Wananchi wa Sudan Kusini wakihofia mapigano
Jeshi la Sudan Kusini limesema waasi wa Sudan Kusini wameutwaa mji muhimu, wa Bor uliopo kilomita 200 kaskazini mwa Juba, wakati mapigano yakiendelea baada ya kuripotiwa kwa jaribio la kupindua serikali Jumapili.

"Askari wetu wamepoteza udhibiti kwa wapiganaji wa Riek Machar," amesema msemaji wa jeshi Philip Aguer.

Rais Salva Kiir amemshutumu Bwana Machar, makamu wa rais wa zamani, kwa kupanga jaribio hilo la mapinduzi, madai ambayo ameyakanusha.

Hali hiyo ya mapigano yaliyoanza katika mji mkuu Juba, tayari yamesababisha watu 500 kuuawa na kuleta wasiwasi wa kutokea kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Umoja wa Mataifa umetaka mgogoro huo umalizwe kwa njia ya mazungumzo ya kisiasa, na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema watu wapatao 20,000 wamepata hifadhi katika viwanja vya Umoja wa Mataifa mjini Juba.

Uingereza na Marekani zimetuma ndege zao kuwaondoa raia wao kutoka Sudan Kusini, na afisa mmoja wa wizara ya ulinzi wa Marekani ameelezea hali hiyo ya mapigano kuwa inaelekea kuwa mbaya.

Tangu uhuru, makundi kadha yamekuwa yakipigana dhidi ya serikali ya Sudan Kusini. Haijabainika iwapo mojawapo ya makundi haya yamehusika katika kuuteka mji wa Bor.

Siku ya Jumatano, meya wa mji wa Bor, Nicholas Nhial Majak, aliiambia BBC kuwa ghasia hizo zimesambaa hadi mji wa Bor, kilomita mia mbili kutoka Juba.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top