Edward Lowassa
Suala la mvua za kutengeneza kutoka nchi ya Thailand maarufu kwa
jina la ‘Mvua za Lowassa’ liliwagonganisha mawaziri wawili wa Serikali
bungeni jana.
Ubishi mkali ulizuka baina ya Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira, Dk Terezya Huvisa na Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi waliokuwa
wakivutana juu ya ukweli kuhusu teknolojia hiyo.
Wakati Waziri Huvisa akisema kwamba hakuna utaalamu wa aina hiyo, Lukuvi alisimamia kumpinga na kusisitiza kuwa jambo hilo lipo.
Suala la mvua hizo lililetwa nchini na aliyekuwa
Waziri Mkuu Edward Lowassa mwaka 2007, baada ya kufanya ziara Thailand
ambako alivutiwa na utaalamu wa kutengeneza mvua na kuahidi kuuleta
nchini.
Kutokana na mvutano wa mawaziri hao, Lowassa
ambaye pia ni Mbunge wa Monduli (CCM), alipewa dakika moja na Mwenyekiti
wa Bunge, Jenister Mhagama kutoa ufafanuzi ambapo aliunga mkono hoja ya
Lukuvi.
Malumbano hayo yalisababishwa na swali la nyongeza
la Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Susan Lyimo ambaye alihoji mpango
wa kutengeneza mvua ulipoishia kwa kuwa Serikali imekuwa kimya.
“Sasa ni miaka takriban sita au saba tangu
Serikali ilipokuja na mpango wa kutengeneza mvua ambao iliuchukua kutoka
nchi za wenzetu, mpango huo umefikia wapi?” aliuliza.
Akijibu swali hilo, Waziri Huvisa alisema: “Mimi
ni Rais wa Mazingira wa Afrika, nasema hakuna kitu kama hicho, si
Marekani wala Malaysia ambao wanaweza kutengeneza mvua, hayo ni
mabadiliko ya tabianchi tu.”
Waziri Lukuvi alionyesha kutokuridhishwa majibu
hayo, ndipo aliposimama kutoa ufafanuzi na kusema Lowassa alikwenda
Thailand ambako kuna utaalamu huo na kusisitiza kwamba upo na bado
unaendelea kutumika hata Ujerumani wanakotumia mitambo ya kijeshi
kusambaratisha mawingu.
Alisema kilichokwamisha mpango huo nchini ni ufinyu wa bajeti ya Serikali.
Baada ya majibu hayo, Lowassa alisimama akitaka
kutetea wazo lake. Hata hivyo, kabla ya kumruhusu, Mhagama alimwomba
akae chini kwanza ili atoe maelekezo.
“Mheshimiwa Lowassa, yeye siyo waziri na hivyo
hastahili kutoa majibu ya Serikali, lakini kwa kutumia kanuni zetu
bungeni kuhusu kutengeneza utaratibu mzuri wa kuongoza Bunge, naomba
Lowassa usimame sasa walau kwa dakika moja au mbili utoe ufafanuzi,”
alisema Mhagama.
Aliposimama Lowassa alizungumza kwa ufupi; “Nakushukuru
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kukazia tu kuwa jibu lililotolewa na
Mheshimiwa Lukuvi ndilo jibu sahihi.”
Majibu hayo yalisababisha Bunge kulipuka kwa shangwe.
Mara baada ya majibu ya Lowassa, Waziri wa Kilimo,
Chakula na Ushirika, Christopher Chiza naye alisimama akitaka kutoa
maelezo.
Hata hivyo, Mhagama alisema inatosha na kuwaagiza mawaziri hao kukutana kuliangalia jambo hilo badala ya kuwa na majibu kinzani.
Hata hivyo, Mhagama alisema inatosha na kuwaagiza mawaziri hao kukutana kuliangalia jambo hilo badala ya kuwa na majibu kinzani.
Awali, katika swali la msingi, Mbunge wa Viti
Maalumu (Chadema), Rachel Mashishanga alitaka kujua ni kwa nini Serikali
isirasimishe utaalamu wa kuleta mvua kutoka kwa waganga wa jadi walioko
Mikoa ya Katavi na Rukwa ili maeneo yanayokabiliwa na ukame yapate
mvua?
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher
Chiza, alipinga mpango huo na kusema hakuna kitu kama hicho isipokuwa
wapo watu wenye utaalamu wa kuangalia mawingu yanayoendana na mvua.
Alisema watu wote wanaosema kuwa wanaweza kutengeneza mvua kwa imani za kishirikina ni waongo na hivyo hawapaswi kuaminiwa.
Alisema siyo wakati mwafaka kwa Serikali
kushinikizwa kurasimisha utaalamu huo wa kuleta mvua kwa kuwa hakuna
tafiti zozote zilizofanyika na kuthibitisha kuwapo kwake.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment