Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhani
MWENYEKITI msaidizi wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Augustino Ramadhan, amesema tume hiyo ililazimika kuweka kipengele cha Serikali tatu, katika rasimu ya kwanza na ile ya pili ya Katiba Mpya, ili kuunusuru Muungano. Jaji Ramadhan, alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na MTANZANIA Jumapili, katika mahojiano maalumu yaliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Katika mahojiano hayo, pamoja na mambo mengine, alizungumzia suala la kipengele cha Serikali tatu, akisema hapakuwa na jinsi ya kuepuka kipengele hicho, kwa sababu Katiba ya Jamhuri ya Muungano, tayari imevunjwa.

Kwamba, Zanzibar tayari wana Katiba yao inayowatambulisha kama nchi kamili, hatua ambayo inakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano, inayotambulisha Tanzania ni nchi moja yenye Muungano wa Zanzibar na Tanganyika.

“Sheria zipo wazi na hakuna haja ya kuzunguka katika suala hili, Katiba ya Jamhuri ya Muungano imevunjwa, leo hii Zanzibar wana Katiba inayotambulisha nchi yao na ukisema unataka Serikali mbili au moja, utakuwa unaizima Katiba ya Zanzibar, hivyo kukaribisha matatizo makubwa katika Muungano.

“Pia ikumbukwe kuna maoni mengine ya Serikali ya mkataba, ambayo nayo yanataka kuwapo makubaliano fulani tu kwenye mkataba wa Muungano na sehemu kubwa Zanzibar ibaki kama nchi kamili yenye kiti kwenye Umoja wa Mataifa(UN), sasa swali linakuja ni nani atasimamia mkataba huo? Yote haya tuliyazingatia na kuona ili kuunusuru Muungano, ni bora tufuate mfumo wa Serikali tatu kama utashi wa watu wengi ulivyotaka,” alisema.

Katika hatua nyingine, Jaji Ramadhan alisema, Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ilibaini suala la ukinzani wa kisheria kwamba, sheria zinazotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano, zinaweza kutupiliwa mbali kwa upande wa Zanzibar.

Akifafanua hoja hiyo, Jaji Ramadhan, alisema sheria zinazotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa upande wa Zanzibar inabidi zijadiliwe upya kwenye Baraza la Wawakilishi na wakati mwingine zinakataliwa, hivyo kujikuta sheria inafanya kazi upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano.

“Hivyo basi, kuweka kipengele cha Serikali tatu tumeangalia kwa umakini, kwanza matakwa ya wananchi wengi kutokana na utashi wao, pili ni kuudumisha Muungano kwa mujibu wa sheria ilivyotuelekeza na tatu ni kuweka usawa wa nchi zote mbili kuwa washirika wa Muungano, ili kuondokana na kero za Muungano ambazo mpaka leo tunakwenda kutimiza miaka 50 ya Muungano hazijatatuliwa,” alisema Jaji Ramadhan.

Jaji Ramadhan, alisema yeye na wajumbe wenzake wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, wamekiangalia kwa kina kipengele hicho kabla ya kukiingiza kwenye rasimu ya Katiba, hivyo anashangazwa na watu wanaokipinga kwa sababu ambazo hawajazitafiti.

Pia alisema kwamba, Tume ya Mabadiliko ya Katiba, imefanya kazi kwa kufuata muongozo wa sheria ya Mabadiliko ya Katiba Mpya, ambayo iliwaelekeza kwamba kazi yao isiathiri Muungano, hivyo anaamini kipengele cha Serikali tatu ni njia sahihi ya kuendelea kuudumisha.

Wakati Jaji Ramadhani akieleza hayo, zipo taarifa kuwa baadhi ya viongozi wastaafu wamepanga kukwamisha kipengele cha Serikali tatu, kabla au baada ya Bunge la Katiba.

Vigogo hao ni pamoja na Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, Mawaziri wakuu wastaafu, Cleopa Msuya na Edward Lowassa,    Rais Mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na Makamu wa Kwanza wa Rais katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Maalim Seif.

Kwamba viongozi hao wameelezea kutopendezwa na kipengele hicho, kwa sababu mbalimbali, ikiwamo suala la gharama za kuendesha mfumo huo na pia kupuuzwa kwa baadhi ya maoni yao.

Mkapa na Msuya, wamesikika wakisema kuwa gharama za kuendesha Serikali tatu zinaweza kuwa mzigo mkubwa kwa Serikali ya Tanganyika, huku Rais Mstaafu wa Zanzibar, Aman Abeid Karume na Makamu wa Kwanza wa Rais, katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Maalim Seif, wakilaumu mapendekezo ya Serikali tatu kwa kusema yanaikosesha Zanzibar mamlaka kamili na pia yanakiuka haki za Wazanzibar wengi waliopendekeza mfumo wa Serikali ya mkataba.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top