Mkuu
wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam (CBE) Prof. Emanuel Mjema
akizungumza wakati wa hafla ya kuwakaribisha waliokuwa wanafunzi wa chuo
hicho waliohitimu miaka iliyopita wakati wa mwendelezo wa shughuli
mbalimbali za chuo hicho kutimiza miaka 50.
Bw.
Alexander Msofe akizungumza na wahitimu wa miaka ya nyuma wa chuo cha
CBE kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo hicho ambaye ndiye alikuwa
mgeni rasmi wakati wa hafla ya kuchangia maendeleo ya CBE iliyowahusisha
wahitimu hao jijini Dar es salaam.
Bw.
Isdori Kwayi, mmoja wa wahitimu wa chuo cha CBE mwaka 1972 akitoa
mchango wake kuhusu namna chuo hicho kinavyoweza kukusanya fedha kutoka
katika vyanzo mbalimbali ili kuboresha miundombinu yake wakati wa
hafla fupi iliyowahusisha wahitimu wa chuo hicho jijini Dar es salaam.
Baadhi
ya wahitimu wa CBE wa miaka iliyopita wakifuatilia masuala mbalimbali
wakati wa hafla ya kuchangia maendeleo ya Chuo cha Elimu ya Biashara Dar
es salaam ambacho kimetimiza miaka 50. Picha na Aron Msigwa –MAELEZO.
Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
Wahitimu
wa vyuo mbalimbali nchini wameaswa kujenga utaratibu wa kuchangia
miradi na shughuli mbalimbali za maendeleo ya elimu katika vyuo
walivyosoma na kuepuka kutumia fedha nyingi katika kuchangia masuala
yasiyo na tija kwa maendeleo ya taifa.
Hayo
yamebainishwa jana jijini Dar es salaam na mkuu wa Chuo cha Elimu ya
Biashara Dar es salaam (CBE) Prof. Emanuel Mjema , wakati wa hafla ya
kuwakaribisha chuoni hapo waliokuwa wanafunzi wa chuo hicho waliohitimu
miaka iliyopita kwenye mwendelezo wa maadhimisho ya miaka 50 ya chuo
hicho.
Akizungumza
na wahitimu hao amesema kuwa wanayo nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko
katika sekta ya elimu hapa nchini kwa kushiriki na kutumia sehemu ya
mapato wanayopata kupunguza changamoto za elimu za uhaba wa vyumba vya
madarasa, maabara na miundombinu mingine isiyo rafiki kwa maendeleo ya
wanafunzi.
“Elimu
ndio msingi wa maendeleo, sisi tulipata elimu iliyo bora lazima
tuchangie kwa sehemu yetu kuonyesha tunayajali maeneo tuliyosoma, hivi
sasa mwamko wa watu wengi uko katika kuchangia sherehe na harusi lakini
kwenye suala la elimu hali ni tofauti” Amesema Prof. Mjema.
Amesema
wahitimu hao wana nafasi kubwa ya kuendelea kuwa mfano kwa kuendelea
kutoa mrejesho kwa uongozi juu ya nini kifanyike katika kuendeleza sekta
ya elimu chuoni hapo sanjali na kueleza mapungufu yaliyopo pamoja na
kutoa michango yao juu ya namna ya kuendeleza kiwango cha taaluma.
Amebainisha
kuwa chuo hicho kinahitaji kiasi cha shilingi bilioni 3 ili kiweze
kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo ya upanuzi wa kampasi zake,
ujenzi wa miundombinu,uongezaji wa vifaa vya kufundishia, madarasa,
maabara na kumbi za mihadhara.
Kwa
upande wake Bw. Alexander Msofe akizungumza na wahitimu hao kwa niaba
ya Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo hicho ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi
katika hafla hiyo amesema chuo hicho kinafurahia matunda ya mafanikio
ya kutimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.
Amewaambia
wahitimu hao kuwa licha ya changamoto mbalimbali zinazokikabili chuo
hicho kimeweza kuongeza idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa kwa mwaka
kutoka 25 waliodahiliwa mwaka 1965 hadi 14,000 katika mwaka wa masomo
wa 2014/15 pamoja na ongezeko la idadi kozi za masomo zinazotolewa
kutoka 1 hadi 6.
Bw.
Msofe ameongeza kuwa chuo cha CBE sasa kinatimiza miaka 50 kikiwa chuo
pekee Afrika ya Mashariki na katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya
Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kinachotoa wanafunzi wa shahada ya
vipimo.
Mafanikio
mengine ni pamoja na kuongezeka kwa kozi za masomo na ngazi za mafunzo
hadi kufikia shahada, kuongezeka kwa wakufunzi wenye shahada za uzamivu
(PhD) chuoni hapo pamoja na chuo kuanzisha ushirikiano wa elimu na vyuo
vikuu vingine nje ya nchi kikiwemo Chuo Kikuu cha Eastern Finland
katika utoaji wa mafunzo ya shahada za uzamivu kwa kutumia TEKNOHAMA kwa
nchi za SADC.
Aidha,
katika kuelekea tamati ya maadhimisho ya chuo hicho yatakayofanyika
Januari 13, mwaka 2015 ameitaka jamii na wahitimu wote wa chuo hicho
wajitokeze wingi kutoa michango yao ya hali na mali itakayowezesha
ujenzi wa vyumba vya madarasa na mihadhara, maabara na vyumba vya kulala
wanafunzi.
Kwa
upande wao wanafunzi waliowahi kusoma chuoni hapo wakizungumza kwa
nyakati tofauti wakati wa hafla hiyo wametoa wito kwa wadau mbalimbali
wenye mapenzi mema kujitokeza kuchangia ukamilishaji wa programu
mbalimbali za maendeleo zilizoanzishwa na uongozi wa chuo hicho.
Wamesema
kuwa badala ya kuiachia serikali pekee jamii na wahitimu hao wanayo
nafasi kubwa ya kuchangia maendeleo ya chuo hicho kutokana na wao
kuendelea kufaidika na elimu waliyoipata kipindi wakiwa wanafunzi wa
chuo hicho.
Wameiomba
serikali kuhakikisha kuwa inaendelea kukisaidia chuo hicho na kukitumia
kupata ushauri wa kufanikisha masuala mbalimbali yakiwemo mafunzo kwa
wafanyabiashara na uimarishaji wa mifumo ya ukusanyaji wa kodi hapa
nchini ili kuondoa tatizo la asilimia kubwa ya watu kukwepa kodi.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment