WATU tisa wakiwamo askari polisi wawili wa Kituo cha Polisi
Oysterbay jijini Dar es Salaam wametiwa mbaroni wakiwa na meno 70 ya
tembo (sawa na tembo 35).
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Ulrich Matei, watuhumiwa
hao walikamatwa Julai 28, mwaka huu usiku saa nne katika kizuizi cha
Kauzeni, Kata ya Vikumbulu, wilayani Kisarawe wakiwa kwenye gari lenye
namba za usajili T 357 ABK aina ya Toyota Surf ambapo aliwataja askari hao kuwa ni Senga Idd Nyembo na Issa Mtama.
Watuhumiwa wengine waliokamatwa pamoja na askari hao ni Hamidu Hamadi
na Prosper Maleto wakazi wa Tandika, jijini Dar es Salaam, Mussa Mohamed
Ali mkazi wa Kinondoni, Amir Bakari mkazi wa Mbagala, Seif Kadro
Mdumuka mkazi wa Kisarawe, Said Kadro Mdumuka na Ramadhani Athuman
wakazi wa Chanika.
Kamanda Matei alifafanua kuwa meno hayo yana uzito wa kilo 305, yakiwa
na thamani ya sh 850,500,000, huku akitoa wito kwa wananchi kuwafichua
watu wanaojihusisha na vitendo vya ujangili ili wachukuliwe hatua bila
kujali nyadhifa zao.
Katika hatua nyingine, mkazi wa Mwananyamala, jijini Dar es Salaam,
Ibrahim Mnyanga (58) anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kukutwa na
vipande 16 vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilogramu 24.5 kinyume cha
sheria.
Mnyanga alikamatwa Julai 22, mwaka huu, saa tisa alasiri eneo la
Msimbazi Centre akiwa na masanduku mawili yenye nyara hizo za serikali.
Kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kulitokana na askari polisi wa Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam waliokuwa kwenye doria ya kawaida kumtilia
shaka.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa
Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi, Suleiman
Kova, alikiri kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo na kusema kuwa atafikishwa
mahakamani muda wowote baada ya upelelezi kukamilika.
Kamanda Kova aliongeza kuwa ameunda jopo la uchunguzi wa kifo cha
mtuhumiwa Seleman Mwinyi (46) mkazi wa Kurasini Shimo la Udongo.
Kwa mujibu wa kamanda huyo, jopo la uchunguzi linaundwa na Jeshi la
Polisi, vyombo vya ulinzi na usalama wakishirikiana na Ofisi ya
Mkurugenzi wa Mashtaka ya Jinai (DPP).
Marehemu Mwinyi alikutwa na mauti akiwa ndani ya chumba cha mahabusu
Kituo cha Polisi Oysterbay huku Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni
akidai kwamba kifo cha mtuhumiwa huyo kilitokana na kipigo kutoka kwa
wananchi wenye hasira.
0 comments:
Post a Comment