MKUU wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo ameliagiza Jeshi la Polisi mkoani humo, kumkamata Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema akihusishwa na uchochezi wa vurugu zilizotokea katika Chuo cha Uhasibu kilichopo Njiro jijini Arusha jana asubuhi.

Mulongo alithibitisha kukamatwa kwa mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Albert Msando ambaye anadaiwa kuwepo chuoni hapo na Lema pamoja na baadhi ya wanafunzi wanaodaiwa kuwa vinara wa vurugu hizo.

Vurugu hizo zilitokea jana saa nne asubuhi baada ya Mkuu wa Mkoa kufika chuoni hapo kwa ajili ya kuwasikiliza wanachuo ambao walitaka kuandamana kufuatia mwenzao Elly Kago (22) kuuawa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia jana jirani na chuo.

Mulongo alifika chuoni hapo baada ya kupigiwa simu na Lema ambaye alifika mapema na kuzungumza na wanafunzi hao, huku akiwatuliza wasiandamane kufuatia kifo cha mwenzao.
Lema aliwaambia vijana hao kuwa mazingira ya nchi ya sasa ni magumu kufuatia wengi wao kukosa ajira na hivyo baadhi yao wasio wastahamilivu kujiingiza katika vitendo vya ujambazi na unyang'anyi.

Hivyo aliwataka wasiwe na jazba badala yake watafute ufumbuzi wa matukio hayo na kuangalia jinsi ya kumsitiri mwenzao.

Baada ya Mulongo kufika na kuwakuta wanafunzi wakizungumza na Lema, alipewa nafasi naye kuzungumza, lakini aliutaka uongozi wa chuo kuandaa vipaza sauti na mahala pazuri pa kuzungumzia.

Maelekezo hayo ya mkuu wa mkoa kutaka vipaza sauti yaliamsha maneno ya chini kwa chini na baada ya kuanza kuzungumza wanafunzi hao walianza kumzomea wakimlazimisha aache.

Alipokatisha hotuba yake, wanafunzi walianza kurusha mawe na hivyo kulazimika kuondolewa chuoni hapo pamoja na viongozi mbalimbali wa serikali chini ya ulinzi, huku mabomu yakirindima kuwatawanya wanafunzi hao.

Wanafunzi hao walisikika wakisema mkuu huyo ‘amewaboa’ kwa kuwa wao wana msiba yeye anaenda kudai vipaza sauti ili kusikiliza madai yao, huku akiwa amevaa suti, hatua iliyotafsiriwa kama kutojali msiba wao.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mbele ya wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Mulongo alisema wameuagiza uongozi wa chuo hicho kukifunga kwa muda usiojulikana kwa ajili ya usalama.

Alisema taarifa za awali za polisi zinasema kuwa vurugu na kifo cha mwanafunzi huyo vina mahusiano makubwa na masuala ya kisiasa kwa ajili ya watu kujijenga kisiasa na kwamba vyombo vya usalama vinaendelea na uchunguzi wa kina juu ya suala hilo.

Mkuu huyo wa mkoa hakutaja idadi ya wanafunzi waliokamatwa hadi jana bali alisema vinara wote wamekamatwa pamoja na Msando huku akisisitiza kuwa Lema ametoroka na anaendelea kusakwa.

“Jambo baya kwa leo ni siasa kuingia katika vurugu hizo, kwani Lema ndiye alihusika hata kuita viongozi wa serikali chuoni hapo ambapo aliingia hapo bila kufuata utaratibu na kuanza kuzungumza na wanafunzi,’’ alisema Mulongo.

Kaimu Mkuu wa Chuo, Dk. Faraji Kasida baada ya kupewa maagizo ya kukifunga chuo hicho ambacho kipo chini ya Wizara ya Fedha alitangaza kuwa kimefungwa kwa muda usiojulikana.

Vurugu hizi zimeibuka zikiwa zimebaki siku chache kabla ya kuanza kwa kampeni za uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata nne za Jiji la Arusha.

Liwale balaa 
Mwandishi Wetu kutoka Liwale anaripoti kuwa wananchi wasiojulikana wamechoma moto ofisi na nyumba za mbunge wa Liwale mkoani Lindi, Faith Mitambo pamoja na nyumba za viongozi wa CCM na wa vyama vya ushirika vya msingi kwenye mji wa Liwale.

Tukio hilo la aina yake lilitokea juzi likianzia katika Kijiji cha Liwale B ambako wakulima wa Chama cha Msingi cha Minali walikataa malipo ya korosho ya sh 200 kwa kilo yakiwa ya pili badala ya sh 600 waliyoahidiwa mwaka jana.

Kwa mujibu wa Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso, vurugu hizo zilitokea saa tisa alasiri, huko wilayani Liwale ambapo kundi la watu wanaodhaniwa kuwa wakulima wa korosho walijaribu kuzuia gari lililokuwa na malipo.

Alisema kuwa wakulima hao walikuwa wakipinga malipo ya pili ya korosho na hivyo kuanza kufanya vurugu na uharibifu mkubwa wa mali.

Senso alisema hadi jana taarifa za awali zilionesha kuwa nyumba 14 zilichomwa moto, baadhi ya mifugo ilijeruhiwa na kuangamizwa na kufanyika uharibifu wa miundombinu ya barabara.

Alisema kufuatia tukio hilo, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema alituma timu maalumu ikiongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCP), Issaya Mngulu kwenda kuongeza nguvu kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa.

“Lengo ni kuhakikisha kuwa hali ya amani na utulivu inarejea haraka na wale wote waliohusika kufanya vitendo vya uhalifu wanakamatwa na kufikishwa mahakamani ili sheria iweze kuchukua mkondo wake. Hadi sasa watuhumiwa 19 wamekamatwa kwa mahojiano,” alisema.
Wakati taarifa za polisi zikieleza hivyo, mashuhuda wa tukio hilo walisema kuwa Mwenyekiti wa chama hicho cha ushirika, Mohamed Limbwilindi alikwenda kijijini hapo akiwa na sh milioni 61.4 ambazo wakulima hao wangelipwa sh 200 kwa kila kilo ya korosho.
Kwamba wengine ambao hawakupewa malipo ya awali walielezwa kuwa watalipwa sh 800, jambo ambalo lilizua mtafaruku miongoni mwao na hivyo kurudisha fedha.
Kutokana na hali hiyo, ilielezwa kuwa wananchi wenye hasira walianza kukateketeza moto ofisi ya chama hicho na nyumba ya mwenyekiti kisha pia nyumba ya katibu wake, Juma Majivuno.
Baada ya vurugu hizo huko Liwale B, alasiri vurugu hizo zilihamia mjini Liwale ambako uharibifu mkubwa wa mali ulifanyika.
Wananchi hao walichoma ofisi ya mbunge, duka la pembejeo la Hassan Mpako, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Msingi cha Umoja mjini Liwale pamoja na nyumba yake.
Akizungumzia tukio hilo, Mpako alisema; “niliona kundi kubwa la watu wanakuja nyumbani kwangu saa 3 usiku wakiwa wamebeba nondo, mawe pamoja na madumu ambayo nadhani yalikuwa na petroli,” alisema.
Mpako alifafanua kuwa watu hao walimweleza; “tunataka fedha zetu za korosho” mazingira aliyodai kuwa yalimlazimisha atimue mbio ili kujisalimisha.
Alisema watu hao waliteketeza nyumba yake pamoja na trekta dogo la mkono, pikipiki, jenereta pamoja akiba ya pembejeo za kilimo ambazo zilikuwa dukani.
Wengine waliochomewa nyumba ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya, Mohamed Ngomambo ambaye alisema anamwachia Mungu.
“Kama nimepoteza wazazi ambao wana thamani kubwa maishani mwangu nyumba ni kitu gani?” alisema Ngomambo.

Kutokana na vurugu hizo, kundi kubwa la askari wa kutuliza ghasia (FFU) toka Lindi limewasili wilayani Liwale kudhibiti hali ya usalama ambayo imetoweka.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, George Mwakajinga alizungumza kwa simu akisema kuwa mbunge wa Liwale nyumba zake mbili na ofisi vilichomwa moto.

Pia Mwenyekiti wa CCM Wilaya, Chande nyumba yake moja ilichomwa moto huku mwenyekiti wa Halmashauri ya Liwale, Abasi Matulilo naye nyumba yake ilichomwa.

“Meneja wa Chama cha Msingi cha Ilulu, Hamza Mkungura nyumba zake mbili ziliteketezwa na duka la dawa na pembejeo vile vile yaliteketezwa huku mifugo ikijeruhiwa na kuchinjwa,” alisema.
Kamanda aliwataja wengine walioathirika na vurugu hizo kuwa ni meneja mikopo wa NMB, Mohamedi Pimbi ambaye duka lake la vifaa vya umeme lilichomwa pamoja na duka la Kanisa Katoliki.

Aliwataja pia Diwani wa CCM, Hasan Muyao na Diwani wa Viti Maalumu Amina Mnocha kuwa nyumba zao zilichomwa pamoja na nyumba ya mjumbe wa NEC wa chama hicho, Hemedi Ngonani ambaye aliharibiwa maduka ya simu na vyakula. 
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top