MJUMBE
wa Bunge Maalum la Katiba, Said Arfi (CHADEMA), jana alitimua hali ya
hewa bungeni baada ya kugusia muundo wa Serikali tatu unaopendekezwa na
rasimu ya katiba, akihoji wajumbe walio wengi wanatoa wapi mamlaka ya
kujitia upofu na kuingiza muundo wa serikali mbili.
Arfi ambaye pia ni mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kutoka
Jimbo la Mpanda Mjini, aliwatibu wajumbe wenzake wakati akisoma
mapendekezo ya wajumbe walio wachache katika kamati namba kumi kuhusu
sura ya kumi na moja na kumi na tano.
Muda mfupi baada ya Arfi kufika mbele kwaajili ya kusoma taarifa
yake, Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta alimtania akimuuliza kama
bado ana msimamo wake wa kutaka kufungua kesi Mahakama Kuu kupinga Bunge
la Katiba.
Arfi kwa kujiamini alisema ndiyo, na kwamba sasa anashawishika zaidi
baada ya kuona wajumbe walio wengi wakijiba mamlaka ya kubadili maudhui
ya msingi ya mapendekezo ya wananchi kwenye rasimu yanayotaka muundo wa
serikali tatu.
Kabla ya kuanza kusoma maoni yake, Arfi alieleza kushangazwa na hatua
ya mjumbe mwenzake, Mohammed Seif Khatib aliyesoma maoni ya wengi kwa
kuwataja kwa majina wajumbe wengine wa UKAWA huku akijua kwamba
hawakushiriki katika mjadala huo, akisema ni kuwapotosha wananchi.
Ghafla, Khatib alisimama na kumpa taarifa akisema kuwa aliwataja
akimaanisha kwamba ni wajumbe wa kamati namba kumi bila kujali kama wapo
au hawapo bungeni.
Baada ya majibizano hayo, Arfi alianza kusoma maoni ya wachache huku
akirejea historia ya chimbuko la vuguvugu la serikali tatu na kuhoji ni
kwanini wajumbe walio wengi wanajitia upofu na kufuta ibara zinazotaja
maneno ya nchi washirika na serikali ya Tanganyika.
Hatua hiyo ilimfanya Sitta kuingilia kati akimtaka mjumbe huyo
ajielekeze kwenye hoja badala ya kurejea kujadili suala la idadi ya
serikali kwa kuwa lilishamalizika, jambo ambalo Arfi alihoji ni kwanini
kila inapotajwa serikali tatu, walio wengi wanakereka na kujitia vipofu.
Kauli hiyo ya neno vipofu, ilimwinua mjumbe kutoka kundi la 201
anayewakilisha watu wenye ulemavu (wasioona), Amoni Mpanju, akimtaka
Arfi afute maneno hayo kwa kuwa yanakera na kuwadhalilisha wasioona
kwamba hawana akili kama wale wanaoona.
Mpanju alishangiliwa na wajumbe wengi, huku baadhi ya sauti za
wanawake zilisikika zikisema “UKAWA huyo aliyebaki humu ndani na
serikali tatu…afute kauli”.
Hata hivyo, Arfi aliomba radhi na kufuta kauli hiyo akisema kuwa
hakuwa na maana hiyo kwani neno hilo limo katika kamusi ya Kiswahili
sanifu, kisha akaendelea kusoma taarifa yake hadi mwisho.
Tanzania Daima
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment