Mawaziri wapya walioteuliwa katika picha ya pamoja na Rais Kikwete 
MABADILIKO ya Baraza la Mawaziri aliyoyafanya Rais Jakaya Kikwete, yamewasha moto ndani ya Chama chake Cha Mapinduzi (CCM) kwa madai kuwa amekisaliti chama hicho tawala, Tanzania Daima limedokezwa.
 
Rais Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa CCM taifa, anadaiwa kukisaliti chama chake kwa kuwarejesha mawaziri mizigo ambao hivi karibuni walipendekezwa na Kamati Kuu (CC) ya CCM kwamba wang’olewe kwa utendaji wao mbovu.

Ikumbukwe kwamba chimbuko la mawaziri mizigo lilitokana na ziara ya Katibu Mkuu, Abdulhaman Kinana na Katibu wa Itikadi na Uenezi taifa, Nape Nnauye, katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, ambapo waliwataja baadhi ya mawaziri kuwa ni mizigo.

Katika mikutano tofauti ya hadhara, viongozi hao wa juu wa CCM walimtaka Rais Kikwete awatimue mawaziri mizigo kwa madai kuwa walishindwa kuendana na kasi ya utekelezaji wa Ilani ya CCM.

Wakiwa bado ziarani katika mikoa hiyo, Kinana alisema mawaziri mizigo watahojiwa na Kamati Kuu ya CCM na hata baada ya kuwahoji, CC iliyoketi mbele ya Rais Kikwete mjini Dodoma ilipendekeza watimuliwe.

Mawaziri waliotajwa kuwa mizigo ambao jana waliapishwa na kurejea kwenye nafasi zile zile ni pamoja na Waziri wa Kilimo na Chakula, Christopher Chiza, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia na Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe.

Lakini baada ya kuwaacha mawaziri mizigo, Rais Kikwete aliwatupa nje mawaziri watano, akiwemo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mazingira), Dk. Terezya Huvisa na nafasi yake kuchukuliwa na Dk. Binilith Satano Mahenge na Naibu wake anakuwa Ummy Ali Mwalimu.

Katika mabadiliko hayo, pia Rais Kikwete aliwatupia virago manaibu waziri wanne, ambao ni Gregory Teu, ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Philip Mulugo, ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Goodluck ole Medeye, ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Benedict ole Nangoro.

Baadhi ya makada maarufu wa chama hicho ambao waliomba majina yao yahifadhiwe, waliliambia gazeti hili kuwa kitendo cha Rais Kikwete kutomtimua hata waziri mmoja kati ya wale waliopendekezwa na chama chake baada ya kujiridhisha kwamba hawana uwezo kiutendaji, ni usaliti wa hali ya juu na unakiweka chama hicho katika mazingira mabaya.

“Si tu kwamba amekiweka chama mahali pabaya, bali pia amewashushia hadhi mzee Kinana na Nape ambao wamerejesha imani ya wananchi kwa chama kwa kiwango kikubwa,” alisema kada huyo ambaye pia ni mmoja wa wenyeviti wa CCM wa moja ya mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Mwenyekiti huyo ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu (CC) ya CCM, alisema hata baada ya Kinana na Nape kutaja majina ya mawaziri mizigo na kutaka waitwe kuhojiwa na Kamati Kuu, Rais Kikwete aliwataka viongozi hao wa chama kuongeza majina mengine ya mawaziri mizigo ili wahojiwe na kuchukuliwa hatua.

“Katika orodha ya Kinana na Nape, Waziri wa Fedha na Uchumi, Saada Mkuya,  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia, hawakuwemo. Hawa waliongezwa baadaye kwa agizo la Rais. Na  bado kulikuwa na pendekezo hata la kutaka kumwita na kumhoji Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, kwamba amezembea kupata fedha za msaada kutoka nje kwa ajili ya kuboresha reli na bandari.

“Rais kama mwenyekiti ameshiriki kikao cha kuwahoji na amepokea mapendekezo, leo amepuuzia mapendekezo ya chama. Wana CCM watawaangaliaje kina Kinana na Nape? Watawezaje kwenda tena kwenye ziara na kuikosoa serikali yao?” alihoji kada huyo.

Kiongozi mwingine wa CCM jijini Dar es Salaam, alisema kwa kawaida chama kinachoongoza serikali ndicho chenye nguvu na kinapotoa maoni dhidi ya serikali kiliyoiunda lakini yatekelezwe.

Kada huyo alikwenda mbali zaidi kwa kumlaumu Rais Kikwete kuwa hata kwenye mchakato wa Katiba kuna uwezekano mkubwa mazungumzo yake na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, kuhusu serikali tatu ni tofauti na msimamo anaouzungumza kwenye chama.

“Warioba na tume yake wamekuja na mapendekezo ya serikali tatu, wanapokutana na rais kujadili maoni hayo, bila shaka wanaimba lugha moja, anapokuja kwenye chama kinachoamini kwenye serikali mbili, anaimba wimbo huo huo. Mwisho wa siku msimamo wake uko wapi? Sitashangaa kuona chama kitaachwa kwenye mataa kama kilivyoachwa kwenye hili la wabunge mizigo,” alisema.

Alipofuatwa ofisini kwake kutaka atoe maoni kuhusu mabadiliko hayo na mapendekezo ya CCM kutaka mawaziri mizigo wang’oke, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye,  kwanza hakupatikana kwa maelezo kwamba alikuwa na kikao na Katibu Mkuu, Kinana,
Alipopigiwa simu yake ya mkononi, alisema hana cha kusema na badala yake alimtaka mwandishi wetu kuwasiliana na msaidizi wake, Daniel Chongolo.

Hata hivyo Chongolo alijibu kwa kifupi kuwa:  “Tuache Rais Kikwete awaapishe mawaziri wafanye kazi, kuhusu kauli ya mawaziri ambao walihojiwa na Kamati Kuu ya CCM litazungumzwa siku yoyote.”

Hata hivyo wakati Nape akishikwa kigugumizi kutoa kauli, Ikulu jana ilitetea kurejea kwa mawaziri mizigo.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alisema ili waziri awe mzigo kuna mambo mengi ya kuangalia.

“Siamini kama kuna waziri mzigo. Unaweza kusema waziri huyo ni mzigo, lakini lazima ujiulize kwanini? Kama hana fedha za kutosha kuendeshea wizara, utasemaje kuwa ni mzigo? Kama hana watendaji wazuri, utasemaje kama waziri huyo ni mzigo?  Kwa hiyo kuna  mambo mengi ya kuangalia,” alisema.

Katika mabadiliko ya mawaziri waliotangazwa juzi, Rais Kikwete aliwatimua mawaziri wengine watano na kuingiza sura mpya kumi, huku mawaziri wanne wakipandishwa hadhi.

Sura mpya katika baraza hilo ni Mwigulu Nchemba (Naibu Waziri Wizara ya Fedha na Uchumi), Asha-Rose Migiro (Waziri wa Katiba na Sheria), Jenista Muhagama (Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi.

Yumo Mbunge wa Kondoa Kusini, Juma Nkamia (Naibu Waziri Wizara ya (Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo), Godfrey Zambi, Mbunge wa Mbozi Mashariki, (Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika), Titus Kamani (Waziri mpya wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi) na Naibu wake atakuwa Kaika Saning’o Telele.

Pindi Chana (Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto), Dk. Kebwe S. Kebwe (Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii) na Mahamod Mgimwa (Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii).
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top