Vita ya kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa
mwaka 2015 imeingia katika sura mpya baada ya Waziri Mkuu mstaafu,
Frederick Sumaye kumlalamikia mrithi wake katika wadhifa huo, Edward
Lowassa akimtuhumu kumfanyia mbinu chafu.
Huku akinukuu habari iliyoandikwa na gazeti hili
Septemba 16, 2013 yenye kichwa cha habari, ‘Lowassa afichua siri ya
mradi wa maji Ziwa Victoria’, Sumaye alisema Lowassa amekuwa akimfanyia
propaganda na mbinu chafu.
Katika habari hiyo, ambayo Lowassa alialikwa
katika Harambee ya kuchangia Shule ya Msingi ya Kanisa la AICT huko
Kahama, Shinyanga hivi karibuni, alikaririwa akisema mawaziri watatu, tu
ndiyo waliounga mkono wakati alipopendekeza kutekelezwa kwa mradi huo
kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri cha Serikali ya Awamu ya Tatu
iliyokuwa chini ya Benjamin Mkapa.
Lowassa, ambaye katika kipindi hicho alikuwa
Waziri wa Maji na Maendeleo ya Mifugo, aliwataja mawaziri waliounga
mkono mradi huo kuwa ni Rais Jakaya Kikwete ambaye wakati huo alikuwa
Waziri wa Mambo ya Nje na Mohamed Seif Khatibu, aliyekuwa Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Sumaye alisema hizo ni mbinu chafu zilizokuwa na lengo la
kumpaka matope… “Najua mhusika ametumia sana mradi huu kisiasa na sisi
wengine tumenyamaza japo ukweli tunaujua. Amenilazimisha niseme ukweli
kuhusu mradi huu kwa sababu mimi nilikuwa Waziri Mkuu na mradi
umetekelezwa chini ya uangalizi wangu,” alisema na kuongeza:
“Kama Waziri anaweza kubuni na kutekeleza mradi
mkubwa hivyo peke yake, akiwa Waziri Mkuu si maji yangefika Dodoma?
Mbona hata bado kuna kuna sehemu za Kanda ya Ziwa bado kuna shida ya
maji?” alihoji Sumaye, ambaye alikuwa Waziri Mkuu kwa miaka 10 katika
Serikali ya Awamu ya Tatu.
Alipotafutwa kwa simu kuelezea madai hayo,
Lowassa, ambaye yuko Dodoma akihudhuria vikao vya Bunge, alisema hawezi
kubishana na Sumaye kwa kuwa anamheshimu kwani amewahi kuwa kiongozi
mkubwa serikalini.
“No comment’ (sina la kusema), siwezi kubishana na
Sumaye kwani amewahi kushika nyadhifa za juu katika nchi hii,” alisema
Lowassa, ambaye pia ni Mbunge wa Monduli (CCM).
Sumaye alimtuhumu Lowassa kwa kusema uongo na kuongeza kuwa amefanya kosa la jinai kutoa siri za Baraza la Mawaziri.
“Pamoja na kwamba hilo lililoelezwa ni uongo
mkavu, mhusika kama waziri mwandamizi wakati huo na sasa anawinda nafasi
kubwa katika nchi, hakutegemewa kutoa siri za Baraza la Mawaziri, labda
amediriki kufanya hivyo kwa sababu anajua anayosema siyo ya kweli,
vinginevyo ni kosa la jinai na akishtakiwa anafungwa jela,” alisema.
Sumaye alisema hizo ni mbinu chafu zinazofanywa dhidi yake kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
“Ziko mbinu nzuri na za kistaarabu na ziko mbinu chafu kama za
kupakana matope (character assassinations). Mtu wa kwanza anajisafishia
njia yake kwa kufyeka miiba na kuondoa magogo njiani ili wakati
ukiwadia, mbio zake zisikwazwe na vigingi vyovyote. Aina ya pili ya
mbinu chafu ni pale mhusika anapotengeneza mbinu za kuwamaliza wengine
wanaodhaniwa kuwa washindani wake,” alisema Sumaye.
Hata hivyo, alipoulizwa kama amejipanga kugombea urais mwaka 2015, Sumaye alisita kujibu kwa muda mrefu, lakini baadaye akajibu:
“Nasema hivi, kama ni kugombea nina haki zote,
kama ni uwezo ninao, kama ni imani ya Watanzania kwa sehemu kubwa
ninayo. Kilichobaki ni uamuzi tu wa mimi kutamka. Kwa hiyo sijatamka
msije mkasema nagombea urais. Nasema tu na mimi katika Watanzania
wanaofikiriwa na mimi nasikia nimo. Kwani ninyi hamnifikirii? Sasa
itakapofika huko mbele, si tutaamua wakati huo?”
Kuhusu hujuma zinazofanywa katika shughuli za
jamii kwa maslahi ya siasa, Sumaye alisema kuna watu wanaomfanyia hujuma
na kuzuia mialiko yake.
Alitoa mfano wa mwaliko wa Oktoba 27 mwaka huu wa
kupokea maandamano ya kikundi cha Joggers katika shughuli, ambayo
ilikuwa ifanyike Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.
“Dakika za mwisho nikapewa taarifa kuwa shughuli
imeshindikana kwa sababu imeingiliwa na kikundi chenye kulinda masilahi
yake au ya mtu wao. Shughuli hiyo baadaye ilifanyika na kupatikana
‘mgeni rasmi’ mwingine,” alisema.
Hata hivyo, katika hatua nyingine, Shirika la
Faita Jogging Sports Clubs limekanusha kumwalika Sumaye kwenye shughuli
yao ya Mnazi Mmoja.
Akizungumza na waandishi wa habari jana,
Mwenyekiti wa shirika hilo, Steven Kaema alisema shirika hilo
halikufanya mawasiliano ya aina yoyote na Sumaye tofauti na anavyodai.
“Hatukuwa na mawasiliano yoyote na Sumaye, sisi
tulituma barua ya mwaliko kwa Makamu wa Rais ambaye alitujibu kuwa
hatakuwepo siku hiyo na tulituma barua nyingine kwa Naibu Waziri wa
Elimu, Philipo Mulugo ambaye naye alijibu kuwa atasafiri kwa hiyo ofisi
yetu haina barua yoyote ya kumuomba Sumaye kuwa mgeni rasmi,” alisema
Kaema.
“Mara ya pili ni mwaliko wa kuzindua Saccos ya
Nshamba Muleba, Kagera, Oktoba 28,” aliendelea Sumaye… “Mwaliko huu
sikuomba, bali viongozi wa chama walinipendekeza kwa sababu zao wenyewe.
Wakati najiandaa kwenda, nikaambiwa shughuli zimeingiliwa na watu
fulani kwa kutoa rushwa kwa baadhi ya viongozi wa Saccos.”
Alipotakiwa kuwataja watu hao anaodai kuwa wanamhujumu, Sumaye katika mialiko yake, alijibu:
“Siwataji, hata ninyi mnawajua. Nataka
niwataaarifu hao wanaohangaika na mialiko yangu kwa taarifa yao ninayo
mingi mpaka mingine nakosa muda wa kuhudhuria. Siitwi kwa sababu ya
fedha maana wanajua sina fedha za aina hiyo maana sijaiibia nchi na watu
wake,” alisema Sumaye.
Alidai kuwa wanaomhujumu wanafanya hivyo ili kumzima
asizungumzie rushwa, ufisadi na dawa za kulevya… “Fisadi huliibia taifa
fedha nyingi kiasi cha wananchi kutaabika halafu huja kutoa kijisehemu
cha fedha alizofisadi kwa njia ya rushwa kukandamiza maendeleo ya watu.”
Rushwa CCM
Sumaye alimpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa
kupambana na rushwa na kutahadharisha kuwa tatizo hilo linaweza
kukiangusha chama hicho. Aliahidi kuwa na Rais bega kwa bega katika vita
hiyo.
“Rais Kikwete amesema kuwa rushwa inaweza ikafanya
chama hiki kikashindwa. Mimi naamini, kama CCM itapitisha majina kwa
kuangalia rushwa bila kujali, chama kitaanguka, bahati nzuri Mwenyekiti
ameliona hilo, siamini kama watapitisha watu ambao watakiangusha…
waliopitishwa kama hawataenguliwa, sitaweza kukaa nao, hata kama
sitahama.”
0 comments:
Post a Comment