Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa
Serikali imekunjua makucha yake katika kudhibiti ada zinazotozwa katika vyombo vya utoaji elimu chini.
Jana, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk.
Shukuru Kawambwa alizindua rasmi mfumo mpya wa ulipaji ada katika vyuo
vya elimu ya juu, huku akisema utasaidia kudhibiti viwango vya ada
vinavyotozwa kwa wanafunzi.
Akizindua mfumo huo jijini Dar es Salaam, Dk.
Kawambwa alisema Serikali imeanzisha mfumo huo unaotarajiwa kuanza
kutumika mwaka huu katika vyuo vyote, kwa lengo la kudhibiti ada
kulingana na fani zinazotolewa.
“Sasa natarajia nitapata usingizi wa kueleweka
maana kelele za viwango vya ada zilikuwa ni kubwa, kila chuo kilikuwa na
ada yake. Niliulizwa vigezo vinavyotumika kupanga sikuwa na jibu,
lakini sasa nitakuwa na majibu tena yanayoeleweka,” alisema.
Suala la viwango vya ada katika shule na vyuo
binafsi liliwahi kuzungumziwa kwa kina siku za nyuma, huku Rais Jakaya
Kikwete na Waziri Kawambwa wakinukuliwa kwa nyakati tofauti kutaka
taasisi za elimu kupunguza viwango vya ada. Aprili 2013 akifungua
Mkutano Mkuu Maalumu wa Chama cha Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo
Visivyokuwa vya Serikali (Tamongsco) uliofanyika mkoani Mbeya, Rais
Kikwete alisema: “Elimu ni huduma muhimu na haki kwa mtoto. Siyo vyema
kugeuzwa kuwa biashara ya kuleta faida kubwa.’’
Aliongeza kuwa Serikali ilikuwa katika mchakato wa
kutathmini ada zinazotozwa vyuoni na sekondari ili kupendekeza viwango
halisi vinavyopaswa kutozwa.
Kwa sasa udadisi wa gazeti hili umebaini kuwa
wanafunzi walioanza masomo katika mwaka wa fedha 2013/2014 wanatozwa ada
kuanzia Sh360,000 kwa mwaka hadi Sh9,900,000.
Kwa mujibu wa Dk. Kawambwa, mfumo huu ambao
baadaye utaendelea hadi shule za sekondari na msingi, umepatikana
kupitia kikosi kazi cha wataalamu ambacho pamoja na majukumu mengine
kilipewa kazi ya kutathmini gharama.
Dk. Kawambwa alisema moja ya faida ya utaratibu
huo mpya ni kudhibiti taasisi zinazotoza ada kubwa kwa sababu za binafsi
ikiwamo biashara.
Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Tumaini Makumira
cha Dar es Salaam (Tudarco), Profesa Uswege Minga alisema endapo gharama
hizo zitakuwa sawa, vyuo binafsi vitaathirika kwa sababu ni gharama
kubwa kuendesha chuo kikuu.
Mwananchi
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment