Mwanasheria Mkuu waserikali, jaji Frederick Werema
Mabilioni ya shilingi yaliyowekwa na Watanzania katika benki za Uswisi yameanza kuhamishwa kimyakimya.
Ripoti ya Benki za Uswisi ya 2012 inaonyesha kuwa
fedha zinazotoka Tanzania zimepungua kwa karibu Sh.36.4 bilioni
ikilinganishwa na zilizokuwapo 2011 nchini humo, lakini haielezi sababu
ya kupungua kwake.
Taarifa za kuhamishwa kimyakimya kwa fedha hizo
ambazo zinaaminika kuwekwa na Watanzania waliowahi kuwa katika utumishi
wa umma, imekuja wakati ambao Serikali inasubiriwa kutoa taarifa yake
kuhusu vigogo walioficha fedha nchini humo, ambazo zinaaminika
walizipata kwa njia zisizo halali.
Awali, kiasi cha fedha kilichotajwa kufichwa
katika benki hizo ni Sh.327.9 bilioni (Dola za Marekani 204.96 milioni),
lakini taarifa mpya ya 2012 inaonyesha kuwa kiasi hicho kimepungua hadi
Dola za Marekani 182.2 milioni (Sh.291.5 bilioni).
Kiasi hicho cha fedha kinaweza kujenga barabara ya
lami yenye urefu wa kilomita 300 ambao ni sawa na kutoka Morogoro hadi
Iringa.
Akizungumzia ripoti hiyo, Balozi wa Uswisi nchini,
Olivier Chave alisema: “Hadi mwisho wa 2012, fedha zilizopo kutoka
Tanzania zimebaki Faranga za Uswisi 160 milioni (Dola za Marekani 182.2
milioni) na siyo zile za awali ambazo ni Faranga za Uswisi 180 milioni
(Dola za Marekani 327.9 milioni)……. hivyo ndiyo kusema kuwa fedha hizo
zinapungua,” alisema Chave na kuongeza:
“Inawezekana ni kutokana na kelele za vyombo vya
habari hasa Mwananchi, pengine wenye fedha wameamua kuzihamishia kwenye
benki za nchi nyingine. Sisi Serikali ya Uswisi tunapochapisha ripoti
kama hizi kuonyesha jumla ya fedha kwa nchi zote duniani, haimaanishi
kuwa fedha zote hizo ni haramu.”
Alisema ni makosa kwa vyombo vya habari kuendelea
kuonyesha kwamba ni Uswisi pekee kunakofichwa fedha chafu, kwani zipo
nchi nyingine ambako watu wa mataifa mbalimbali huweka fedha zao ambazo
zimepatikana kwa njia haramu.
Benki za Uswisi zimekuwa zikidaiwa kutumika
kuficha fedha chafu kutoka maeneo mbalimbali duniani kutokana na usiri
wake katika kutunza taarifa za wateja.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa Kenya inaongoza kwa
nchi za Afrika Mashariki kwa kuwa na kiasi kikubwa cha fedha ambacho ni
karibu Sh.1.6 trilioni ikifuatiwa na Uganda Sh.376.7 bilioni, kisha
Tanzania Sh.291.5 bilioni. Rwanda ina Sh.55.1 bilioni na Burundi Sh.42.2 bilioni.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick
Werema alipoulizwa jana kuhusiana na taarifa hizo mpya alisema suala
hilo la fedha zilizopo Uswisi si la kuzungumza kwenye vyombo vya habari.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
“Hili jambo ni jambo nyeti sana kwa sababu kazi tuliyopewa
kuchunguza suala hili bado hatujamaliza, kwa hiyo kuanza kulizungumza
kwenye vyombo vya habari kunaweza kuathiri kazi hii,” alisema Jaji
Werema.
Aliwaomba Watanzania kuvuta subira juu ya jambo hilo akisema kamati yake inaendelea kufuatilia na taarifa itawasilishwa.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment