Kamati ya Maridhiano Zanzibar imetangaza maazimio sita yanayotakiwa kuzingatiwa katika mchakato wa kupata Katiba Mpya kabla ya Bunge la Katiba kujadili rasimu ya mwisho na kufanyika kura ya maoni mwakani.
 
Maazimio hayo yametangazwa na Kamati hiyo pamoja na Baraza la Katiba Zanzibar (Bakaza) katika mkutano na waandishi wa habari uliyofanyika, Shangani mjini Zanzibar jana.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Hassan Nassor Moyo alisema Marekebisho ya sheria hiyo yaliyofanywa na Serikali na kupitishwa na Bunge yana upungufu makubwa katika utaratibu kuandaa muswada huo na uchukuaji wa maoni yake.
Alisema kabla ya Rais kusaini muswada huo, wadau kutoka Zanzibar wapewe nafasi ya kutoa maoni yao na urudishwe upya bungeni kujadiliwa na kupitishwa kwa manufaa ya pande mbili za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Aidha, alisema kifungu kinachotoa nafasi kwa wabunge wa Bunge la Katiba kupitisha Katiba kwa wingi wa kura kama theluthi mbili itashindikana kupatikana muafaka, kifutwe na badala yake utaratibu wa awali wa kupitisha kwa kutumia theluthi mbili ubakie kutumika kwa manufaa pande mbili za Muungano.
“Tunapinga kifungu kinachoweka ukomo wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba mara baada ya kuwasilisha Rasimu ya mwisho ya Katiba kwa Rais,”alisema Moyo ambaye ni aliwahi kuwa Waziri wa Sheria wa Serikali ya Muungano.
Alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba inapaswa kuendelea na kazi yake ya kutetea rasimu ndani ya Bunge la Katiba badala ya kuitwa kama waalikwa kama kutaonekana na haja ya kufanya hivyo wakati wa mjadala wa Bunge hilo.
Mambo mengine yaliyopendekezwa na Kamati hiyo ni wajumbe wa Bunge maalumu la Katiba wawe idadi sawa baina ya Zanzibar na Tanzania Bara hasa kwa kuzingatia Katiba inayopitishwa ni ya Jamhuri ya Muungano unaotokana washirika wawili waliokuwa na sifa sawa kabla ya kuungana mwaka 1964.
Alisema wajumbe 166 wa Bunge la Katiba kutoka makundi mbalimbali ya kijamii na asasi za kiraia wachaguliwe na makundi na taasisi zenyewe badala ya kazi hiyo kufanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa  kushirikiana na Rais wa Zanzibar.
Hata hivyo, alisema Kamati yake inaunga mkono ushauri wa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba wa kutaka  viongozi wa kisiasa na makundi ya kijamii kukutana na kukaa pamoja kuzungumzia mvutano uliyojitokeza baada ya kufanyika kwa marekebisho ya muswada huo.
Mwananchi
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top