Makubaliano baina ya Rais Jakaya Kikwete na viongozi wa Kituo
cha Demokrasia Tanzania (TCD), kutaka Bunge Maalumu lifikie ukomo Oktoba
4, mwaka huu yamezua sintofahamu mjini hapa huku uamuzi huo ukionekana
kuwachanganya viongozi wa Bunge hilo.
Kutwa nzima ya jana, viongozi wa Bunge Maalumu
walishinda kwenye vikao vya mashauriano huku wabunge wa CCM wakitarajiwa
kukutana jana usiku kwenye makao makuu ya chama hicho kupewa taarifa
rasmi za uamuzi huo.
Katika makubaliano baina ya TCD na Rais Kikwete,
imeamuliwa kuwa uamuzi wa Rais kupitia Tangazo la Serikali (GN) 254 la
kuongeza siku 60 hadi Oktoba 4 uheshimiwe na baada ya tarehe hiyo Bunge
liahirishwe.
Uamuzi huo ni kinyume cha azimio la Bunge Maalumu
la Agosti 5, 2014 ambalo lilirekebisha Kanuni ya 14 (4) na kuifuta
Jumamosi katika siku zilizotajwa kuwa za kazi, pia sikukuu na siku za
Jumapili.
Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta alikaririwa
akiwaambia wajumbe wa Bunge hilo kwamba Rais alikuwa ameridhia kwamba
siku 60 alizotoa hazingejumuisha Jumamosi, Jumapili na siku za sikukuu.
Ni kwa msingi huo, Bunge hilo likapanga kwamba
lingeendelea na shughuli zake hadi Oktoba 31, wakati Mwenyekiti wa Bunge
atakapokabidhi Katiba inayopendekezwa kwa Rais Kikwete.
Hata hivyo, makubaliano yaliyofikiwa baina ya
viongozi wa TCD na Rais yanaonekana kuvuruga kabisa ratiba ya Bunge hilo
ambalo jana na juzi, Kamati ya Uongozi ilikutana mara kadhaa kuona
jinsi ya kunusuru mchakato huo.
Ingawa haikufahamika mara moja kama vikao hivyo
vya kamati ya uongozi inayoongozwa na Sitta mwenyewe vinajadili nini,
lakini taarifa zimedai huenda kukawa na mabadiliko makubwa ya ratiba.
Habari nyingine zinadai kwamba mabadiliko hayo
huenda yakapunguza muda wa baadhi ya shughuli za kazi za Bunge hilo ili
liweze kukamilisha kazi yake ikiwamo wajumbe kupiga kura ya uamuzi.
Katika kikao cha jana asubuhi, kamati hiyo
ilishindwa kurekebisha ratiba yake ili iendane na siku zilizosalia,
hivyo kuahirishwa kwa kuwapa kazi wataalamu wake kuleta mapendekezo
ambayo yangejadiliwa jana mchana.
Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad
alithibitisha jana kwamba ratiba ya Bunge imebadilika kutokana na hoja
nyingi kukubalika ndani ya kamati.
“Kamati ya uongozi itakutana baadaye (jana)
kuangalia vipengele ambavyo hawakukubaliana kwenye kamati ndivyo
wavipangie muda na ratiba itajulikana baada ya kikao hicho,” alisema
Hamad.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Hofu ya akidi
Hata hivyo, habari zaidi zinadai kwamba uongozi wa
Bunge Maalumu ulichanganywa na kuwapo kwa hoja za baadhi ya wajumbe
wake kutaka kwenda Makka kwa ajili ya kushiriki Ibada ya Hijja, hali
inayotishia akidi kwa ajili ya kuendesha vikao.
Kanuni za Bunge Maalumu zinataka kuwapo kwa nusu
ya wajumbe kutoka pande zote za Muungano wakati wa kuendesha vikao vyake
na theluthi mbili ya wajumbe hao kila upande wakati wa kufanya uamuzi
au kupiga kura.
“Tumetoka kwenye kikao mchana huu na pengine
tutaitana tena maana hatujafikia mwafaka, kuna mambo mengi yamejitokeza
lakini kubwa ni hili la wenzetu ambao wanataka kwenda Hijja, kuondoka
kwao kunaweza kuathiri akidi kwa kiasi kikubwa,” kilisema chanzo chetu
kutoka ndani ya kamati hiyo.
Kutokana na matakwa hayo, hivi sasa Ofisi ya
Katibu wa Bunge inafanya tathmini ili kufahamu idadi ya wajumbe ambao
watakwenda Hijja Septemba 22, mwaka huu, ambao wengi wanatoka Zanzibar.
Hamad alikiri kwamba kuna mambo mengi ambayo ofisi
yake inayafanyia kazi na kwamba hilo la Hijja ni mojawapo... “Kwa sasa
siko katika nafasi ya kuzungumza kwa kirefu, kikao cha Kamati ya Uongozi
kimeisha na bado kuna kazi nyingi za kuona jinsi tunavyoendelea.”
Tayari Bunge hilo limetikiswa na kutokuwapo kwa
wajumbe waliosusia vikao tangu Aprili 16, mwaka huu ambao ni wajumbe
wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambao unaundwa na vyama
vya CUF, Chadema na NCCR Mageuzi na baadhi kutoka Kundi la 201.
Taarifa ya TCD
Jana saa 7:00 mchana, Mwenyekiti wa TCD, John
Cheyo alikutana na wanahabari na kueleza kuwa katika mazungumzo yao na
Rais wamekubaliana mambo matano ya msingi kwa mustakabali wa nchi.
Alisema pamoja na kazi ya msingi iliyofanywa na
Bunge Maalumu, mchakato unaoendelea hauwezi kutoa Katiba Mpya ambayo
itatumika katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
“Muda hautoshi kukamilisha mchakato na kufanya
mabadiliko yatakayohitajika ya sheria, kanuni na taasisi mbalimbali
zinazohitajika,” alisema Cheyo ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi Mashariki
(UDP).
Alisema kura ya maoni ilipangwa kufanyika Aprili
2015 na kama itabidi irudiwe, basi itabidi irudiwe itakuwa Juni au Julai
2015, muda ambao Bunge la Jamhuri linatakiwa livunjwe.
“Ili Katiba Mpya itumike katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, itabidi
uhai wa Bunge na Serikali uongezwe zaidi ya 2015, jambo ambalo sisi
viongozi wote hatuliungi mkono,” alisema Cheyo.
Alisema kwa kutambua kuwa kama kura ya maoni
ikifanyika, italazimisha Uchaguzi Mkuu wa 2015 kuahirishwa,
wamekubaliana kura hiyo iahirishwe hadi baada ya uchaguzi huo.
Bunge Maalumu
Cheyo alisema Bunge Maalumu kwa sasa linafanya
kazi kwa mujibu wa Tangazo la Serikali (GN), namba 254 lililotolewa na
Rais Kikwete ambalo uhai wake utakoma Oktoba 4.
“Inategemewa kuwa Oktoba 4 Katiba inayopendekezwa
itapatikana. Tulikubaliana hatua hii iachwe ifikiwe na baada ya hapo
Bunge liahirishwe hadi baada ya Uchaguzi Mkuu 2015.
“Tarehe 4 Oktoba ndiyo mwisho. Hiyo ndiyo sheria
iliyopo, sisi hatuna mamlaka ya kuandika GN mpya, GN imetolewa na Bunge
hili liko kihalali. Tulichokuwa tunabishana lisife kesho,” alisema.
Akijibu maswali ya wanahabari kama ana uhakika
Bunge hilo litaweza kukamilisha kazi yake ndani ya siku zilizobaki,
Cheyo alisema “Tumeheshimu sheria iliyopo tarehe nne Watanzania
wanategemea Katiba Mpya itakuwa imepatikana, sasa kama haitapatikana
hilo msiniulize kwa sababu hilo si jukumu langu.”
Alipoulizwa kama rais ajaye baada ya Uchaguzi Mkuu
wa 2015 ataendeleza mchakato pale ulipoishia alisema: “Naomba Mungu
rais ajaye awe anayejali maoni ya wananchi hilo naomba kabisa. Sasa
tukipata rais ambaye hatutambui sisi wote na mawazo yetu, basi tutakuwa
tumekosea katika kupiga kura.”
Mabadiliko ya 15 ya Katiba
Cheyo alisema kwa vile Uchaguzi Mkuu wa 2015
utafanyika kwa kutumia Katiba ya 1977, ni vyema yakafanyika mabadiliko
madogo ili kuruhusu uchaguzi huru na wa haki.
Mabadiliko hayo yatalenga kuwezesha uwapo wa tume
huru ya uchaguzi, mshindi wa urais ashinde kwa zaidi ya asilimia 50,
kuruhusu mgombea binafsi na kuingiza ibara itakayoruhusu matokeo ya
urais kupingwa mahakamani.
“Vyama vya siasa ambavyo vinapenda kupendekeza
mambo mengine ya kurekebisha katika Katiba ya 1977 vinaombwa kufanya
hivyo kwa vile muda tulionao ni mdogo,” alisema Cheyo.
Alisema walikubaliana kuwa marekebisho hayo yafanyike katika
Bunge la Jamhuri litakaloanza Novemba 5 na ikishindikana yafanywe
Februari 2015.
Ukawa kurudi bungeni
Cheyo alisema suala la kurudi au kutorudi ndani ya
Bunge Maalumu la Katiba kwa wajumbe wa Ukawa halikuwa sehemu ya mkutano
kati ya Rais na TCD.
“Kila siku nasema uamuzi wa vyama tuuheshimu. Wale
wana sababu zao za kutoingia bungeni ni lazima tuheshimu msimamo wao
kwa sababu wanazo sababu,” alisema.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment