Kwanza kabisa napenda kushukuru sana serikali yetu tukufu kwa kuninyima nafasi ya kuandika. Vidole vyangu vimepumzika vizuri na nilipata nafasi ya kusoma pia kidogo. Tena niliamua kusoma hadithi ya zamani sana.
Nadhani na wengi wenu mmesoma pia lakini safari hii kwa kuwa sikuweza kuandika, nikabaki natafakari zaidi.
Hadithi yenyewe ni Nguo Mpya za Mfalme. Yaani ile hadithi ya mfalme mwenye kiburi cha kaburi, aliyejiona hadi akashindwa kuona wengine. Sasa watu kama hao wanadanganyika kirahisi maana inatosha kumsifia tu kupita kiasi, ataamini chochote kile. Ndiyo maana wale matapeli wa kimataifa waliweza kumdanganya kwamba wamemtengenezea suti nzuri kiasi kwamba ni wale wenye akili tu wanaweza kuiona.
Sasa kwa kuwa mfalme alijiona mwenye akili kupita kiasi, angekubali kweli kwamba haoni? Akajiangalia kwenye kioo na kujiona alivyo bila nguo lakini wala hakutafakari kwamba iwapo wasio na akili hawaoni suti, wataona nini?
Akakubaliana na sifa za matapeli moja kwa moja na kuwapatia pesa zao taslimu badala ya kuwapatia karatasi na kusema kwamba ni wenye akili tu wataona zile karatasi ni manoti ya fedha. Matapeli walijiondokea harakaharaka, kabla hawajaanza kucheka maana ….
Baada ya hapo, mfalme, bila kujiuliza tena ataonekanaje na wasio na akili akajipeleka mitaani kutamba na suti yake. Alitanguliwa na matarumbeta na ngoma kibao kuwaita watu kuja kuona suti ya kipekee, akasindikizwa na mawaziri wake na wengine wengi ambao wote walikuwa wanaimba wimbo wa kusifia jinsi mfalme alivyovaa na kwamba nguo yake ni sifa kubwa kwa nchi yao, inaonyesha jinsi nchi ilikuwa imeendelea.
Sasa hebu fikiria wewe ungekuwa mmoja wa watazamaji, ungejisikiaje? Ungefumba macho ili usione mambo ya siri ya mfalme? Lakini hata kama usingeona wewe, wengine wote wanaona. Au ungewashawishi wengine wafumbe macho pia. Lakini hata kama wote wangefumba macho, hali ya mfalme ingebadilika?
Mmh! Ungejiunga na waliokuwa wanamsifia usionekane mtu asiye na akili wala uzalendo? Hapa roho isingekusuta? Kwa kweli wananchi walipata tabu sana lakini mwisho wa siku badala ya kutazamana na kukubaliana kusema kwa sauti moja ‘Mfalme hana nguo!’waliamua kusifia tu.

Wakashindana kushangilia kwa vigelegele na viherehere. Kweli uoga ni ugonjwa mbaya sana. Unaona kabisa siri ya wazi hadi wachefuka, lakini bado kunyamaza tu.
Hadi mtoto akapasua anga ya uoga na unafiki
‘Jamani mbona mfalme yuko uchi?’
‘We nyamaza mtoto. Huna akili kabisa.’
‘Hapana mama. Hana nguo. Mbona naona ….’
Bila shaka mtoto alizabwa kibao na kuzibwa mdomo.
‘Marufuku kusema unayoona. Kama mfalme haoni hivi wewe ni nani kuona tofauti. Amevaa, amevaa, amevaa!’
Tena kama mzazi alijaribu kuficha maana sauti ya yule mtoto lilikuwa kali. Lilipasua anga na kuzima matarumbeta hadi hata mabaunsa wa mfalme walikuja mbio mbio kujua ni nani anayethubutu kumwumbua mfalme. Ndiyo. Na mabaunsa walifuatana na wale waliojidai kulinda usalama wa mfalme. Badala ya kulinda usalama wake kwa kuhakikisha kwamba haonekani bila nguo, wanalinda usalama kwa kuwanyamazisha walioona ukweli huo.
Hata hivyo, walipokaribia pale waliposikia sauti, kumbe na mtoto mwingine aliachana na uoga wa wazazi wake na kupaza sauti.
‘Kweli. Hebu ona. Haoni aibu?
Mabaunsa na wanausalama wakabadili mwelekeo na kumtafuta huyu mwingine. Lakini mwingine alidakia. Na mwingine. Na mwingine hadi mabaunsa walichanganyikiwa kabisa. Kumbe waweza kumdaka mtu mmoja mmoja, au hata kuwanyamazisha lakini watu wakisema kwa pamoja watapata wapi watu wa kutosha?
Basi wakati wanakimbia huku na kule kama kuku waliokatwa kichwa, hata watu wazima wasio na uzima wowote wakalazimika kukubali ukweli. Vicheko vikaambukizana kila mtu akianza kumwonyesha mfalme.
Ha ha ha ha ha ha ha ha!
Sasa hebu fikiria iwapo wewe ni mfalme utajisikiaje? Bila shaka utajiona mjinga kwelikweli. Lakini daima nimejiuliza baada ya hapa alifanya nini. Ametamba huku akifikiri anaendeleza umahiri na umaarufu wake, kumbe ni kinyume. Alimkamata yule mtoto na kumtia ndani kwa kumwaibisha? Kwamba nyeti za mwenyewe ni siri ya taifa? Eti kumwaibisha kiongozi ni kulibomoa taifa lake? Au alimwita na kumpongeza kwa kuwa wa kwanza kumwambia ukweli. Au aliwatuma watu kumwua yule mtoto ili kuondoa ushahidi maana enzi zile bahati nzuri hakukuwa na kamera au simu za mkononi.
Hivyo ukifunga mdomo wa mkweli waoga na wanafiki watarudi palepale walipoanzia? Au labda alimwita yule mtoto na kumpa pesa nyingi sana abadili kauli, eti aliona vibaya na kwamba kweli alikuwa amevaa suti.

Na mabaunsa je? Na wanausalama wanaolinda usalama kwa kunyamazisha ukweli? Waliendelea na unyama wa unyamazishaji kwa kufikiri kwamba wanalinda bosi wao? Au labda walizidisha unyama wa unyamazishaji kwa woga wa kumwaga unga baada ya kushindwa kulinda heshima za unyeti. Bila kusahau kutangaza kwamba mtoto alitumwa na maadui zake. Na ikiwa ni maadui zake, ni maadui wa taifa pia kwa hiyo kutangaza utupu wake ni uhaini.
Hivyo, bila hata mfalme kujua walimsweka ndani, na kuanza kumtesa kujua nani alimtuma yule mtoto. Walianza kuwakamata watu ovyo ovyo. Yeyote aliyecheka alikuwa mtuhumiwa.
Na baada ya hapo? Hivi ukweli ukishatoka kwenye chupa, si kama jini? Haliwezi kurudishwa ndani ya chupa tena. Hapo wewe ungekuwa mfalme ungefanya nini?
Mwananchi 
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top