Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir, amesema kuwa jeshi limetibua njama ya mapinduzi dhidi ya serikali yake.
Rais Kiir amewalaumu wanajeshi wanaomuunga mkono
aliyekuwa naibu wake Riek Machar ambaye alifutwa kazi, kwa mapigano
yaliyozuka kati ya wanajeshi wake Jumapili usiku. Amesema kuwa serikali
sasa imedhibiti hali.
Akiongea na waandishi wa habari,
Bwana Kiir alisema serikali imedhibiti hali huku ikitangaza sheria ya
kutotoka nje nyakati za usiku.
Wanajeshi mahasimu, walipigana vikali kwa masaa kadhaa na inaarifiwa kuna majeruhi kadhaa huku mamia wakitoroka mji wa Juba..
Kwa sasa milio ya risasi imekwisha. Kumekuwa na
hali ya taharuki nchini Sudan Kusini tangu mwezi Julai wakati Rais Kiir
alipowafuta kazi mawaziri wake akiwemo bwana Machar.
Wito wa utulivu
Awali Umoja wa Mataifa ulitoa wito wa utulivu
nchini Sudan Kusini baada ya kuzuka mapigano kati ya vikosi vya jeshi
katika mji mkuu Juba.
Umoja huo pia ulisema kuwa ni jukumu la Viongozi nchini humo kuitisha utulivu.
Kwa mujibu wa mwakilishi maalum wa katibu mkuu
wa Umoja wa Mataifa, Hilde Johnson, pande zinazozana zimetakiwa
kusitisha mapigano haraka iwezekanavyo.
Alisema amekuwa akishauriana na viongozi wa taifa hilo wakiwemo viongozi mkuu kuhakikisha kuna utulivu.
Milio ya risasi ilisikika usiku kucha hadi
asubuhi ya leo katika mji mkuu wa Sudan Kusini Juba kwa mujibu wa
maafisa wa balozi na wengine waliohsuhudia tukio hilo.
Inaarifiwa mapigano hayo yametokea kati ya walinzi wa Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir.
Mapigano yanasemekana yalianza saa nne usiku wa
kuamkia leo katika kambi kuu kuu za jeshi mjini Juba na kuendelea kuwa
makali kwa karibu saa moja kabla ya kundi moja kufurushwa.
Milio ya risasi ilisikika usiku kucha na kusababisha hali ya taharuki huku wananchi wakizuiwa kutoka nje.
Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, taarifa
kutoka katika balozi za Marekani na Uingereza mjini Juba, zimetaka raia
wa nchi zao kujizuia na kutoka nje.
Ubalozi wa Marekani umesema kuwa duru mbali
mbali zinaarifu mapigano makali ya ufyatulinaji wa risasi yamesikika
katika sehemu mbali mbali mjini Juba.
Mwandishi wa habari wa shirika la AFP amesema
kuwa aliona wanajeshi waliokuwa wamejihami vikali wakishika doria katika
barabara za Juba mapema asubuhi ya leo makabiliano makali yakiendelea
katika kambi za jeshi.
Hata hivyo hakuna taarifa rasmi kutoka kwa jeshi kwani huduma za simu zimesemekana kutatizika.
Duru za kiijeshi zilisema kuwa makabiliano
yalizuka kati ya kikosi cha jeshi cha Tiger, wakati moja ya kikosi
ambacho kina wanajeshi wengi wa kabila la Nuer kushuku kuhusu muundo wa
kikosi kingine cha jeshi ambacho wanajeshi wake wengi ni wa kabila la
Dinka na hivyo kuanza kugombana kiasi cha kuanza kufyuatuliana risasi.
Inaarifiwa wanajeshi hao wa Nuer wamewafukuza
wenzao wa Dinka ambao wengi wao walifuzu hivi karibuni na kuajiriwa
katika serikali ya Rais Kiir.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment