Wanamgambo wa kundi la anti-balaka, Jamhuri ya Afrika ya Kati
Takriban watu elfu moja wameuawa na waasi wa zamani
nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati katika mapambano yaliyodumu kwa siku
mbili yaliyojitokeza mwezi huu, makadirio haya yanazidi yale ya Umoja wa
Mataifa. Shirika la Amnesty International limesema.
Shirika hilo limesema kuwa uhalifu wa kivita bado unaendelea kufanyika nchini humo.
Wapiganaji hao ambao wengi wao ni
Waislamu walimuondoa madarakani aliyekuwa rais wa taifa hilo, Francois
Bozize mwezi March, hali iliyosababisha mgogoro ndani ya jamii nchini
humo.
Kiongozi wa waasi Michel Djotodia hivi sasa ni
kiongozi wa kwanza kutoka jamii ya Waislamu anayeongoza taifa lenye
Wakristo wengi na ndiye kiongozi wa mpito wa Jamhuri ya Afrika ya kati.
Katika ripoti hiyo, Amnesty International
imesema waasi wa zamani wa Seleka waliwaua takriban watu 1000 mjini
Bangui, kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kulipa kisasi dhidi ya wapiganaji
wa Kikristo wanaodaiwa kuwashambulia waasi wa Kiislam.
Idadi ya waliopoteza maisha imeelezwa kuongezeka
kuliko ile iliyotolewa na Umoja wa Mataifa ambao ulisema watu 450
waliuawa mjini Bangui na wengine 150 sehemu nyingine nchini humo.
Mashambulio hayo yamekuja baada ya wanamgambo
wajulikanao kwa jina la anti-balaka ambao walikuwa wakiingia kila nyumba
na kuwaua watu 60 wa jamii ya Kiislamu. Amnesty International imeeleza.
Mashambulio yaliyofanywa na wanamgambo wa zamani
wa Seleka yamehusisha mauaji pia uvamizi na uporaji katika nyumba za
raia,ambapo wanawake na watoto kadhaa wameuawa.
Shirika hilo limesema kuwa raia huuawa kila siku
mjini Bangui, ingawa kumekuwepo na vikosi vya Ufaransa na Umoja wa
Afrika, Ufaransa ikiwa na askari 1,600 nchini humo.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human
Rights Watch limesema wapiganaji wa Kikristo walishambulia jamii ya
kiislamu kaskazini mwa mji wa Bossangoa na kuwachinja watoto huku
wakiwashinikiza wazazi wao kushuhudia mauaji hayo.
Mwanzoni mwa mwezi huu, Rais Djotodia aliiambia
redio ya Kifaransa kuwa yuko tayari kuzungumza na viongozi wa wanamgambo
wa Kikristo ili kutatua mzozo huo.
Kauli hiyo imekuja baada ya Umoja wa Afrika kuidhinisha kuongeza vikosi vyake na kufikia askari 6,000.
Vikosi vya Umoja wa Afrika na vya Ufaransa vinafanya jitihada za kuwanyang'anya silaha wanamgambo hao.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment