Turn off for: Swahili
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 13.2.2013
RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
ametoa wito kwa wananchi wote kuitumia fursa ya kupata vitambulisho vya
Taifa kwani ni haki yao ya kikatiba na kuwasihi waachane na propaganda
za baadhi ya watu za kuhusishwa utoaji wa Vitambulisho vya Taifa na utashi wa kisiasa.
Dk. Shein aliyasema hayo leo huko katika viwanja vya Baraza la Wawakilishi, viliopo Chukwani Mjini wa Zanzibar. Katika Sherehe za utoaji wa Vitambulisho vya Taifa.
Katika
maelezo yake, Dk. Shein alirejea kauli yake ya kuwahakikishia wananchi
wa Zanzibar kuwa Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi vitaendelea kuwepo
na kutumika kwa madhumuni yaliokusudiwa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar
ya mwaka 1984.
Alisema
kuwa uzoefu wa makosa yaliyotokea wakati wa usajili wa Vitambulisho vya
Mzanzibari Mkaazi utumike ili kuondoa kasoro na matokeo yatakayoathiri
kupatikana ufanisi katika kuendesha zoezi hilo la Vitambulisho vya
Taifa.
Alieleza
kuwa kuwepo kwa vitambulisho vya Taifa, kutaisaidia Serikali katika
kupanua wigo wa ukusanyaji wa mapato yake na hivyo kuweza kuziimarisha
huduma za kijamii, kama vile elimu, afya na upatikanaji wa maji safi na
salama.
Aidha,
alisisitiza kuwa mapato hayo yatasaidia kuimarisha miundombinu ya
barabaram huduma za umeme na pia, kuimarisha ulinzi wa raia na mali zao
kadhalika itakuwa ni rahisi katika kukabiliana na tatizo la wafanyakazi
hewa jambo ambalo hupelekea serikali kupoteza fedha nyingi.
Dk.
Shein aliwakumbusha watendaji wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa
(NIDA) kuendeleza umakini na uadilifu walio nao, kwa kutambua dhamana
kubwa waliyonayo kwa niaba ya Watanzania.
“Kazi
yenu inahitaji uzalendo, ustahamilivu na kuweka mbele maslahi ya nchi
badala ya maslahi binafsi, jambo ambalo sina shaka mnalielewa vyema na
mtalitekeleza, lakini ni wajibu kukumbushana kwani, tunaambiwa kuwa
ukumbusho huwafaa walioamini”alisema Dk. Shein.
Aidha, kwa upande wa Zanzibar, Dk. Shein alisema kuwa wananchi
wake hawana budi kuzingatia kuwa kutokana na nchi yenyewe ni ya visiwa
haiwezi kuhimili ongezeko lkubwa la watu kutokana na rasilimali zilizopo
hasa rasilimali ya ardhi.
Hivyo,
alisisitiza kuwa NIDA haina budi kuhakikisha kuwa vitambulisho
vinavyotolewa ni kwa ajili ya wale wenye haki ya kupatiwa vitambulisho
hivyo ambao ni raia halali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pia,
Dk. Shein aliwahimiza viongozi wa vyama vya siasa, madhehebu ya dini
pamoja na vyombo vya habari kuunga mkono jitihada za Serikali katika
zoezi hili kwa kuhakikisha kuwa wanawapa wananchi elimu ya kutosha juu
ya zoezi hilo pamoja na umuhimu wake.
Dk.
Shein alitoa pongezi kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kwa
kulifanikisha jambo hilo la kihistoria, Mkurugenzi wa NIDA na
wafanyakazi wote wa Mamlaka hiyo kwa jitihada zao na ushirikiano wao
hadi yakapatikana mafanikio hayo.
Nae Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Pereira Ame Silima alieleza kuwa umuhimu wa kuwa na vitambulisho
vya Taifa ni jambo la msingi ambalo litaweza kuwa na manufaa makubwa
kwa kuunganisha mifumo mikubwa ya Usajili ya Kitaifa.
Alisema
kuwa pamoja na kufanikiwa kufikia hatua ya kuanza kuwa na vitambulisho
vya Taifa, mradi huo unakabiliwa na changamoto kubwa ambayo ni
upatikanaji wa fedha za kuendeshea mradi, ikitiliwa maanani kuwa zoezi
hilolinatakiwa kuhusushwa pia na Daftari la kudumu la wapiga kura, kwa
madhumuni ya vitambulisho kutumika katika kura ya maoni ya katiba mwaka
2014, pamoja na kusaidia katika uchaguzi mkuu 2015.
Mapema
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Taifa, Bwana Dickson Maimu alisema kuwa
NIDA itaendelea na utoaji wa vitambulisho kwa watu wote waliosajiliwa na
kuchukuliwa alama za vidole, picha na saini kulingana na ratiba ya
utekelezaji wa zoezi la usajili na utambuzi wa watu kitaifa itatolewa
kwa umma hapo baadae.
Katika
sherehe hizo, Rais Dk. Shein alikabidhiwa kitambulisho chake na Naibu
Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ambapo pia, Makamu wa Pili wa Rais,
nae alikabidhiwa chake na Dk. Shein. Baada ya hapo Dk. Shein
aliwakabidhi vitambulisho vyao watu mbali mbali katika makundi tofauti
kutoka Bara na Zanzibar akiwemo Mama Maria Nyerere, Mkuu wa Majenshi ya
Ulinzi na Usalama Davis Mwamunyange, Wawakilishi, viongozi wa dini,
wastaafu, wenye ulemavu, wake wa viongozi na wengineo.
Utoaji
wa vitambulisho vya Taifa awamu ya kwanza ni tukio ambalo lilizinduliwa
rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete
mnamo Februari 7 mwaka huu huko katika viwanja vya Karimjee mjini Dar-es
Salam.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
0 comments:
Post a Comment