Rais Jakaya Kikwete, kesho anatarajiwa kulihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Habari zilizopatikana Mjini Dodoma jana na
kuthibitishwa na uongozi wa Bunge pamoja na Ikulu, Dar es Salaam
zinasema atahutubia mchana.
Kutokana na ujio huo, Serikali imewaelekeza
Mawaziri na Manaibu Waziri kutotoka nje ya Dodoma hadi hapo Rais
atakapokuwa amehutubia Bunge. Kadhalika safari zote za Kamati za Bunge
ambazo zilikuwa katika mchakato wa kutekelezwa zimeahirishwa hadi baada
ya kesho, ili kutoa fursa kwa wabunge wote kuwapo wakati wa hotuba hiyo.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema
jana kuwa hata yeye amesikia taarifa kuwa Rais atazungumza bungeni
lakini hajui atazungumza kitu gani… “Hata mimi nimesikia kuwa
atazungumza lakini sijui atazungumza jambo gani kwa kuwa siyo miongoni
mwa watu wanaomwandalia hotuba,” alisema Balozi Sefue.
Kadhalika, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva
Rweyemamu alithibitisha kuwa Rais Kikwete atalihutubia Bunge, Alhamisi…
“Nathibitisha ni kweli, ila kwa taarifa nyingine watafuteni watendaji wa
Bunge, kama Katibu wa Bunge nadhani wana taarifa zaidi.”
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah
alithibitisha jana katika Viwanja vya Bunge Dodoma kuwapo kwa ratiba ya
Rais Kikwete kulihutubia Bunge na kwamba taarifa rasmi ingetolewa jana
jioni kwa wabunge.
“Ni kweli Rais anatarajiwa kuja kulihutubia Bunge na leo (jana) jioni, tutatoa taarifa rasmi bungeni,” alisema Dk Kashililah.
Mara ya mwisho Rais Kikwete alilihutubia Bunge
wakati akifungua rasmi Bunge la Kumi, Novemba 18, 2010 alipoeleza
vipaumbele vya Serikali yake katika awamu ya pili ya uongozi wake. Rais
Kikwete analihutubia Bunge wakati likisubiri kujadili mapendekezo ya
marekebisho katika Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba ya 2013 ambayo ilipitishwa katika mkutano uliopita.
Tayari Muswada wa Marekebisho unaopendekezwa
umewasilishwa katika Ofisi ya Katibu wa Bunge chini ya hati ya dharura
na leo utajadiliwa katika Kikao cha Kamati ya Uongozi ili kupata kibali
cha kuingizwa ndani ya Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala na baadaye
Bungeni.
Dk Kashililah alisema amepokea muswada huo na
kwamba uamuzi wa lini utafikishwa bungeni utafanywa na Kamati ya Uongozi
ya Bunge ambayo itakutana na leo.
Kamati hiyo ndiyo yenye mamlaka ya kuifanyia
marekebisho ratiba ya vikao vya Bunge na kuruhusu mambo yanayopaswa
kuingizwa bungeni kujadiliwa.
Muswada huo ni matokeo ya majadiliano baina ya
Serikali kwa upande mmoja na vyama vya siasa vyenye wabunge chini ya
uratibu wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kwa upande mwingine,
baada ya vyama vya siasa kutoridhishwa na muswada ulipitishwa katika
mkutano wa Bunge uliopita.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Itakumbukwa kwamba wabunge wa vyama vya upinzani vya Chadema,
NCCR Mageuzi na CUF walisusia shughuli za mchakato wa kupitishwa kwa
marekebisho ya sheria hiyo bungeni, hivyo kutoa fursa kwa wabunge wa CCM
kufanya watakavyo kisha kupitisha sheria hiyo.
Baada ya kupitishwa huko, vyama hivyo viliendesha
kampeni ya kuitisha maandamano nchi nzima, lakini kabla hayajafanyika
Rais Kikwete aliwaalika viongozi wake katika meza ya majadiliano,
mchakato ambao umezaa mabadiliko yanayokusudiwa kuingizwa bungeni wiki
hii.
Katika mazingira hayo kumekuwa na hofu kwamba
huenda wabunge hasa wa CCM wakatumia wingi wao kukwamisha mabadiliko
yanayopendekezwa kutokana na kukasirishwa kwao na kile kilichoonekana
kuwa ni Rais Kikwete kuwasikiliza wapinzani.
Hiyo inaweza kuwa ndiyo sababu kubwa ya Rais
Kikwete kuamua kulihutubia Bunge kwa lengo la kujenga msingi wa
maridhiano katika mchakato wa kuandikwa kwa Katiba Mpya kama ambavyo
amekuwa akisisitiza mara kwa mara.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment