10 WAKATA RUFANI KAMATI YA RUFANI YA UCHAGUZI TFF
RUFANI
kumi zimewasilishwa mbele ya Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi
ya TFF kuhusiana na uchaguzi utakaofanyika Februari 22 na 24 mwaka huu.
Wakati
uchaguzi wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPL Board) utafanyika Februari
22 mwaka huu, ule wa TFF wenyewe utafanyika Februari 24 mwaka huu.
Waliowasilisha
rufani mbele ya Kamati hiyo inayoongozwa na Idd Mtiginjola ni pamoja na
waombaji uongozi saba walioenguliwa katika kinyang’anyiro hicho.
Warufani hao ni Omari Mussa Nkwarulo na Michael Richard Wambura
walioomba kugombea urais na umakamu wa rais.
Wengine
ambao waliomba ujumbe wa Kamati ya Utendaji kuwakilisha kanda
mbalimbali ni Farid Nahdi (Morogoro na Pwani), Mbasha Matutu (Shinyanga
na Simiyu), Omari Isack Abdulkadir (Dar es Salaam), Eliud Peter Mvella
(Iringa na Mbeya) na Shaffih Kajuna Dauda (Dar es Salaam).
Warufani
wengine ni wadau ambao waliweka pingamizi dhidi ya baadhi ya waombaji
uongozi katika TPL Board na TFF, pingamizi ambazo zilitupwa mbele ya
Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa sababu za kiufundi.
Wadau
hao waliokata rufani ni Agape Fue dhidi ya Kamati ya Uchaguzi TFF
kupinga kumpitisha Jamal Malinzi kugombea urais, Medard Justinian dhidi
ya Kamati ya Uchaguzi TFF kupinga kumpitisha Athuman Nyamlani kugombea
urais, na Frank Mchaki dhidi ya Kamati ya Uchaguzi TFF kupinga
kumpitisha Hamad Yahya kugombea uenyekiti wa TPL Board.
Kamati
ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF imetoa siku ya kesho (Februari 9 mwaka
huu) kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa 8 mchana kwa wote wenye maslahi na
rufani hizo (interested parties) kupitia rufani hizo na kuwasilisha hoja
zao kwa maandishi.
Kwa
watakaoshindwa kufanya hivyo watapata fursa ya kuwasilisha hoja zao kwa
mdomo, ambapo wanaweza kuwa wenyewe au wanasheria wao siku ya
usikilizwaji wa rufani hizo. Rufani zitasikilizwa Jumapili (Februari 10
mwaka huu) kuanzia saa 2 asubuhi.
OLJORO MWENYEJI WA SIMBA VPL 2012/2013
Ligi
Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara msimu wa
2012/2013 inaingia raundi ya 16 kesho (Februari 9 mwaka huu) kwa mechi
nne ambapo Oljoro JKT itaikaribisha Simba jijini Arusha.
Mechi
hiyo namba 129 itafanyika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri
Abeid huku Simba ikiingia na kumbukumbu ya sare katika mechi yake
iliyopita dhidi ya JKT Ruvu wakati wenyeji wao wakiwa wameshinda 2-0
dhidi ya Kagera Sugar.
Uwanja
wa Kaitaba mjini Bukoba wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 3,000 tu
utatumika kwa mechi kati ya wenyeji Kagera Sugar na Mgambo Shooting.
Mwamuzi wa mechi hiyo atakuwa Amon Paul kutoka Musoma mkoani Mara.
Toto
Africans baada ya kufanya vibaya katika mechi tatu zilizopita ugenini
imerejea nyumbaji jijini Mwanza itakapoumana na Coastal Union ya Tanga
katika mchezo utaochezwa Uwanja wa CCM Kirumba.
Mwamuzi
Simon Mberwa kutoka mkoani Pwani ndiye atakayechezesha mechi kati ya
wenyeji Tanzania Prisons na African Lyon ambayo imepata huduma za kocha
mpya Salum Bausi kutoka Zanzibar. Hiyo itakuwa mechi ya kwanza kwa Bausi
kuiongoza timu katika VPL.
Maofisa
wengine wa mechi hiyo ni mwamuzi msaidizi namba moja Abdallah Rashid,
mwamuzi msaidizi namba mbili Abdallah Mkomwa wote kutoka Pwani wakati
mwamuzi wa mezani ni John Kanyenye wa Mbeya. Kamishna wa mechi hiyo ni
Rashid Rwena kutoka Ruvuma.
Mechi
kati ya Mtibwa Sugar na Azam iliyokuwa ichezwe kesho imesogezwa mbele
kwa siku moja ambapo sasa itafanyika Jumapili (Februari 10 mwaka huu)
katika Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro.
FDL KUENDELEA KUTIMUA VUMBI WIKIENDI
Ligi
Daraja la Kwanza (FDL) kuwania tiketi za kucheza Ligi Kuu ya Vodacom
(VPL) msimu ujao inaendelea kutimua vumbi wikiendi hii kwa mechi kumi na
moja zitakazopigwa kwenye viwanja mbalimbali.
Kundi
A keshokutwa (Februari 10 mwaka huu) Mbeya City itacheza na Polisi
Iringa katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya, Mkamba
Rangers itaumana na Burkina Faso (Uwanja wa CCM Mkamba) wakati JKT Mlale
itakuwa mwenyeji wa Kurugenzi kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea.
Green
Warriors na Ndanda zitacheza kesho (Februari 9 mwaka huu) kwenye Uwanja
wa Karume, Dar es Salaam katika moja ya mechi za kundi B. Mechi
nyingine kundi hilo kesho ni kati ya Tessema na Villa Squad kwenye
Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi.
Keshokutwa
(Februari 10 mwaka huu) Transit Camp itacheza na Ashanti United kwenye
Uwanja wa Karume, Dar es Salaam wakati Polisi Dar es Salaam na Moro
United zitavaana Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi.
Kundi
C kesho (Februari 9 mwaka huu) ni Polisi Dodoma vs Polisi Tabora
(Uwanja wa Jamhuri, Dodoma), Polisi Mara vs Mwadui (Uwanja wa Karume,
Musoma), Morani vs Kanembwa JKT (Uwanja wa Kiteto, Manyara) na Rhino
Rangers vs Pamba (Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora).
0 comments:
Post a Comment