Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera Uratibu na Bunge), William Lukuvi
HATUA ya Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya (CCM) kusukuma
mashambulizi mazito na kuwatuhumu baadhi ya majaji wa Mahakama Kuu,
watumishi wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) na Idara ya
Mahakama kwa madai ya kushirikiana na wauzaji wa dawa za kulevya,
imezua mshituko mkubwa miongoni mwa jamii.
Katika hoja yake binafsi bungeni juzi, Bulaya alisema baadhi ya
watumishi katika ofisi hizo wamekuwa wakishirikiana na watu
wanaokamatwa na dawa za kulevya kwa kuwapa siri na mbinu za kuharibu
ushahidi ili washinde kesi.
Bulaya alisema: “Kutokana na kupanuka kwa mtandao huu wa kuhujumu,
licha ya kushirikiana na washitakiwa, mtandao uliopo katika ofisi hiyo
ya DPP umekuwa ukituhumiwa kufanya njama za kushirikiana na baadhi ya
watumishi wa mahakama, hasa majaji kuhamisha kesi kupeleka kwa majaji
ambao wanadaiwa kuhusika na mtandao huu.”
Wadadisi wa mambo wamedai kuwa hatua ya Bulaya ni ya ujasiri na
ameyaweka rehani maisha yake kutokana na uzito wa suala hilo ambalo
limekuwa likiitesa serikali kwa muda mrefu.
Wamedai kuwa mbunge huyo ameonyesha ujasiri wa hali ya juu, na kwamba
kwa kila namna amewatisha vigogo wanaodaiwa kuhusika na biashara hiyo,
hivyo kama asipolindwa na serikali maisha yake huenda yakawa hatarini.
Hofu ya wadadisi wa mambo inatokana na ukweli kwamba, mbunge mwingine
kijana wa CCM, Amina Chifupa, alikufa miezi michache tu baadaye baada
ya kuchachamalia bungeni akiitaka serikali kutaja majina ya wauza ‘unga’
hadharani, huku yeye mwenyewe akiweka bayana kuwa yuko tayari kumtaja
hata mumewe, Mohamed Mpakanjia, ikiwa atagundua kuwa anafanya biashara
hiyo.
Katika Bunge lililopita, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera Uratibu na Bunge), William Lukuvi, wakati akijibu hoja za baadhi
ya wabunge kuhusiana na kutaja majina ya watu wanaotuhumiwa kuhusika
na biashara hiyo, aliweweseka akisema kuwa halitakuwa jambo jema kutaja
majina, na kwamba kama serikali ikikubaliana na hoja za wabunge,
hakuna kati yao atakayepona.
Kadhalika, uzito wa hoja hiyo, umedhihirika pia kutokana na kukwama
kwa miaka kadhaa sasa kwa Rais Jakaya Kikwete kuweka wazi majina
aliyodai kuwa nayo ya watu wanaotuhumiwa kuhusika na biashara ya dawa
za kulevya.
Juzi akiongea kwa kujiamini, Bulaya alitoa mfano wa namna washitakiwa
wawili raia wa Pakistan walivyotoroka nchini wakiwa nje ya dhamana.
Aidha, katika kesi ya Mwinyi Rashid Ismail Mkoko (KLR /IR 4143/2011),
mshitakiwa aliomba dhamana Mahakama Kuu wakati kesi ilikuwa bado ipo
Mahakama ya Kisutu ndipo wakili wa serikali akamwambia jaji kuwa
anaomba kuifuta.
Alisema jaji huku akifahamu kuwa kesi hiyo imefika mbele yake kwa
ajili ya kusikiliza maombi ya dhamana tu, na kuwa ilikuwa haijafikishwa
Mahakama Kuu kwa utaratibu wa sheria, aliamua kumfutia kesi mshitakiwa
na kuamuru kuwa yuko huru.
Sambamba na hilo, katika kesi Na. 794/2011 katika Mahakama ya Wilaya
ya Ilala, hakimu aliwafunga kifungo cha nje kwa miezi 15 washitakiwa,
Abdulrahman Shaban Sindanema, Said Nassoro Khamis na Abdulrahim Haroub
Said waliokiri kosa la kuuza na kusambaza dawa za kulevya aina ya
heroin.
Kwa mujibu wa Bulaya adhabu iliyotolewa na hakimu huyu, haipo kwa
mujibu wa sheria. Kwa mujibu wa kifungu cha 16 cha sheria ya kuzuia
dawa za kulevya, adhabu iliyowekwa kwa wauzaji au wasambazaji wa dawa
za kulevya ni kifungo cha maisha na si chini ya miaka ishirini jela kwa
kipindi hicho.
Alitoa mfano wa kesi nyingine kuwa ni Na. 274/2005, Jamhuri dhidi ya
Yusuph Hashim Nyose, aliyekamatwa na kilo 1.3 za dawa za kulevya aina
ya heroin alizokuwa amemeza na kisha kuzitoa kupitia njia ya haja kubwa
baada ya kukamatwa na zilikuwa na thamani ya shilingi 12,600,000.
Pamoja na ushahidi uliotolewa mahakamani na mashahidi sita wa upande
wa Jamhuri, ikiwa ni pamoja na mkemia aliyethibitisha kuwa ni dawa za
kulevya na mashahidi walioshuhudia mshitakiwa akizitoa kwa njia ya haja
kubwa, hakimu alimwachilia huru.
Kutokana na hali hiyo, Bulaya alisema: “Lazima Watanzania tuchukue
hatua sasa, kwa sababu kama nilivyoainisha hapo juu kwamba kwa kipindi
cha miaka mitatu tu (2010-2013), wakati tani 64 za dawa za kulevya
zilipita bila kukamatwa…zikiwa mtaani zikiharibu vijana na watoto wetu,
katika kipindi hicho hicho kiasi kilichoweza kukamatwa ni tani 1.6 tu!
Takwimu hizo za kutisha zinatoa picha kwamba sehemu kubwa ya shehena
za dawa za kulevya hupitishwa bila kugundulika au kukamatwa na vyombo
vya dola.”
Alishangaa kwamba ni kwa bahati mbaya, licha ya ukubwa wa tatizo,
pamoja na athari zake kwa jamii ya Watanzania, hakuna tafiti
zinazoonyesha ukubwa wa tatizo kwa nchi nzima, huku vyombo vya dola
vikiwa ndivyo vinara wa kuwatorosha watuhumiwa wanaoendesha biashara
hii, ikiwemo ofisi ya DPP na Idara ya Mahakama.
Tuhuma hizo nzito zilimlazimu Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole
Sendeka (CCM) jana kuomba mwongozo wa Spika akitaka serikali itoe kauli
yake kuhusu maelezo binafsi yaliyotolewa juzi na mbunge huyo wa viti
maalumu ya kuitaka serikali kufanya mabadiliko ya sheria ya dawa za
kulevya na kuanzisha mahakama maalumu.
“Mheshimiwa Naibu Spika ninasimama hapa kuomba mwongozo. Naomba chini
ya kanuni 68(7) na 28 kuhusu maelezo yaliyotolewa na Esther Bulaya,
kuhusu suala zima la namna ya kuwashughulikia wahalifu wa dawa za
kulevya.
Baada ya mbunge huyo kueleza kwa kina mambo ambayo
yanabainisha na kuweka shaka juu ya uadilifu na uaminifu wa watoa
haki katika mahakama zetu na ofisi ya DPP na vyombo vya usalama,
Sendeka alitaka serikali itoe majibu kuhusu suala hilo la vita dhidi ya
dawa za kulevya ambalo si jukumu la Mahakama na vyombo vya usalama
pekee bali Tanzania kwa ujumla.
Alibainisha kuwa ili wananchi waweze kujua jinsi waliotoa uamuzi au
hukumu ambayo haikuwa kwenye misingi, sheria na mahakama zilivyochukua
hatua dhidi ya mahakimu na majaji walio husika.
Mara baada ya Sendeka kumaliza kuomba mwongozo huo, Naibu Spika, Job
Ndugai, alitoa fursa kwa Waziri Lukuvi, ambaye alisema serikali
inaandaa taarifa inayoeleza jitihada za serikali.
“Serikali imejiandaa kutoa kauli kupitia kwa Waziri wa Katiba na
Sheria na itatoka kabla ya kuondoka hapa bungeni, na itaeleza
tulivyojipanga kuunda chombo kipya cha kushughulikia dawa za kulevya
pamoja na kuanzisha sheria itakayosaidia chombo hicho,” alisema.
0 comments:
Post a Comment