MKURUGENZI
wa Oganaizesheni, Mafunzo na Uratibu wa Kanda wa Chama Cha Demokrasia
na Maendeleo (CHADEMA) Benson Kigaila, amesema ofisi ya Katibu Mkuu wa
chama hicho haijapokea pingamizi lolote kutoka kwa mgombea wa nafasi
yoyote dhidi ya mwenzake.
Majibu ya Kigaila yamekuja siku moja baada ya vyombo vya habari na
mitandao ya kijamii kumkariri mgombea wa nafasi ya mwenyekiti Taifa wa
CHADEMA, Kansa Mbarouk, akidai kwamba amepeleka barua ya kumwekea
pingamizi la kugombea nafasi hiyo dhidi ya mwenyekiti wa sasa wa chama
hicho, Freeman Mbowe.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kigaila alisema hadi juzi
saa tano usiku alipotoka ofisi za makao makuu ya chama hicho, hakukuwa
na barua yoyote iliyohusu pingamizi lolote, iliyofikishwa katika Ofisi
wa Katibu Mkuu wa chama hicho Dk. Willibrod Slaa.
“Hakuna barua yoyote iliyoletwa katika ofisi za Katibu Mkuu …nafikiri
walioomba kuchaguliwa nafasi yoyote katika chama na baraza wanafahamu
kuwa kama wana pingamizi lolote wanapaswa kulipeleka kwa Katibu Mkuu
wao,” alisema Kigaila.
Kigaila aliwataka wagombea kusoma vizuri katiba na kanuni za chama na
mabaraza yao ili kujiweka vizuri katika kipindi hiki cha uchaguzi
unaoendelea katika chama chao.
Katika pingamizi lililodaiwa kupelekwa katika ofisi za CHADEMA Makao
Makuu, Ofisi za Msajili wa Vyama vya Siasa na Mhakamani, Mbarouk
anasemekana kudai kuwa Mbowe, kwa kugombea ueneyekiti, amekiuka katiba
ya chama hicho na maagizo ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini.
Vyombo vya habari jana vilinukuu barua ya Mbarouk yenye kumbukumbu
namba Mbarouk/UCH/14 inayodaiwa kwenda kwa Katibu Mkuu wa CHADEMA na
Msajili wa Vyama vya Siasaikisema kuwa hadi Septemba 14 siku ya uchaguzi
mkuu wa chama hicho, Mbowe atakuwa ametumikia vipindi viwili katika
nafasi ya mwenyekiti wa taifa.
“Msajili wa vyama alikuwa ametoa maelekezo kwamba chama kiitishe
Baraza Kuu na Mkutano Mkuu Maalumu kwa lengo la kubadilisha kipengele
kinachoweka ukomo wa uongozi kama litaona kuna haja hiyo kabla ya
kufanyika uchaguzi mkuu. Hata hivyo hadi naandika barua hii hakuna
dalili zozote kwamba mkutano mkuu maalumu utaitishwa na maandalizi ya
uchaguzi yanaendelea bila kujali agizo la msajili wa vyama,”
alilikaririwa Mbarouk katika barua hiyo.
Hata hivyo hoja, ambayo imekuwa ikkibuliwa na baadhi ya wanachama
walioondolewa kwenye chama au uongozi kwa sababu mbalimbali,
ilishajibiwa na CHADEMA, kupitia kwa Mkurugenzi wa Habari na
Mawasiliano, John Mnyika, mwanzoni mwa mwezi Julai mwaka huu.
Alisema Agosti 13 mwaka 2006, CHADEMA ilifanya marekebisho makubwa ya
katiba, bendera na kadi za chama hicho na kufuta katiba ya 2004,
bendera na kadi zilizokuwa zinatumika wakati huo.
Katika mkutano huo kulifanyika mabadiliko ya kifungu cha 6.3.2 c
kilichokuwa kinaweka ukomo wa uongozi, hivyo kusomeka kuwa, “kiongozi
anayemaliza muda wake ana haki ya kugombea tena ilimradi awe amekidhi
masharti ya kuchaguliwa ambayo yameainishwa kwenye kanuni za chama
kifungu cha kumi.”
Aliongeza kuwa Mbowe na Dk. Slaa bado wanazo sifa kama wakitaka
kugombea kwa mujibu wa katiba, kanuni, maadili na itifaki za chama, na
kwamba wala si kwa mujibu wa matamshi ya msajili wa vyama.
“Wenye kujua nani ana sifa ya kugombea na nani hana, maamuzi hayo
hutolewa na mkutano mkuu na Baraza Kuu la chama kwa mujibu wa katiba
wala hawafanyi hayo kwa maelekezo ya msajili,” alisema Mnyika, ambaye
anafahamu vema suala hilo, kwani alikuwa katibu wa kamati iliyoandika
katiba mpya, baada ya kukusanya maoni ya wanachama kutoka wilayani na
mikoani kuhusu marekebisho ya katiba.
“Hatua hiyo ilifuata baada ya waraka uliosambazwa nchi nzima
kukusanya maoni ya wanachama, hivyo suala la marekebisho ya katiba
haikuwa hoja ya Mbowe wala Dk. Slaa,” alisisitiza.
Wafuatiliaji wa masuala ya siasa ndani ya CHADEMA wanasema pingamizi
hilo hewa ni sehemu ya hujuma zinazopangwa na mahasimu wa chama hicho
kama jaribio la kuharibu uchaguzi mkuu unaoendelea sasa.
CCM na vyama vinavyopambana na CHADEMA, hasa vinavyoundwa na wafuasi
za zamani wa chama hicho waliovuliwa uanachama au kuachishwa uongozi,
vinaogopa uwezo wa Mbowe katika kuongoza chama hicho, na vinadhani
kwamba ni rahisi kujipenyeza na kuhujumu iwapo Mbowe hatakuwa kiongozi.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa hata ofisi ya msajili wa vyama
vya siasa imekuwa ikusumbuliwa na mamlaka za serikali ili msajili
ahakikishe Mbowe hagombei uongozi katika CHADEMA kwa sababu yoyote.
Hata hivyo, baadhi ya maofisa waandamizi wa Ofisi ya Msajili wa Vyama
vya siasa wameliambia gazeti hili kuwa ofisi hiyo itashinda hila na
vishawishi hivyo.
Tanzania Daima
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment