Rais wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini Hayati
Nelson Mandela amezikwa katika kijiji cha Qunu mkoa wa Cape Mashariki
nchini Afrika Kusini.
Mjane wa Mandela Graca Machel pamoja na Rais wa
Afrika Kusini Jacob Zuma walikuwepo katika hafla ya mazishi
iliyohudhuriwa na jamaa za karibu wa familia ya Mandela pamoja na
viongozi wengine wakuu.
Takriban watu 4,500 ikiwemo wageni
wa kimataifa walihudhuria mazishi hayo ambayo yalikuwa ya mchanganyiko
wa tamaduni za kale na mambo ya kisasa.
Familia ya Mandela ilikesha wakijiandaa kwa mazishi hayo.
Kiongozi mmoja wa kitamaduni aliita mizimu ya
mababu wa kale na pia wakiongelesha mwili wa Mandela kumwambia kuwa sasa
anazikwa. Ni kuambatana na tamaduni na mila za watu wa ukoo wa Mandela
wa Thembu.
Viongozi wa Afrika, familia na marafiki walitoa
heshima zao za mwisho kwa hayati Nelson Mandela katika mazishi yake ya
kitaifa katika kijiji cha Qunu katika mkoa wa Cape Mashariki.
Mandela
alikuwa rais wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini.
Rais Jacob Zuma alisema kuwa safari ndefu ya
Mandela kuelekea uhuru imekwisha lakini raia wa Afrika Kusini wana
jukumu la kuendeleza sera zake na urithi wake.
Mandela alifariki tarehe 5 mwezi Disemba akiwa na umri wa miaka 95.
Siku ya kumi na ya mwisho ya maombolezi kufuatia
kifo cha Mandela, imekamilishwa na Mandela kupigiwa mizinga 19 na jeshi
huku mwili wake ukizikwa katika kijiji cha Qunu. Mishumaa 95 iliwashwa
kila mmoja ikiwa ishara ya miaka ya Mandela.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment