
Rais Uhuru Kenyatta
Kesi inayomkabili Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta huenda
ikachelewa kuanza baada ya mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya
kimataifa ya uhalifu wa jinai (ICC) Kukiri kuwa hana ushahidi wa kutosha
wa kuendeleza kesi hiyo.
Rais wa Kenya amekanusha mashtaka ya dhuluma
dhidi ya ubinadamu zinazohusiana na ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa
mwaka 2007 ambapo zaidi ya watu elfu moja waliuawawa katika mapiganao hayo na
maelfu ya wengine kupoteza makazi yao.
Katika
taarifa kwa vyombo vya habari Bi. Fatou Bensouda amesema kuwa uamuzi
huo unatokana na mashahidi wawili wakuu katika kesi hiyo kukataa kutoa
ushahidi dhidi ya Rais Kenyatta.
Mmoja wao amesema kuwa hayuko radhi
kusema anayojua kuhusu kesi hiyo ilhali wa pili amesema kuwa alidanganya
katika ushahidi wake wa awali katika kesi hiyo.
Kujiondoa kwa mashahidi hao imemfanya kiongozi
wa mashtaka kusema kuwa kesi dhidi ya Bwana Kenyatta haifikii kiwango
cha ushahidi kinachohitajika jambo lililomchochea kuomba kesi hyo
isimamishwe kwa muda ili aweze kusawazisha na kukusanya ushahidi zaidi.
Kesi ya Bwana Kenyatta ilipaswa kuanza huko The
Hague tarehe 5 Februari mwaka ujao. Bwana Kenyatta alishtakiwa pamoja
na naibu wake William Ruto na mtangazaji Joshua Arap Sang kwa makosa ya
mauji, kusababisha watu kuhamishwa kwa nguvu katika makazi yao,
kusababisha mateso kwa umma na ubakaji kufuatia ghasia zilizotokana na
matokeo ya urais katika uchaguzi huo.
Kesi ya Kenyatta na naibu wake imekuwa
ikifuatiliwa kwa karibu na jamii ya kimataifa haswa baada ya Umoja wa
Afrika kutishia kuyaondoa mataifa ya Afrika katika uanachama wa mahakama
hiyo iliyobuniwa chini ya mkataba wa Roma. Umoja wa Afrika umekuwa
ukidai mahakama hiyo imekuwa ikiwalenga viongozi wa bara Afrika.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment