Rais Jakaya Kikwete
ZIARA ndefu ya Rais Jakaya Kikwete nchini Marekani huenda ikaibuka na mabadiliko katika Baraza la Mawaziri au Taasisi nyeti za serikali, Raia Mwema limeelezwa.

Rais Kikwete aliondoka wiki iliyopita kwa ziara ya wiki mbili Marekani, katika wakati ambao serikali yake imegubikwa na masuala mazito yanayohitaji maamuzi yake.

Masuala hayo ni mchakato wa Katiba na uchunguzi uliofanywa na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuhusu fedha zilizochotwa kutoka katika akaunti ya Tegeta Escrow ya Benki Kuu ya Tanzania (IPTL).

Taarifa ambazo gazeti hili linazo zinaeleza kwamba baadhi ya vigogo wa serikali wametajwa
kuhusika katika suala hilo linalotajwa kuwa na harufu ya ufisadi na huenda Kikwete anatatizwa kuhusu hatua za kuchukua.

Habari hizi zinatiwa nguvu na kauli ya Spika wa Bunge, Anne Makinda, wiki hii kwamba endapo kusingekuwa na Bunge Maalumu la Katiba (BMK) na badala yake ripoti ya uchunguzi wa CAG kuwasilishwa kwenye Bunge la kawaida, kuna mawaziri wasingepona kwenye sakata hili.

Makinda alitoa kauli hiyo wakati wa tukio la kumuaga CAG aliyestaafu, Ludovick Utouh, ambaye ofisi yake ndiyo iliyochunguza suala la akaunti hiyo iliyokuwa ikihifadhi fedha za Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na kampuni ya Independent Power Tanzania (IPTL).

Kiasi cha shilingi bilioni 200 zinadaiwa kuchotwa kutoka katika akaunti hiyo na kulipwa kwa kampuni ya Pan African Power (PAP) katika mazingira ambayo vyombo hivyo vya serikali vilikuwa vinayachunguza.

“Makinda alisema aliyoyasema kwa sababu ameiona hiyo ripoti na anajua kilicho ndani. Makinda yuko bungeni tangu miaka ya 1970 na anajua ni lipi la kusema na lipi si la kusema hadharani. Kama amesema kuna mawaziri wasingepona, ujue maana yake kuna mawaziri wasingepona,” kilisema mojawapoi ya vyanzo vya gazeti ambavyo kwa sababu za wazi hatutaweza kutaja majina yake.

Vyanzo vya gazeti hili serikalini vimeeleza kwamba umekuwa utaratibu wa kawaida wa Kikwete kukaa nje ya nchi kwa kipindi kirefu wakati anapokuwa na mambo yanayomsumbua kichwani na anayotaka ufumbuzi wake.

Ziara ya kwanza ndefu ya Kikwete ughaibuni ilikuwa Oktoba mwaka 2007, wiki chache baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kiliibua iliyoitwa Orodha ya Mafisadi katika tukio lililofanyika Septemba 15 mwaka huo.

Watu wa karibu na Kikwete wameliambia gazeti hili kuwa “Rais alitumia ziara hiyo katika nchi za Ulaya na Marekani kubadili upepo na kupunguza msongo wa mawazo kwa sababu suala hilo lilichukuliwa kwa uzito mkubwa hata na Jumuiya ya Kimataifa”.

Kikwete pia alikuwa nje ya nchi, safari hii Afrika Kusini, mwaka 2011, wakati Bunge lilipoamua kuchukua hatua dhidi ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, ambaye alikuwa katika kashfa ya kudaiwa kutaka kuhonga wabunge ili wapitishe bajeti ya wizara yake.

Ni katika wakati huo ndipo alipofanya pia mabadiliko yaliyomwondoa Jairo pamoja na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.

Desemba 18 mwaka jana, Kikwete alianza ziara ndefu nchini Marekani na siku mbili baadaye akakubali kujiuzulu kwa mawaziri wanne katika Baraza lake la Mawaziri kutokana na Operesheni Tokomeza.

Kikwete aliondoka nchini kwa kile kilichoelezwa kwenda Marekani kwa ajili ya kufanyiwa matibabu ya afya yake, lakini aliporejea; mawaziri Khamis Kagasheki, Emmanuel Nchimbi, Shamsi Vuai Nahodha na David Matayo, walikuwa tayari wameondolewa kutoka serikalini.

Mara hii tena Rais Kikwete ameenda Marekani kwa wiki mbili. Hii si ziara ya kawaida. Na ameondoka baada ya kuona ripoti za CAG na Takukuru ambazo Makinda amesema kuna mawaziri hawatapona. Kikwete mwenyewe ndiye anayejua nini kinafuata, alisema mmoja wa manaibu mawaziri wa serikali ya Kikwete.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top