MAWAZIRI na manaibu waziri walioteuliwa kushika nafasi mbalimbali
jana waliapishwa na Rais Jakaya Kikwete katika viwanja vya Ikulu jijini
Dar es Salaam, huku baadhi yao wakianza na tambo za uwajibikaji na
wengine wakiomba ushirikiano wa karibu kutoka kwa wadau ili waweze
kutimiza majukumu yao.
Wakizungumza na waandishi wa habari, baadhi ya mawaziri hao, Saada
Mkuya Salum (Wizara ya Fedha na Uchumi), Juma Nkamia (Naibu Waziri
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo) na Dk. Asha-Rose Migiro
(Wizara ya Katiba na Sheria), kila mmoja aliomba ushirikiano kutoka kwa
wadau na Watanzania kwa ujumla.
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, alisema changamoto ya kwanza
atakayokabiliana nayo ni kuimarisha eneo la fedha ili nchi iweze
kujitegemea na kuwabeza wanaomwita ‘waziri mzigo’, wasubiri waone
utendaji wake.
Akizungumzia suala la mishahara ya wafanyakazi, alisema kama kuna
upungufu uliojitokeza kipindi cha nyuma kwa mishahara kuchelewa,
halitajirudia na kwamba mishahara itatolewa kwa wakati husika.
Alisema wanachotarajia kufanya kama wizara ni kuimarisha mapato ya
ndani ili kuweza kuondokana na utegemezi wa mataifa mengine, hasa katika
miradi ya ndani.
Alisema lazima serikali ijielekeze katika kupata miundombinu ya
kiuchumi kwa ajili ya kuondoka katika hatua ya sasa na kuelekea hatua
nyingine.
Aliongeza kuwa wakati wa uhai wa William Mgimwa, kuna mipango mingi
ya kimaendeleo waliyofanya na kuahidi kuitekeleza kwa nafasi yake mpya
ya uwaziri.
“Mimi sijui dhana ya kuitwa mizigo ina tafsiri gani, ninachojua ni
kuwa Katibu Mkuu wetu, Kinana, alikuwa mikoani na wananachi walikuwa
wanalalamikia baadhi ya mambo, hivyo ilikuwa ni wajibu wake kutuita na
kupata ufafanuzi wa yale yaliyokuwa yanalalamikiwa na wananchi na si
kwamba sisi ni mizigo,” alisema Mkuya.
Mwigulu aahidi kupambana na fedha chafu
Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi (Sera), Mwigulu Nchemba, amesema
jambo la msingi atakalolitilia mkazo ni udhibiti wa fedha chafu na
kwamba hiyo ni moja ya sekta iliyo katika Benki Kuu.
Alisema taasisi za kifedha zitafanya uchambuzi wa kitaalamu na kisha
kuwasilisha bungeni mipango dhabiti ya kuwabana watu wanaotafuta njia
ya kusafisha fedha haramu.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro, alisema alipokuwa
nje ya majukumu ya kiserikali amejifunza mengi ambayo atayatumia katika
majukumu yake ya sasa, huku akieleza kuwa uzalendo utatawala katika
suala zima la upatikanaji wa Katiba mpya.
Alisema hataruhusu hisia za kichama zitawale katika kuwapatia
Watanzania katiba waitakayo, kwa kile alichoeleza kuwa mchakato wa
katiba unamhusu kila Mtanzania pasipo kuangalia itikadi yake ya chama.
Nkamia alilia ushirikiano kwa waandishi
Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia,
kwa upande wake alisema pasipo ushirikiano kutoka kwa wadau wasitegemee
miujiza katika sekta nzima ya habari.
“Naomba kila mmoja wetu kwa nafasi yake ashiriki na tushirikiane,
katika hili hakuna muujiza utakaofanywa na mtu mmoja, hasa ninyi ndugu
zangu waandishi ni nguzo muhimu katika kutoa ushirikiano, naomba
tushirikiane,” alisema Nkamia.
Mwanza waponda
Naye mwandishi, Sitta Tumma, kutoka Mwanza, anaripoti kuwa baadhi ya
wananchi wakiwemo wanasiasa jijini Mwanza na mjini Musoma, mkoani Mara,
wameponda na kubeza uteuzi huo, ambapo wameuita ni mtindo wa kupeana
fadhila na kutesa kwa zamu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya wananchi na
wanasiasa hao walisema baraza hilo ni mzigo usiobebeka kwa wananchi, na
Rais Kikwete amejitwisha mzigo ambao hatima yake ni kiama kwa taifa,
kwani Watanzania walitarajia kuona mawaziri wawajibikaji, na si watu wa
kutafuta fedha za uchaguzi mwaka 2015.
Walieleza kushangazwa na kuingizwa wizarani Naibu Katibu Mkuu wa CCM
(Bara), Mwigulu Nchemba, ambaye amepewa Unaibu Waziri wa Fedha (Sera),
Dk. Titus Kamani (Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi), Shukuru
Kawambwa (Wizara nyeti ya Elimu), Hawa Ghasia (TAMISEMI), Juma Nkamia
(Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo), Profesa Anna
Tibaijuka (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi), Lazaro Nyalandu
(Wizara ya Maliasili na Utalii), pamoja na Mathias Chikawe kupewa Wizara
ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Mwenyekiti mstaafu wa CCM Wilaya ya Nyamagana, jijini hapa, Athumani
Zebedayo, alieleza kushangazwa na hatua ya Rais Kikwete kumbakisha
serikalini Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Shukuru Kawambwa na
mawaziri wengine mizigo waliotakiwa na CCM kuondolewa.
Alisema kuachwa kwa mawaziri hao kunatia shaka iwapo kuna dhamira ya
kweli ya kuwasaidia wananchi kupata maendeleo yaliyodumaa, na kwamba ni
maajabu pia kuingizwa katika baraza hilo, Nchemba, Dk. Kamani, Ghasia,
Chikawe, Nyalandu, Tibaijuka na Nkamia, kwani watu hao hawawezi
kuwasaidia wananchi maskini.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment