SIKU mbili baada ya serikali kutumia sheria ya magazeti ya mwaka
1976 inayolalamikiwa na wadau wa sekta ya habari kuyafungia magazeti
mawili ya kila siku ya Mwananchi na Mtanzania, wadau mbalimbali
wamejitokeza na kuipinga adhabu hiyo.
Sheria hiyo inampa ruhusa waziri mwenye dhamana ya habari kupiga
marufuku uchapaji na matumizi ya gazeti lolote ambalo anafikiri liko
kinyume na maslahi ya umma.
Katika adhabu hiyo, gazeti la Mtanzania limefungiwa kwa siku 90 huku
Mwananchi likifungiwa kwa siku 14, adhabu mbazo zimeanza Septemba 27,
mwaka huu, yakidaiwa kuchochea.
Wakizungumzia adhabu hizo, wadau hao, Mbunge wa Kigoma Kaskazini,
Zitto Kabwe (CHADEMA), mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
Dk. Azavel Lwaitama, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA) na
mwandishi nguli, Ndimara Tegambwage walidai kuwa serikali imeendelea
kutumia sheria mbovu kubana uhuru wa habari nchini.
Zitto: JK amezidiwa
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Zitto alisema kuwa
serikali imechukua uamuzi huo kwa kutumia sheria ya kidikteta ya
magazeti ya mwaka 1976, ambayo Tume ya Jaji Francis Nyalali
iliiorodhesha kama sheria kandamizi.
Alisema kuwa sababu zilizotolewa kuhalalisha uamuzi huu hazina maana,
na kwamba serikali ingeweza kufungua mashitaka ya kawaida mahakamani
kushitaki magazeti hayo iwapo haikupendezwa na habari walizochapisha.
“Moja ya sababu ya kufungiwa kwa gazeti la Mwananchi ni kuchapisha
taarifa kuhusu mishahara ya serikali. Serikali inasema habari hii ni
siri.
“Serikali hii hii ambayo imesaini makubaliano ya kuendesha serikali
kwa uwazi (Open Government Initiative) na kumwagiwa sifa na Rais Barack
Obama wa Marekani, inalifungia gazeti kwa kuandika habari za mishahara
ya watumishi wa serikali,” alisema.
Zitto aliongeza kuwa mishahara kuanzia wa rais hadi mtendaji wa kijiji haipaswi kuwa jambo la siri.
“Kwamba kuonyesha kuwa jambo hili linapaswa kuwa wazi, mkutano ujao wa
Bunge tutatafuta kila namna kutaja mshahara wa rais, makamu wa rais,
waziri mkuu na baadhi ya watendaji wa mashirika makubwa ya umma kama
njia ya kuwaunga mkono gazeti la Mwananchi kwa habari yao hiyo,”
alisema.
Kwa mujibu wa Zitto, mapato ya mbunge yanajulikana sasa kuwa ni sh
milioni 11.2 kwa mwezi kabla ya kuongeza posho za vikao za sh 200,000
kwa siku na posho ya kujikimu ya sh 130,000 kwa siku.
“Watanzania wana haki ya kujua wanawalipa kiasi gani watumishi wao. Tutaanza na mshahara wa rais,” alisema.
Alisema kuwa gazeti la Mtanzania limefungiwa pamoja na mambo mengine
kwa kuandika ‘mapinduzi ni lazima’. Kwamba inashangaza Serikali ya CCM
inaogopa neno mapinduzi.
“Marehemu Mzee Steven Salum Nandonde, aliyekuwa mbunge wa Tandahimba
alipata kusema bungeni kuwa ‘lazima nchi ipinduliwe’. Ni matumizi ya
lugha tu. Mzee Nandonde yeye alikuwa analalamikia maendeleo duni ya
mikoa ya kusini na kutaka kaskazini iwe kusini na kusini iwe kaskazini,”
alisema.
Zitto aliongeza kuwa serikali inafungia gazeti kwa sababu ya kuandika
‘Mapinduzi ni lazima’ ilhali kila siku Zanzibar wanasema ‘Mapinduzi
daima’.
“Gazeti la Mtanzania linahaririwa na Absalom Kibanda, mwandishi wa
habari ambaye bado anaponya majeraha ya mwili na kisaikolojia ya kuteswa
na watu ambao hadi leo hawajakamatwa.
“Badala ya serikali kuwakamata watesaji wa Kibanda, inamnyima kazi
Kibanda ili ateseke kwa njaa kwa kukaa miezi mitatu bila kazi,” alisema.
Pia aliongeza kuwa inawatesa Watanzania kwa njaa ya kupata habari
ambayo ni haki ya msingi ya kikatiba. Kwamba hiyo ndiyo zawadi serikali
inampa Kibanda baada ya kung’olewa kucha, kunyofolewa jicho, kukatwa
vidole na kuteswa kwa namna isiyoelezeka.
“Matukio ya hivi karibuni na namna serikali inavyoyachukulia
yanaonyesha dhahiri kwamba Rais Kikwete kazidiwa nguvu na kundi la
wahafidhina ndani ya chama na serikali yake.
“Rais ambayo alianza kwa kuhubiri uvumilivu wa hali ya juu, na hata
yeye mwenyewe kupata kusema uvumilivu huu wengine wanauona kama udhaifu,
lakini ameamua kujenga taifa la kutovumiliana,” alisema.
Kwa mujibu wa Zitto, rais alipata kulalamika hadharani kwamba kuna
wenzake wanataka aongeze ukali, hivyo ni dhahiri kundi hili la
wahafidhina sasa ndilo linalomwongoza Rais Kikwete.
“Kitu kimoja tu rais azingatie, kundi hili linaongozwa na maslahi
binafsi ya kubakia kwenye utawala wakati yeye anapaswa kuacha ‘legacy’,”
alisema.
Alisema kuwa Rais Kikwete asipokuwa makini atakuwa rais karatasi (lame duck) tu tunapoelekea mwisho wa utawala wake.
Kwamba uamuzi wa hovyo na wa kidikteta wa kufungia magazeti unamchora vibaya mbele ya wananchi na jamii ya kimataifa.
“Wananchi sasa waifanye serikali kujutia uamuzi wake wa kufungia
magazeti. Nimeamua mimi binafsi kama mbunge (leo Septemba 30, 2013)
kupeleka taarifa rasmi kwa Katibu wa Bunge ya kupeleka muswada bungeni
wa kuifuta kabisa sheria kandamizi ya magazeti ya mwaka 1976,” alisema.
Ndimara anena
Katika andiko lake kwenye mtandao wa kijamii, mwandishi wa habari
nguli, Ndimara Tegambwage alisema kufungia magazeti ni uhalifu dhidi ya
haki.
Alisema: Serikali inaendelea kufungia vyombo vya habari. Orodha inaongezeka. Mara hii ni zamu ya Mwananchi na Mtanzania.
MwanaHALISI lilifungiwa miezi 15 iliyopita (mwaka mmoja na robo).
Hakuna dalili za kulifungulia. ‘Redio mbao’ zinasema hata wamiliki wake
wasiruhusiwe kuanzisha gazeti jingine. Limekuwa suala la binafsi.
Hatua ya serikali ya kufungia gazeti hilo imeathiri na inaendelea
kuathiri waandishi, wake/waume zao na watoto wao; wazazi wao, ndugu
waliowategemea, wauza magazeti, wenye maduka karibu na ofisi za gazeti
hili, wauza matunda, mihogo, karanga, kahawa na kashata waliokuwa
wakitua MwanaHALISI.
Wengi wameathirika hivyo kiuchumi. Sasa waandishi wamekuwa
wabangaizaji kwa kuomba vibarua katika magazeti ya wengine. Wananchi
wengi wameathirika kwa njia ya kukosa taarifa.
Mtu mmoja serikalini au kundi la watu; wanatumia nafasi zao kutaka
kuua kwa njaa waandishi na familia zao; na kunyima wananchi taarifa
muhimu zinazowawezesha kupata uelewa juu ya wanavyotawaliwa na jinsi ya
kujinasua kutoka mkenge wa ghiliba, wizi na ufisadi.
Jana serikali iliongeza machungu kwa waandishi na wananchi na orodha
yote niliyotaja hapo juu kwa amri ya kufungia magazeti ya Mwananchi na
Mtanzania. Na serikali inajua. Hiyo siyo njia sahihi ya kutenda kazi.
Serikali inaingilia kazi na majukumu ya mahakama.
Kwa ufupi, serikali inapuuza na kudharau mahakama. Kuna sheria ya
magazeti ya mwaka 1976, katili kama ilivyo, lakini bado inatumika na
watawala ndio wameiweka mbelekoni. Kwanini serikali haiitumii kwa njia
ya kwenda mahakamani? Inaogopa nini? Woga wake ni upi?
Kuna Baraza la Habari Tanzania (MCT). Limejaa na linashirikisha
wataalamu wa nyanja muhimu katika tasnia hii - waandishi wa habari na
wanasheria. Lina uwezo mkubwa wa kusikiliza na kutolea uamuzi malalamiko
ya mtu au taasisi yoyote. Serikali hailitumiii.
Wahusika ndani ya
serikali wanatumia ubabe wa amri kwa nia ya ‘kuua sisimizi kwa kutumia
nyundo’, lakini nje ya mkondo wa sheria au ushauri wa kitaaluma ambao
unaheshimika zaidi kuliko amri au mitulinga.
Kesho serikali itazima gazeti au chombo kingine cha habari. Itaondosha
ajira za waandishi. Itafinyaza fursa za kujiendeleza katika taaluma
hii. Itanyakua haki ya uhuru wa kupata taarifa na habari.
Itafanya kazi zake gizani na kwa hiyo bila mrejesho kutoka kwa jamii
pana iliyokuwa inapata taarifa kupitia vyombo vya habari vinavyofungiwa.
Kufungia au hata kufuta chombo cha habari, licha ya kwamba ni kuvunja
haki za binadamu; vilevile ni kuziba mifereji ya fikra ya jamii;
kuongeza umasikini, kuasisi woga miongoni mwa watu, kujenga visima vya
chuki na hasira dhidi ya serikali; kutaka watu waishi kwa umbeya na
kurudisha jamii katika ujima.
Hatupendi kuamini kuwa haya yanatendwa na serikali inayojiita ya
‘kidemokrasia’ na inayojigamba kuwa na uwazi na utawala bora. Hapana!
Kuna serikali ngapi - moja itende demokrasia na nyingine itende uhalifu
dhidi ya haki ya uhuru wa habari? Ghiliba!
Tumependekeza tangu 1985. Kwamba serikali iache wananchi na waandishi
wa habari waiseme wanavyoiona. Kama sivyo ilivyo, basi ipuuze. Kama
ndivyo ilivyo, basi ijisahihishe.
Serikali ina maguvu mengi ya kutumia kuleta mabadiliko kwa maslahi ya
watu; na siyo kwa kuangamiza uhuru wa kufikiri na kutoa mawazo.
Inakokwenda serikali, siko!
Lwaitama
Mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Lwaitama
alisema si sahihi kufungia magazeti na serikali kuanza kupangia wananchi
wasome au wasisome nini.
“Tunaomba tuambiwe mahojiano hayo na maonyo yalifanyika chini ya
uangalizi wa nani? Na yalifanyikia wapi? Hapa ninaona kuna kikundi
kidogo cha watu fulani katika serikali wameamua kuanza kufungia magazeti
kwa manufaa yao,” alisema.
Dk. Lwaitama aliongeza kuwa tuhuma zinapotolewa zipelekwe kwenye
chombo cha uamuzi ili hukumu itolewe, kwamba haiwezekani serikali ndiyo
inatoa tuhumu na kuhukumu yenyewe.
“Tumekuonya, hatupendezwi na uandishi wako, hivyo tunakufungia siku 14
au siku 90,” hizi ni kauli za utawala wa kibabe, na udikiteta. Hakuna
dhana ya utawala bora,” alisema.
Alihoji kuwa kama kosa ni uchochezi, mbona kuna kesi mahakamani
inayomhusu Kibanda na mwandishi Samson Mwigamba wakidaiwa kuchapisha
makala ya uchochezi?
Kwamba kesi hiyo ina utofauti gani na tuhuma hizi zinazoitwa uchochezi
hadi kusababisha magazeti ya Mwananchi na Mtanzania kufungiwa bila
kupelekwa mahakamani?
Dk. Lwaitama alisisitiza kuwa kitendo kilichofanywa ni kama vile
Tanzania hakuna mahakama wakati rais anateua majaji kila mara, na hivyo
kuhoji kazi zao ni zipi kama mawaziri wanajipangia hukumu.
Wanaharakati
Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THIRD
Coalition), Onesmo Olengurumwa alisema leo wanakutana na wadau
mbalimbali wa habari kwa lengo la kujadili na kutoa tamko rasmi
kuhusiana na suala la kufungiwa magazeti hayo.
Alisema mara baada ya kukutana watazungumza na waandishi wa habari kutoa maazimio waliyofikia katika kikao hicho.
Hata hivyo, alisema sheria ya magazeti ya mwaka 1976 ni kandamizi na inahitaji kuondolewa.
Olengurumwa aliongeza kuwa sheria zilizopo zinakandamiza uhuru wa vyombo vya habari.
“Sheria hii ni kandamizi kwa kuwa serikali wao ndio walalamikaji,
lakini wao wenyewe wanatoa uamuzi bila kushirikisha upande wa pili,
jambo ambalo ni unyimwaji wa uhuru wa vyombo vya habari,” alisema.
Zanzibar wacharuka
Jumuia ya Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar (Wahamaza) nayo
imeungana na watetezi wa uhuru wa vyombo vya habari kusikitikia uamuzi
wa serikali kufungia magazeti ya Mwananchi na Mtanzania.
Katibu wa Wahamaza, Salma Saidi alisema uamuzi wa serikali umetolewa
wakati wanatasnia ya habari wanadai uhuru zaidi wa habari, na wakati
bado wanalalamikia kufungia gazeti la MwanaHALISI kwa muda usiojulikana.
“Wahamaza inaamini kuwa adhabu ya kuyafungia magazeti ni kubwa mno na
haikusitahiki, na sababu zilizotolewa na serikali kuyafungia magazeti
hayo hazitoshelezi,” alisema.
Alisema kuwa wanaamini kwamba njia bora ya serikali kujenga utawala
bora wenye kuheshimu sheria ni kutumia mahakama katika malalamiko dhidi
ya habari zinatolewa na vyombo vya habari.
“Wahamaza inatoa wito kwa wadau wa vyombo vya habari nchini kuendelea
na harakati za kuitaka serikali kufuta sheria zote zitazotumia
kukandamiza vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na sheria ya kufungia
magazeti,” alisema.
0 comments:
Post a Comment