Kutoka kushoto: Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye akisikiliza hotuba wakati wa ibada ya kumkumbuka mpigania haki mashuhuri na Rais wa zamani wa Afrika Kusini Nelson Mandela. Aliyeketi kulia kwake ni Mwanasiasa Mkongwe Kingunge Ngombale Mwiru, akifuatiwa na Balozi wa Algeria hapa nchini, Djelloul Tabet na mwakilishi wa watu wa Palestina, Nasir Abujaish.
 
Wasomi na watu mbalimbali wamesema katika  kumwenzi Rais wa Kwanza Mzalendo wa Afrika Kusini, Hayati Nelson Mandela ni kutekeleza yote aliyofanya kwa vitendo siyo kuomboleza kwa kulia.
 
Pia, walisema viongozi wa Bara la Afrika wanatakiwa kutambua kuwa uongozi ni dhamana ya wananchi na hawana budi kuepuka kutumia madaraka kujineemesha wao na familia zao.
Hayo yalisemwa jana wakati wa kumbukumbu ya Mandela, iliyoandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na kuhudhuriwa na watu mbalimbali wakiwamo  wasomi, wanasiasa na  mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini.
Kada wa CCM, Kingunge Ngombale–Mwiru alisema wanatakiwa kumuenzi Mandela kwa kufanya kwa vitendo mema aliyoyaacha ambapo alisema viongozi hawatakiwi kuhuzunika na kulia,  kwani aliyofanya Mandela yanatosha kusherehekea siyo kuhuzunika.
Alisema baada ya kifo cha Mwalimu Julius Nyerere kila mtu alihuzunika na kuongea mambo mengi, lakini hakuna aliyetekeleza kwa vitendo aliyofanya.
“Ukiangalia viongozi wa zamani na sasa wana tofauti kubwa.  Viongozi wetu wa sasa wakipata madaraka wanajifikiria wao kwanza badala ya wananchi,” alisema.
Naye Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye alisema tatizo lililopo bara la Afrika, ni suala la Uongozi na Utawala Bora vitu ambavyo vikifuatwa na kuzingatiwa vitasadia maendeleo.
“Ukishakuwa na uongozi  na utawala bora, yale mambo ya kienyeji hayatakuwapo hivyo kila mmoja anatakiwa kuiga aliyofanya Mandela na Nyerere, tutaibadili Afrika,” alisema Sumaye.
Balozi wa Palestina nchini, Dk Nasri Abu Jaish alisema kifo cha Mandela siyo pigo kwa wananchi wa Afrika Kusini na Afrika pekee,  bali dunia nzima kwa sababu ni mwalimu wa dunia.  “Alikuwa mwalimu kwa viongozi, hakuwabagua watu, aliwaunganisha na kusaidia nchi zingine,” alisema.
Mwananchi 
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top