Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimemtupia mpira Rais Jakaya Kikwete
wa kuamua hatima ya mawaziri saba, wanaotuhumiwa kushindwa kutekeleza
majukumu yao.
Mawaziri hao waliotajwa ni ‘mzigo’ kwa Serikali
juzi walihojiwa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM chini ya
Mwenyekiti wake Rais Kikwete, ambapo jana Katibu wa Itikadi na Uenezi wa
chama hicho, Nape Nnauye alisema wamemshauri Rais Kikwete mambo matatu;
kuwafukuza, kuwahamisha wizara au kuwahimiza wafanye kazi.
“Kamati Kuu imetoa maazimio saba ambayo yote
yanazihusu wizara saba zinazoongozwa na mawaziri hao. Tumemshauri Rais
Kikwete, yeye ndiye ataamua nini cha kufanya kwa sababu ndiye
aliyewateuwa mawaziri hao,” alisema Nape.
Wakiwa Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma katika
ziara ya chama hicho, Nape pamoja na Katibu Mkuu wa chama hicho,
Abdulrahman Kinana aliwatupia lawama mawaziri hao wakati wakielezea
changamoto zinazowakabili wakulima ambao ni asilimia 80 ya Watanzania,
huku mawaziri husika wakikaa kimya.
Nape alisema mawaziri hao waliitwa kuhojiwa na
kutakiwa kutoa maelezo ya masuala yaliyoibuliwa wakati wa ziara hiyo
ambayo pia iliwahusisha baadhi ya wajumbe wa Sekretarieti.
Katika maelezo yake kwa waandishi wa habari jana,
Nape aliwataja mawaziri hao kuwa ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya
Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika
Christopher Chiza, Naibu Waziri wa Fedha Saada Mkuya (alihojiwa kwa
niaba ya Waziri wa Fedha Dk William Mgimwa).
Wengine ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk
Abdallah Kigoda, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo
David, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma,
Celina Kombani na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia.
Sakata la kutaka mawaziri ‘mizigo’ kutoswa
limekuwa likiibuliwa na wabunge mbalimbali katika mikutano ya Bunge
mjini Dodoma, huku baadhi wakipendekeza hata Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
naye atoswe kutokana na kushindwa kuwasimamia mawaziri.
Ushauri wa CCM kwa JK
Nape alisema kuwa kazi ya Kamati Kuu ni kushauri,
“Kazi yetu ni kushauri na siyo kufukuza. Rais Kikwete ndiye amewateua
mawaziri hao, ameupokea ushauri na yeye ndiye mwenye uwezo wa
kuwafukuza, kuwahamisha au kuwasukuma watende kazi. Hiyo siyo kazi yetu”
Alipobanwa zaidi kueleza ushauri ambao Kamati Kuu
ilimpa Rais Kikwete Nape alisema, “Kuna ushauri mwingine ambao tumempa
Rais Kikwete hatuwezi kuuweka hadharani.”
Alisema kuwa wakati wa kuhojiwa kila waziri
alikuja na majibu yanayoihusu wizara yake kutokana na udhaifu ulioelezwa
na wananchi.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
“Katika kikao kijacho cha Kamati Kuu moja ya mambo
yatakayojadiliwa ni pamoja na kuangalia utekelezaji wa mambo saba
tuliyoishauri Serikali kupitia hizo wizara saba,” alisema.
Nape alisema kuwa walipoeleza udhaifu wa mawaziri
hao hawakueleza kuwa ni mzigo kwa Serikali, bali walilenga kueleza
upungufu wao katika kusimamia masuala mbalimbali.
“Mfano Waziri wa Kilimo kwa miaka minne hajawahi
kwenda mkoani Ruvuma ambako kuna ghala la chakula pia hajawahi
kushughulikia matatizo yanayowakabili wakulima wa korosho na mahindi,”
alisema.
Hata hivyo, Nape alisema kuwafukuza mawaziri siyo
dawa na kuweka mambo sawa kwa maelezo kuwa wakati mwingine utendaji kazi
ndani ya Serikali unakwenda ovyo kwa sababu ya mfumo na sheria mbovu.
“Watu wanadhani ushauri tuliompa Rais Kikwete ni
kuwafukuza mawaziri, wakati mwingine kufukuza siyo mwisho wa suluhisho.
Kwa mfano tumebadili mawaziri Tamisemi lakini kila mwaka ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inaonyesha udhaifu katika wizara hiyo,” alisema Nape.
Kwa mfano tumebadili mawaziri Tamisemi lakini kila mwaka ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inaonyesha udhaifu katika wizara hiyo,” alisema Nape.
Maagizo
Nape alisema agizo la kwanza ni kuhusu kilimo cha
pamba ambapo Kamati Kuu iangalie upya Serikali ipitie upya upatikanaji
wa pembejeo za ruzuku kwa wakulima wa pamba nchini.
Alisema kuwa kuhusu kilimo cha mkataba kwa
wakulima wa pamba, Serikali imetakiwa kuratibu utaratibu wa kilimo hicho
ikiwamo kutowalazimisha.
“Kwa mfano Waziri husika hajafika kwa muda wa
miaka minne na nusu mkoani Ruvuma ambako ndiko kuna ghala la chakula na
tulipofika Tunduma tulikuta foleni pale mizani huku watumishi wakiwa
wanafanya kazi kwa saa tisa, lakini baada ya kueleza udhaifu huo sasa
wanafanya kwa saa 24,” alisema.
Aliongeza, “Chama kimeiagiza serikali
kutowalazimisha wakulima kutumia mbegu ya Quiton, badala yake elimu
itumike zaidi badala ya nguvu.”
Alisisitiza kuwa Kamati Kuu imeitaka Serikali
kuangalia upya urasimu katika uwekezaji wa viwanda nchini, hasa
vinavyoongeza thamani ya mazao na kutoa ajira.
Kwa upande wa wakulima wa korosho, Nape alisema
kuwa Kamati Kuu imeisisitizia serikali kujipanga kutatua tatizo la
korosho na kuhakikisha inabanguliwa nchini.
“Serikali inatakiwa kuangalia upya orodha ndefu ya makato kwa
wakulima hasa wa korosho na vyama vya msingi au mamlaka zinginezo, ili
kuondoa makato yasiyo ya lazima na kuongeza kipato cha mkulima,”
“Kuhusu pembejeo za ruzuku Kamati Kuu imepokea
taarifa ya malalamiko ya wakulima juu ya ufanyaji kazi wa mbolea ya
Minjingu na kuagiza wananchi wawe huru kutumia mbolea wanayoitaka badala
ya kulazimishwa,” alisema.
Kwa upande wakulima wa mahindi alisema kuwa
serikali imetakiwa kumalizia malipo yaliyobaki na kuhakikisha
wanakomesha utaratibu wa kuwakopa wananchi mazao yao bila kuwalipa.
“Utaratibu uwekwe wa kufanya tathmini mapema ya
mahitaji na uwezo wa kununua mahindi wa serikali ili kuepusha utaratibu
wa kuchukua mahindi ya wakulima bila kuwalipa,”alisema.
Nnauye alisema kwa upande wa madai ya walimu
Kamati Kuu imeiagiza Serikali kukamilisha uhakiki wa madai ya walimu na
kuwalipa haki zao ikiwamo kuhakikisha madeni hayazaliwi tena.
Kamati hiyo pia imekemea watendaji wachache wanaojihusisha na ubadhirifu kwenye halmashauri mbalimbali nchini.
“Serikali imeshauriwa kuangalia upya sheria kama
zinakidhi mahitaji ya wakati na mazingira ya sasa ili kuongeza uwezo wa
udhibiti na kuokoa pesa za walipakodi zinazopotea kwa walafi wachache
kwenye halmashauri mbalimbali nchini,” alisema Nnauye.
Kwa upande wa matatizo ya upatikanaji wa maji safi
na salama serikali imeagizwa kufanya mkakati wa makusudi na wa dharura
kulitafutia ufumbuzi wa haraka na wa kudumu tatizo hilo ikiwamo
kuangalia upya utaratibu uliotumika kuwamilikisha watu wachache maeneo
makubwa ya ardhi, ambao wameshindwa kuyaendeleza badala yake wanayatumia
kuwakodishia wakulima wadogo.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment