Mahakama Kuu imewatetea majaji na mahakimu dhidi ya tuhuma zilizotolewa kwao kuwa waliwaachia kwa dhamana washtakiwa wa dawa za kulevya kinyume cha sheria na kuwafanya watoroke.
 
Jaji Kiongozi, Fakih Jundu amesema mahakama haipaswi kubebeshwa lawama katika hilo, bali ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kutokana na kutokutimiza masharti ya kisheria wanapofungua kesi mahakamani.
Kauli ya Jaji kiongozi imekuja baada ya shutuma zilizotolewa dhidi yao baada ya chombo kimoja cha habari (jina tunalo) kuandika habari kwa kuwataja kwa majina baadhi ya majaji na mahakama kuwa wamekuwa wakiwalinda washtakiwa wa dawa za kulevya katika kesi ambazo wamekuwa wakizisikiliza.
Shutuma hizo zilihusiana na tukio la hivi karibuni ambapo raia wawili wa Pakistani waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya dawa za kupewa kuachiwa kwa dhamana na Mahakama Kuu na zimekuwepo taarifa kuwa wametoroka nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, ofisini kwake, Jaji Jundu alikanusha tuhuma hizo akisema kuwa majaji na mahakimu wamekuwa wakitoa uamuzi kwa kuzingatia ushahidi na misingi ya kisheria.
“Kuna wakati huwa tunawaeleza DPP kuwa kuna madhaifu katika kesi mbalimbali wanazofungua. Hivyo huwa tunawaeleza kuwa ni vyema muwe mnajipanga sawasawa kabla ya kuzileta,” alibainisha.
Jaji Jundu alisema miongoni mwa dosari hizo ni pamoja na kesi za dawa kufunguliwa bila kuwa na hati ya kiapo cha kamishna wa dawa za kulevya, inayoonyesha thamani ya dawa hizo.
Alifafanua kuwa ni kweli kwamba Sheria Na. 9 ya kudhibiti dawa za kulevya ya mwaka 1995, inazuia mtu yeyote aliyekamatwa na dawa zenye thamani kuanzia Sh10 milioni asipewe dhamana.
Hata hivyo,alisema sheria hiyo hiyo, katika kifungu Na. 27 (1) (b) kinamtaka, DPP kuambatanisha katika hati ya mashtaka kiapo kinachoonyesha thamani halisi ya dawa za kulevya alizokamatwa nazo mshtakiwa.
Kiapo hicho, Jaji Jundu aliongeza kuwa kwa mujibu wa sheria hiyo, ni lazima kithibitishwe na kamishna wa Tume ya Taifa ya Kuratibu na Kudhibiti Dawa za Kulevya.
Mwananchi 
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top