Rais Jakaya Kikwete
SIKU moja baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba kuonyesha hofu juu ya mbinu za kutaka kuivunja tume yake, wadau mbalimbali wameibuka na kutaka jambo hilo kuangaliwa kitaifa.

Jaji Warioba alizungumza na waandishi wa habari juzi na kusema kuwa muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba wa mwaka 2013, uliopitishwa na Bunge hivi karibuni, unalenga kuifuta tume hiyo kabla ya kumaliza muda wake.

Aliwataka wanasiasa kuacha malumbano katika mchakato huo wa upatikanaji katiba mpya, akiwashauri waketi pamoja na kukubaliana vipengele vyenye utata vinavyobishaniwa.

Katika kuunga mkono kauli ya Jaji Warioba, wadau mbalimbali waliozungumza na gazeti hili jana, walisema kuwa kuna haja ya kuangalia suala la katiba kitaifa ili kuepusha mgogoro unaoweza kujitokeza.

Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), alisema kama Rais Jakaya Kikwete ataamua kuusaini muswada huo pasipo kupatikana muafaka wa mambo yanayolalamikiwa, atakuwa ameruhusu mwendelezo wa matukio ya mashinikizo kutoka sehemu mbalimbali ya nchi.

Alisema kuwa mambo yanayolalamikiwa ni pamoja na rais kuwa na uwezo wa kuteua wajumbe 166, pamoja na kutoshirikishwa kwa wananchi wa Tanzania visiwani na kueleza kuwa ni muhimu madai hayo yakafanyiwa kazi kabla ya muswada kusainiwa.

“Ninaona hatari mbele ya Tanzania ijayo, suala la katiba si la kufikiria walio wengi bungeni wanaweza kupitisha kwa wingi wao, na kama rais atasaini pasipo mambo ya msingi kushughulikiwa, basi aviandae vyombo viwe tayari kukabiliana na matokeo yatakayojitokeza,” alisema.

Lugola ambaye amekuwa akisimamia ukweli bila kujali kuburuzwa na chama chake, aliongeza kuwa ni makosa makubwa kuwadharau wabunge wa upinzani kwa sababu ya uchache wao pasipo kuangalia hoja inayotolewa na watu hao.

Huku akisisitiza kuzingatiwa kwa hoja inayotolewa badala ya wingi wa kundi, Lugola alisema katika mambo ya msingi ni vema uamuzi wa kupitisha jambo kwa wingi wa kura badala ya hoja likaepukwa.

Lugola aliongeza kuwa katiba ni suala linalotoa mustakabali wa maisha ya Watanzania kwa muda mrefu, na kwamba haifai kukimbizwa huku masuala ya msingi yakiachwa pembeni.

Kuhusu kuvunjwa kwa Tume ya Jaji Warioba, mbunge huyo alisema mwenyekiti huyo ni mtu asiyeeleweka katika misimamo yake, na kwamba anachofanya sasa ni kutetea na kutaka kulinda maslahi yake.

Alisema wananchi wanapaswa kujiuliza kwanini alikuwa akiwazuia kuingilia maoni ya mchakato wa katiba, na sasa anajitokeza kulalamikia kipengele kimoja kinacholinda maslahi ya tume.

Naye Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (CHADEMA), alisema rais anapaswa kuliangalia suala la katiba kama mkuu wa nchi, na kwamba ni wajibu wake kuhakikisha anaiunganisha nchi badala ya kuigawa.

Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, alisema katiba huandikwa kwa muafaka na sio kwa vyama kuweka maslahi yake mbele.

“Namshauri rais asiusaini huu muswada na aurudishe bungeni ili ujadiliwe upya na viongozi wa kisiasa wajenge muafaka,” alisema.

Kuhusu Tume ya Warioba, mbunge huyo alisema inapaswa kufanya kazi kwa mujibu wa sheria, na kwamba suala la muda wa mwisho wa tume lifafanuliwe upya na sheria.

Mkurugenzi wa Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC), Hellen Kijo-Bisimba, alisema kuwa hatua ya kuivunja tume hiyo kabla ya wakati ni sawa na mchakato huo kuwa yatima.

“Huwezi kuivunja Tume ya Jaji Warioba sasa, maana bado ina kazi kubwa ya kufanya ikiwa ni pamoja na kutoa elimu wakati wa mchakato wa kura za maoni,” alisema.

Alitolea mfano na kusema kuwa unapoamua kuivunja tume kabla ya muda ni sawa na kuiruhusu treni kwenda bila kichwa.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top