Tanzania
iko mbioni kukabiliwa na mgogoro mkubwa wa kikatiba. Tayari mabadiliko
ya katiba ya Zanzibar yanakinzana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya 1977 lakini hayakinzani na sheria mama ambayo ni makubaliano
ya Muungano (Articles of the Union).
Ili kukabiliana na
changamoto ya kupata katiba mpya, kuwa na daftari safi la wapiga kura,
kuunda Tume huru ya uchaguzi, na kuwa na uchaguzi ulio huru na wa haki
2015, Rais Kikwete baada ya kushauriana na wadau mbalimbali aunde
serikali ya umoja wa kitaifa.
Serikali ya Umoja wa Kitaifa pia
iimarishe uwajibikaji wa vyombo vya dola na viongozi, ishughulikie
kadhia ya matumizi mabaya ya fedha za umma na iimarishe ukusanyaji wa
mapato serikali ili miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa barabara na
ufuaji wa umeme iweze kukamilishwa.
Mchakato wa Katiba mpya
unapaswa kuwapa wananchi matumaini ya kujenga Tanzania mpya yenye haki
sawa kwa wote na itakayojenga uchumi ambao hatua kwa hatua, utaleta
neema kwa wananchi wote. Katiba itamke wazi rasilimali na maliasili ya
nchi itatumiwa kwa manufaa ya wananchi wote na vizazi vijavyo.
Uandikaji
wa katiba mpya ni fursa adhimu ya kujenga muafaka wa kitaifa unaowapa
imani na matumaini wananchi kuwa mfumo wa utawala, siasa na uchumi
unaowekwa na katiba unalinda maslahi yao na utawaletea maendeleo
wayatakayo.
Mchakato wa kupata katiba mpya kabla ya 2015 una
vikwazo vingi. Ni wazi Katiba Mpya haiwezi kapatikani ifikapo tarehe 26
Aprili 2014 wakati tunasheherekea miaka 50 ya Muungano. Rasimu ya mwisho
ya Tume ya Katiba itapatikana mwezi huu. Rais anawajibika kukamilisha
uundaji wa Bunge la Katiba kwa kuteua wabunge 201 baada ya kupata
mapendekezo toka wadau mbali mbali vikiwemo vyama vya siasa, vyama vya
wafanyakazi, vyama vya wakulima, taasisi za dini na kadhalika. Itakuwa
bahati kama Bunge la katiba litaweza kuanza shughuli zake katika ya kumi
la mwisho la mwezi wa Januari.
Tume ya Jaji Warioba imefanya
kazi kubwa ya kuratibu maoni na kuja na mapendekezo ya katiba mpya
ambayo hayakushinikizwa na matakwa ya Chama tawala cha CCM. Mwanazuoni
na mchambuzi wa mambo ya katiba na sheria Prof. Chris Maina Peter
amediriki kuita Rasimu ya Katiba kuwa Mapinduzi ya kimya kimya. Tume
imeonyesha ujasiri mkubwa na uhuru wake hasa ukizingatia pendekezo kuu
la Rasimu ya Katiba ni mfumo wa serikali tatu (Sura ya sita ibara ya 57 –
66) ambao unakinzana na msimamo rasmi wa Chama tawala cha CCM na wosia
wa hayati Mwalimu Nyerere kuhusu mfumo wa Muungano.
Rasimu ya
Katiba ina mabadiliko makubwa ya msingi ikiwa ni pamoja na mfumo wa
Muungano wa serikali tatu, kupunguza mambo ya muungano kutoka 22 na kuwa
saba, kuruhusiwa mgombea binafsi, Rais kutangazwa kushinda akipata
zaidi ya asilimia 50 ya kura zote zilizopigwa la sivyo uchaguzi urudiwe
kwa wale wawili walio ongoza kwa kura, haki ya wananchi kumuondoa Mbunge
wao madarakani, Ukomo wa vipindi vitatu vya mtu mmoja kuwa mbunge,
Tume huru ya uchaguzi, Mawaziri kutokuwa wabunge, Spika kutokuwa mbunge,
haki za watu wenye ulemavu, kupanuliwa kwa haki za binadamu, kuondolewa
kwa viti maalum vya wanawake na badala yake kila jimbo kuwa na mbunge
mwanamke na mbunge mwanaume,
Kuanzishwa kwa Mahakama ya Juu
(Supreme Court), haki ya kumiliki mali na hifadhi ya mali haitahusu mali
iliyothibitishwa kwamba haikupatikana kwa njia halali na mengine
mengi.
Hata hivyo mambo mengi muhimu kama vile umilikaji wa ardhi,
maliasili na rasilimali za nchi kutumiwa kwa manufaa ya wananchi wote,
elimu, afya, mazingira ya kukuza uchumi unaoleta neema kwa wananchi
wote, wajibu, uwezo na uhuru wa serikali za mitaa hayajaingizwa ndani ya
katiba kikamilifu kwani rasimu ya katiba imeshughulikia mambo ya
muungano. Hoja ya Tume ya Jaji Warioba ni kuwa mambo haya yataingizwa
kikamilifu katika katiba ya washiriki wa Muungano – Tanzania Bara na
Zanzibar.
Bila kuwepo kwa rasimu ya katiba ya Tanzania Bara na
Marekebisho ya katiba ya Zanzibar isikinzane na Katiba ya Muungano,
zoezi la kupata dira na mwongozo wa kusimamia utawala, uchumi na siasa
za Watanzania haujakamilika. Walau Zanzibar wana katiba lakini
Tanganyika haina katiba wala mchakato wa kuipata katiba hiyo haujaanza.
Isitoshe rasimu ya Katiba ya Muungano ina mapungufu makubwa na kuna
mambo mengi kama vile mfumo wa Muungano, Mambo ya Muungano, Ukuu wa
Katiba ya Muungano, Mapato ya kugharamia Muungano yanahitaji mjadala wa
kina ili kufikia Muafaka.
Bunge la Katiba litakuwa na kazi
kubwa ya kupata muafaka kuhusu mambo haya muhimu. Hata wakifikia muafaka
na kupata katiba mpya, mapendekezo yaliyomo katika Rasimu ya Katiba
yatahitaji mabadiliko makubwa ya kisheria na kitaasisi ili kuweza
kuitekeleza katiba mpya. Kenya ilikamilisha katiba yake na kuipitisha
kwenye kura ya maoni Agosti 2010. “Hata hivyo, mabadiliko mbali mbali ya
kisheria na kitaasisi kwa ajili ya utekelezaji wa Katiba hiyo
yalichukua zaidi ya miaka miwili na nusu hadi Uchaguzi Mkuu wa mwezi
Machi, 2013.”
Wengi wetu tungependa zoezi la kupata katiba mpya
likamilike kabla ya uchaguzi mkuu wa 2015. Hali halisi ni wazi zoezi
hilo haliwezi kukamilika kwa ufanisi kabla ya 2015. Sheria ya mabadiliko
ya katiba inaeleza kuwa ikiwa katiba mpya haikupitishwa kwenye kura ya
maoni, katiba ya sasa itaendelea kutumika.
Mchakato wa kupata
katiba mpya, maoni yaliyotolewa na wananchi na rasimu ya katiba
inayotokana na maoni hayo imebainisha wazi Watanzania hawaitaki katiba
ya sasa. Kufanya uchaguzi kwa kutumia katiba ya sasa na Tume ya Uchaguzi
iliyopo hakutakubalika na wananchi na kunaweza kuwa chanzo cha mgogoro
mkubwa wa kisiasa.
Kura ya maoni inakabiliwa na kikwazo kikubwa cha
kutokuwepo kwa daftari la kudumu la wapiga kura lililoandikisha wapiga
kura wote. Daftari la wapiga kura halijaboreshwa na kuandikisha wapiga
kura wapya baada ya uchaguzi mkuu wa 2010.
Mwezi Februari Rais
Kikwete alitangaza kuwa vitambulisho vya kitaifa ambavyo vinatumia
alama ya mwili ndivyo vitakavyotumiwa kwa kupigia kura ya maoni na
uchaguzi mkuu. Alieleza mamlaka ya vitambulisho vya taifa itashirikiana
na Tume ya Uchaguzi katika utoaji wa vitambulisho vya kitaifa ambavyo
pia vitakuwa vitambulisho vya kupigia kura.
Zoezi la kuwapa
wananchi vitambulisho vya kitaifa linaenda taratibu sana. NIDA
haijakamilisha kutoa vitambulisho hivyo hata kwa wilaya za Dar es
Salaam. Kwa kasi hii ya uandikishaji na utoaji wa vitambulisho vya
kitaifa, zoezi hili halitakamilika katika miaka miwili inayokuja.
Itafika 2015 na wananchi wengi wenye umri wa miaka 18 watakuwa
hawajapata vitambulisho vya taifa.
Vitambulisho vya NEC
havikidhi mahitaji. Vitambulisho hivyo vinaghushiwa kwa urahisi sana.
Wadau wengi hawana imani na daftari la NEC. Ni vyema vitambulisho vya
NIDA vyenye alama za mwili ndivyo vitumiwe kama vitambulisho vya kupigia
kura.
Kura ya maoni kuhusu katiba haiwezi kuendeshwa kwa
ufanisi bila kuwa na daftari la wapiga kura linaloaminika. Kura ya maoni
inabidi ipigwe na wananchi wa pande mbili za Muungano. Tume ya Uchaguzi
ya Taifa inatumia Tume ya Zanzibar kuwa wakala na daftari la ZEC
kubaini wapiga kura wa Zanzibar. Daftari la ZEC linawanyima wananchi
wengi wa Zanzibar kuandikishwa kupiga kura kwa madai kuwa hawana
vitambulisho vya ukaazi.
Tume ya Taifa itawajibika kuwaandikisha Wazanzibari hawa wapate haki ya kupiga kura ya maoni kuhusu katiba.
Ili kusimamia vizuri mchakato wa kupata katiba mpya na kuhakikisha
kuwepo kwa maridhiano na mshikamano wa kitaifa katika kipindi hiki nyeti
ninamshauri Rais Kikwete aunde serikali ya umoja wa kitaifa.
Jukumu kubwa la serikali hiyo iwe kukamilisha mchakato wa kupata katiba
mpya, kuunda Tume Huru ya Uchaguzi, kuandikisha wananchi wote
wanaostahili kupiga kura wapewe vitambulisho vinavyotumia alama ya mwili
ili kuhakikisha uchaguzi wa 2015 unakuwa huru na wa haki.
Serikali ya umoja wa kitaifa pia iimarishe utendaji wa serikali,
ipambane na ubadhirifu ulioainishwa na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za
Serikali na Kamati za Bunge, ianzae kujenga utamaduni wa uwajibikaji na
kutumia vizuri fedha za umma kwa maendeleo ya wananchi.
Ibrahim Haruna Lipumba Mwenyekiti, Jumapili, 15 Disemba 2013.
0 comments:
Post a Comment