Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein
Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ametupilia mbali maombi
ya kumtaka kufungua mazungumzo na viongozi wa Ukawa, ili kupatikana kwa
mwafaka kwa wabunge wa Bunge la Katiba kutoka Zanzibar na kurejea
bungeni.
Akizungumza na Mwananchi Katibu wa Kamati ya
Kuwaunganisha wabunge kutoka Zanzibar, Mohamed Yussuf Mshamba amesema
kamati yake imepokea barua maalumu kutoka Ofisi ya Rais ikiwataarifu
kuwa Rais hayuko tayari kufungua mazungumzo hayo.
“Tumepokea majibu kutoka Ofisi ya Rais, Ikulu
Zanzibar, tumeelezwa kuwa suala hilo ni vyema likabaki mikononi mwa
Bunge la Katiba na suala la usuluhishi imeshauriwa tufanye wenyewe
ZIRPP,” alisema Mshamba.
Aidha alisema kwamba kutokana na msimamo huo wa
Rais Dk Shein, kazi ya kuwaunganisha wabunge wa Zanzibar imekuwa ngumu
kwa vile matarajio ya ZIRPP ilitegemea kazi hiyo ingerahisishwa na Rais
na kuzika tofauti ya kimsimamo.
Mshamba alisema maombi yao waliyawasilisha Agosti
mwaka huu baada ya kamati ya kuwaunganisha Wazanzibari kukamilisha
kazi ya kukusanya maoni ya wananchi kupitia kongamano la wazi juu ya
nini kifanyike na kuhakikiisha Wazanzibari wanamaliza tofauti zao na
kutetea maslahi ya Zanzibar.
‘Kwa ufupi kazi ambayo tumekuwa tukijaribu
kuifanya imekuwa ngumu, tunachowaomba wabunge wa Zanzibar waache tofauti
za kiitikadi na kuweka mbele maslahi ya Zanzibar, njia pekee rahisi na
mwafaka warudi bungeni kushirikivikao,” alisisitiza Mshamba.
Alisema kimsingi kuna makosa yaliyofanyika tokea
mwanzo, ikiwa ni pamoja na utungaji wa sheria yenyewe ya Bunge la
Katiba na kujikuta wakiingizwa wanasiasa kwenye Bunge hilo, badala ya
kuwa la wataalamu na watu wengine wasiotokana na vyama vya kisiasa.
Mshamba alieleza kuwa kuanza kwa ‘mguu’ huo mbaya
kumesababisha kuzuka kwa mivutano na mijadala yenye mitazamo zaidi ya
itikadi za kisiasa badala ya kuongozwa na nguvu ya hoja, ufahamu,
upembuzi yakinifu na uzoefu wa wabunge wa Bunge hilo.
“Chadema pekee ndicho ambacho katika ilani yake
iliahidi kuwa kikishika madaraka ya uongozi kitabeba jukumu la kuandika
katiba mpya, si CCM, NCCR-Mageuzi, TLP wala CUF vilivyoahidi jambo
hilo, sasa inashangaza kuona vyama hivyo vimekuwa mstari wa mbele
kushupalia Katiba Mpya na kususia Bunge la Katiba,” alisema Mshamba.
Mwananchi
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment