Waasi
wa M23 katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wametangaza kumaliza
uasi wao ndani ya nchi hiyo muda mfupi baada ya kupigwa katika ngome yao
ya mwisho na majeshi ya serikali ya Congo yakishirikiana na kikosi
maalum cha Umoja wa Mataifa kilichopewa uwezo wa kupigana na waasi hao.
Katika taarifa waliyoitoa waasi hao wamesema badala ya kufanya uasi sasa wataendesha harakati zao kutumia njia ya kisiasa.
Muda mfupi uliopita Kiongozi wa waasi hao
Bertrand Bisimwa ametangaza kuwaamuru mkuu wa wapiganaji wa M23 na
makamanda wa vikosi vyote muhimu wa kundi hilo kuwaandaa wapiganaji wao
kusalimisha silaha, kutawanyika kuondoka katika eneo la mapigano na
kukubaliana na matakwa yatakayowekwa na serikali ya Congo.
Awali Msemaji wa Serikali ya Jamuhuri ya
Kidemokrasia ya Congo Lambert Mende aliambia BBC kuwa majeshi ya nchi
yameishambulia ngome ya mwisho ya waasi na wamekimbia na wengine huenda
wakawa wamejisalimisha.
Majeshi ya serikali ya Kongo yakishirikana na
kikosi maalum cha Umoja wa Mataifa kilichopewa uwezo wa kupambana na
waasi hao walianza mapambano dhidi ya M23 Octoba mwaka huu na kufanikiwa
kuwaondoa katika eneo la Bunagana kwenye mpaka wa Uganda ambayo ni
ngome yao muhimu.
0 comments:
Post a Comment