa mbele kushiriki katika jitihada za
kutafuta suluhisho. Wasifanye ajizi bali watekeleze yanayowahusu kwa ukamilifu
na kwa wakati. Bila ya hivyo vurugu hazitaisha. Halikadhalika, ushirikiano na uelewa wa
wahusika wenyewe wa mgogoro au suala linaloweza kusababisha vurugu na utayari
wao nao unaweza kuepusha shari na madhara.
Pale ambapo ushirikiano utakapokosekana na migongano kujitokeza, umahiri
wa polisi kushirikisha wadau wote unahitajika kutuhakikishia ushindi.
Natambua
kuwa katika kutimiza wajibu wenu kumekuwepo na lawama nyingi na madai dhidi ya
Jeshi la Polisi. Nawapongeza kwa jinsi
mnavyoshughulikia tuhuma dhidi yenu.
Mmekuwa mnachukua hatua za kufanya uchunguzi na pale kosa
lilipodhihirika hamkusita kuchukua hatua.
Naomba muendelee na utaratibu huo mzuri.
Unaliletea heshima Jeshi letu na kuwaziba midomo watu wasiowatakia
mema. Aidha, nawaomba mtambue maeneo ya
udhaifu na kuyatafutia ufumbuzi kuanzia kwenye mafunzo ya vyuoni mpaka malezi ya
askari wawapo kambini.
Hatua kadhaa zinachukuliwa
kuzikabili changamoto
Makamanda na Maofisa Waandamizi
wa Jeshi la Polisi;
Nashukuru
Ndugu IGP na Mheshimiwa Waziri kwa kuwa wawazi kuhusu changamoto zinazowakabili
na jinsi mnavyoendelea kuzikabili na mlivyojipanga kuzikabili siku za
usoni. Napenda kuwahakikishia kuwa
Serikali itakuwa nanyi bega kwa bega kutafuta ufumbuzi wa changamoto
zinazowakabili. Natambua kuwa changamoto
kubwa na ya msingi ni ile ya kutokutengewa fedha za kutosha. Hili ni tatizo la kweli lakini tumekuwa
tunalishughulikia na nawaahidi tutaendelea kufanya hivyo. Jeshi la Polisi ni muhimu sana hatutaacha
lidhoofike.
Ndio maana tangu tulipoingia
madarakani (mwaka 2005) tumeongeza sana
bajeti ya Jeshi la Polisi na kuboresha mazingira ya kazi kwa kadri tulivyoweza.
Kwa mfano mwaka 2005/06 bajeti ya
Jeshi la Polisi ilikuwa shilingi bilioni
103.7 na tumeiongeza mwaka hadi mwaka mpaka kufikia
shilingi bilioni 334 mwaka 2012/13. Tutaendelea kuiongeza mwaka ujao wa fedha na miaka
ijayo. Tulipoingia madarakani tulianzisha
program ya ujenzi nyumba bora za kuishi za askari, wakaguzi na maafisa wa Jeshi
la Polisi. Mpaka sasa ujenzi wa maghorofa 90 yanayochukua familia 360 umekamilika. Programu hiyo ambayo inafanana na ile ya
Jeshi la Ulinzi ilisimama kwa matatizo ya upatikanaji wa fedha ambayo
tutayatafutia ufumbuzi.
Aidha, kuanzia mwaka huu tutaongeza
uwekezaji kwenye kuboresha usafiri, zana na vitendea kazi katika Jeshi la
Polisi. Kazi itaenda sambamba na kuboresha
maslahi na mazingira ya kuishi na kufanya kazi.
Ndugu
wajumbe;
Kwa maneno mengine napenda kuwaambia
tutaendeleza na kazi kubwa tuliyoianza na tunayoendelea kuitekeleza ya
kuboresha utendaji wa Jeshi la Polisi.
Kimsingi lengo ni kulifanya jeshi lila kisasa. Hayo ndiyo maudhui na malengo ya Programu ya
Maboresho ya Jeshi la Polisi ya Miaka Mitano (2010/2011-2014/2015). Programu hii mliibuni na kuitayarisha
wenyewe. Sisi Serikalini tulipoletewa
mapendekezo yenu tuliyapokea kwa mikono miwili na Baraza la Mawaziri lililofanyika
tarehe 31 Machi, 2011 liliupitisha Mpango
huo.
Sote tuliunga mkono nia njema ya
kutaka Jeshi la Polisi liwe la kisasa na lenye watendaji wenye weledi wa hali
ya juu na walio tayari kushirikiana na jamii kuzuia uhalifu. Hivyo nawapongeza kwa kuanza kutekeleza Programu
hiyo japokuwa kuna changamoto za hapa na pale. Nawaahidi kuwa tutaendelea kutoa
fedha zetu hata kuomba mikopo na misaada.
Pamoja na hayo, nawaomba mtupie macho
kutoa mafunzo mahsusi kwa uendelezaji wa rasilimali watu hususan katika
taaluma ambazo mnao watu wachache au
hawapo kabisa. Mpango huo pia uwe na
mapendekezo ya namna ya kuimarisha vyuo vyetu vya ndani ikiwa ni pamoja na kuboresha
mitaala, vifaa vya kufundishia na uwezo wa wakufunzi. Tuvifanye vyuo vyetu kuwa
vya kisasa ili vikidhi mahitaji ya sasa na ya baadae.
Mafunzo
yanayotolewa yalenge kuwaanda maofisa na askari kutumia zaidi sayansi na
teknolojia katika utendaji wao. Lazima
Jeshi la Polisi liende na wakati. Hakuna namna tunaweza kukwepa. Hivyo lazima
mafunzo yaweke msisitizo kwenye matumizi ya sayansi na teknolojia. Matumizi
hayo yanakuwa na maana zaidi katika kipindi hiki ambacho nchi yetu ina Mfumo wa
Taifa wa Usajili na Utambuzi wa Watu niliouzindua tarehe 7 Februari 2013. Mfumo huu utarahisisha sana kazi ya Jeshi la
Polisi kama mtautumia ipasavyo. Mimi nina imani kuwa tukiimaarisha mafunzo,
Jeshi la Polisi litafanya makubwa kuliko ilivyo sasa.
Malalamiko
dhidi ya Jeshi la Polisi
Inspekta
Jenerali wa Polisi;
Naomba
muongeze bidii kupambana na utovu wa maadili ili tupunguze kunyoshewa kidole kuhusu
tuhuma za rushwa na kasi ndogo ya upelelezi wa makosa. Hili la rushwa
nimelisema mara nyingi, lakini kutokana na umuhimu wake leo narudia tena
kulisema. Tuhuma za rushwa zinachafua sifa nzuri ya Jeshi letu. Nafahamu kuwa
sio wote katika Jeshi la Polisi wanaojihusisha na vitendo vya kuomba na kupokea
rushwa. Jeshi lina maofisa na askari wengi ambao ni waadilifu na wachapa kazi
wenye uzalendo wa kweli kwa nchi yetu. Lakini waswahili wana msemo usemao: “nazi mbovu harabu ya nzima”.
Maana yake ni kuwa askari wachache
wasiokuwa waadilifu wanaweza kuharibu sifa ya wengi walio wazuri. Najua na ninyi jambo hili linawakera. Hivyo naomba viongozi muweke uzito
unaostahili kwa masuala ya uadilifu na uaminifu wa askari na maofisa wa Jeshi
la Polisi. Wekeni utaratibu mzuri wa kupokea na kushughulikia maoni na
malalamiko ya wananchi. Msiwaonee muhali wale wataobainika, miongoni mwenu, kujihusisha
na vitendo vya rushwa.
Pamoja na vitendo vya kuomba na kupokea
rushwa, Jeshi la Polisi linalalamikiwa na wananchi kwa kuendesha upelelezi wa
kesi za jinai kwa kasi ndogo. Kwa sababu hiyo, kesi zilizoko mahakamani
zinachukua muda mrefu kumalizika kuliko inavyostahili. Nawaomba, mlitafutie ufumbuzi wa haraka suala
hili. Mimi nilidhani tulipotenganisha
shughuli za upelelezi na uendesha mashtaka ingesaidia. Inaelekea bado. Nawasihi Maafisa, Wakaguzi na askari
waliopangiwa kufanya kazi za upelelezi kuifanya kazi hiyo kwa ufanisi na kasi
inayokubalika kisheria. Mkifanya hivyo
mtasaidia kupunguza moja ya kero kubwa na ya muda mrefu ya msongamano wa
mahabusu magerezani.
Ushirikiano uimarishwe
Ndugu
wajumbe;
Nawapongeza
sana kwa kuwashirikisha wananchi kwa karibu katika kupambana na uhalifu. Tafadhali dumisheni na kuendeleza falsafa ya
ulinzi shirikishi. Ni muhimu sana na ni
jawabu sahihi kwa uhaba wa polisi nchini. Uwiano wa askari polisi na raia ni 1:1,184 wakati ule unaokubalika kimataifa
ni 1:450. Lakini hata kama tungekuwa
na uwezo wa kuongeza ukubwa wa Jeshi la Polisi na kufikia au kukaribia uwiano
unaofaa, lisingeweza kupambana na uhalifu bila kushirikiana na wananchi na vyombo
vingine vya dola na jamii kwa ujumla. Hivyo ni vyema kuimarisha ushirikiano
uliopo baina ya Jeshi la Polisi na wananchi na vyombo vingine vya dola kwa ujumla. Aidha tujenge
uwezo wa wadau wengine wanaosaidia kuelimisha jamii kutii sheria bila shuruti.
Hawa tuwape muongozo sahihi wa namna ya kufanya nao kazi. Watakuwa mtaji mkubwa
katika mapambano dhidi ya uhalifu nchini.
Vilevile hatuna budi kuimarisha
ushirikiano uliopo kati yetu na taasisi mbali mbali za kanda na za kimataifa
zinazojihusisha na mapambano dhidi ya uhalifu kama vile Inter-pol, “East African
Police Chiefs Cooperation Organisation (EAPCCO)” na “Southern African Regional Police Chiefs Cooperation Organisation (SARPCCO)”.
Taasisi hizi zinasaidia sana na zitaendelea kufanya hivyo katika kupambana na
uhalifu wa kimataifa kama vile biashara ya madawa ya kulevya na uharamia. Bila
ya kuwa na ushirikiano mzuri, Jeshi letu peke yake haliwezi kupambana na
kushinda uhalifu wa namna hiyo.
Mwisho
Mheshimiwa Waziri;
Inspekta Jenerali wa Polisi;
Makamanda na viongozi wakuu wa Jeshi la Polisi;
Ndugu wajumbe;
Mabibi na Mabwana;
Kwa
kumalizia napenda kuwapongeza wale wote walioshiriki kuandaa mkutano huu kwa
kazi nzuri waliyofanya. Nawaomba wajumbe wote wa mkutano mkitoka hapa
mkatekeleze kwa vitendo kwenye mikoa na maeneo yenu yale mtayokubaliana. Sisi
tunawaombea kila la heri na mafanikio katika kutekeleza majukumu yenu mazito na
muhimu kwa taifa letu na watu wake.
Baada
ya kusema hayo sasa ninayo furaha
kutamka kuwa Mkutano Mkuu wa Maofisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi wa mwaka
2013 nimeufungua rasmi. Nawatakia Mkutano mwema na wenye mafanikio.
Asanteni
kwa kunisikiliza.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment