NAIBU Katibu Mkuu wa Umoja wa vijana wa CCM (UVCCM) Zanzibar, Shaka
Hamdu Shaka amesema hakuna wa kumzuia Rais Jakaya Kikwete, asisaini
muswada wa mabadiliko ya Katiba.
Amesema iwapo Rais Kikwete, atakubali shinikizo la wapinzani
kutokusaini Muswada huo, atakwenda kinyume na kiapo chake cha utiifu na
uaminifu kwa Watanzania.
Shaka alisema hayo jana, mjini Unguja, alipokuwa akizungumza na
waandishi wa habari akielezea hatua ya Muungano wa vyama vitatu vya
siasa, vinavyopinga muswada wa mabadiliko ya Katiba, kutiwa saini na
rais.
Akifafanua alisema rais Kikwete, asiposaini muswada huo atakuwa
amekwenda kinyume na kifungu cha sheria namba 97, na hivyo atakuwa
amepingana na sheria ya Bunge. Na kusisitiza: “Rais hana haja ya
kushinikizwa na Wapinzani,”.
Shaka alisema mchakato wa mabadiliko ya Katiba, unaoendeshwa nchini
humo, ni kwa mujibu wa sheria na Katiba na hauendeshwi kwa matakwa na
utashi wa vyama vya CHADEMA, CUF pamoja na NCCR-MAGEUZI.
Kiongozi huyo wa Umoja wa Vijana wa CCM Zanzibar, pia alisema vyama
hivyo vilipaswa kwanza kujenga hoja ndani ya kamati za Bunge na baadaye
katika Bunge lenyewe:
“Kitendo cha Wabunge wa upinzani cha kutoka ndani ya ukumbi wa
Bunge…ni sawa na kuwadhalilisha na kuwasaliti Watanzania,” alisema
Shaka.
Alisema ‘UVCCM’ inao ushahidi wa kutosha kwamba Waziri wa Katiba na
Sheria wa Zanzibar, Abubakar Khamis Bakari pamoja na Mwanasheria Mkuu wa
Zanzibar, Othman Masoud waliandika mapendekezo ya vipengele vya muswada
wa Katiba, vifungu vinne na kuorodhesha kama maoni ya Wazanzibari.
Shaka alisema Abubakar, alitamka kwamba hana tatizo na uteuzi wa
nafasi 166 za Wabunge wa Bunge la Katiba kutoka katika maeneo
mbalimbali, kama asasi za kiraia na makundi mengine: “Vipi sasa
wanamzuia rais asisaini muswada huo?,” alihoji Shaka.
Chanzo: Habari Leo
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment