Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola akiomba mwongozo kwa Naibu Spika, Job
Ndugai wakati wa kikao cha kwanza cha Mkutano wa 13 wa Bunge, mjini
Dodoma jana.
Wabunge jana walichachamaa na kushinikiza kutolewa kwa orodha ya
vigogo wanaojihusisha na ujangili wakati wa kikao cha kwanza cha
mkutano wa 13 wa Bunge unaofanyika mjini Dodoma.
Wabunge hao walitaka kutajwa kwa majina ya mawaziri, viongozi wa Serikali na wabunge wanaojihusisha na biashara hiyo.
Baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na
majibu, Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola, aliomba mwongozo,
akiitaka Serikali kuwataja hadharani na kuwachukulia hatua viongozi wake
na wanasiasa, wakiwamo mawaziri na wabunge, ambao wanatajwa kuhusika na
vitendo vya ujangili nchini.
Lugola aliomba mwongozo wa Naibu Spika baada ya
kutoridhishwa na jibu lililotolewa na Naibu Waziri wa Maliasili na
Utalii, Lazaro Nyalandu, wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa
Kahama (CCM), James Lembeli.
Katika jibu hilo, Nyalandu alilieleza Bunge kuwa
Operesheni Tokomeza inayolenga kukomesha vitendo vya ujangili nchini
bado inaendelea, lakini alishindwa kulieleza Bunge ni nani hasa
wamebainika kuhusika na vitendo hivyo.
Lugola, hata hivyo, aliitaka Serikali kuwasilisha ripoti bungeni kuhusiana na utekelezaji wa operesheni hiyo.
“Tangu Aprili tumekuwa tukipewa majibu mepesi kuhusiana na operesheni hii, wakati suala hili si la masihara,” alionya Lugola.
Lugola alisema kuwa taarifa zimewataja watu
wanaohusika na vitendo hivyo wakiwamo viongozi serikalini, mawaziri
pamoja na wabunge, lakini tangu operesheni hiyo ilipoanza hakuna yeyote
miongoni mwa hao wanaotajwa ambaye amekamatwa isipokuwa wananchi wa
kawaida.
Alisema operesheni hiyo imekuwa ikiendeshwa kwa
unyama kwani wanaokamatwa hupigwa na kuteswa bila ya ushahidi
unaoonyesha kuhusika kwao na vitendo vya ujangili.
“Inashangaza sana kuwa wale wanaotajwa
hawachukuliwi hatua, lakini wananchi wanazidi kuteseka… Mathalani, zipo
taarifa kuwa wakuu wa polisi katika mikoa inayopakana na Mbuga ya
Serengeti ndio waratibu wa shughuli za ujangili, lakini hatujasikia hao
wakichukuliwa hatua,” alisema.
Kabla ya Naibu Spika kutoa majibu ya mwongozo
ulioombwa na Lugola, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera,
Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisimama na kukiri kuwapo kwa
vitendo vya utesaji wa watu wanaokamatwa katika operesheni hiyo.
Alitolea mfano tukio la kukamatwa kwa msaidizi
wake jimboni ambaye alipigwa na kuteswa na askari hao kabla ya kuachiwa
baada ya kushikiliwa kwa siku moja, huku akionyesha kuwa ushahidi wa
tukio hilo anao kwenye simu yake.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
“Lakini sisemi haya kwa kutaka kuitetea Serikali kuwa isilete
ripoti hapa bungeni. Nadhani kuwa kuleta ripoti hivi sasa haitakuwa
vizuri. Ni vizuri tusubiri mpaka kazi hii ikamilike na nina uhakika kuwa
Wizara itaandaa ripoti na kuiwasilisha kwenye kamati husika,” alisema
na kuongeza:
“Nadhani kuwa `entry point’ (mahali pa kuanzia) yetu iwe ni kwenye ripoti hii itakayowasilishwa kwenye Kamati,”
Suala la ujangili limeingizwa bungeni wakati
kukiwa na usiri mkubwa wa nani anahusika na vitendo hivyo, huku majina
ya vigogo wanaotajwa kuhusika nayo wakiwa hawafahamiki.
Polisi watajwa vinara
Awali akijibu swali la msingi lililoulizwa na
Mbunge wa Kigamboni (CCM), Dk Faustine Ndugulile, Nyalandu alisema Jeshi
la Polisi ni vinara miongoni mwa makundi manne ya majeshi ambayo
watumishi wake wamekamatwa wakijihusisha na ujangili.
Katika matukio saba ya ujangili yaliyowahusisha
watumishi tisa wa vyombo vya ulinzi na usalama, Nyalandu alisema kati ya
hao sita ni polisi wakati kwa kupande wa Jeshi la Wananchi Tanzania
(JWTZ), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Magereza alikamatwa mtu mmoja
mmoja.
“Katika matukio hayo, jumla ya meno ya tembo 686
na vipande 447 vikiwa na uzito wa kilogramu 4,253.9 vilikamatwa, jambo
ambalo linaonyesha ukubwa wa tatizo hilo kwa vyombo vya ulinzi,” alisema
Nyalandu.
Katika swali la msingi, Dk Ndugulile alitaka
kufahamu idadi ya matukio ya upatikanaji wa pembe za ndovu yaliyohusisha
vyombo vya ulinzi na usalama.
Katika swali la nyongeza, Lembeli ambaye ndiye
aliyeuliza swali hilo kwa niaba ya Dk Ndugulile, aliitaka Serikali
kuacha kigugumizi na kueleza ukweli kuwa wapo baadhi ya viongozi,
wakiwamo wabunge ambao wamekuwa wakijihusisha na biashara hiyo.
“Katika biashara ile kuna hali ya kulindana sana,
hebu Serikali itueleze taarifa za kuwa wahusika wengine ni wanasiasa na
baadhi ya wabunge, ukweli uko wapi, na kuna taarifa kuwa viongozi wa
Polisi wanaoishi kuzunguka hifadhi zetu ndio ambao wanatumiwa
kusafirisha nyara hizo, Serikali inasemaje?” alihoji Lembeli.
Nyalandu alisema Tanzania iko katika hali mbaya
katika kiwango cha mauaji ya tembo ambapo wastani unaonyesha kuwa kila
siku tembo 30 huuawa na majangili.
“Hata hivyo, suala la ulinzi bado tuko nyuma sana
kwani wastani wa ulinzi wa kimataifa ni askari mmoja kwa kilomita za
mraba 25, lakini sisi askari wetu mmoja analinda kilomita za mraba 150
ndani ya hifadhi,” alisema Nyalandu.
Serikali yakiri tatizo
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi
Vuai Nahodha akizungumza bungeni kwa niaba ya Waziri Mkuu, alikiri
kuwapo fununu za wanasiasa ambao wamekuwa wakijihusisha na biashara hiyo
na kusema Serikali italifanyia kazi jambo hilo.
Nahodha aliwataka Watanzania kuwa watulivu wakati
vyombo vya Ulinzi na Usalama vinaposhughulika na kusafisha tatizo hili
na kuonya wanasiasa kuacha kutoa shinikizo kwa kutumia nguvu zao za
kisiasa.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment