Mhe. Rais Kikwete akihutubia Kikao cha 68 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Mjini New York.
Rais Jakaya Kikwete juzi alihutubia kikao cha 68 cha Baraza Kuu
la Umoja wa Mataifa (Unga), New York, Marekani na kusema kama nchi
tajiri duniani zingetoa fedha za kutosha kama zilivyokuwa zimeahidi, ni
dhahiri kuwa dunia ingeweza kufanikisha utekelezaji wa Mipango ya
Maendeleo ya Milenia (MDG’s) na malengo yake yote katika kipindi cha
miaka 15 kama ilivyokuwa imeamuliwa mwaka 2000.
Aidha, Rais Kikwete alisema Afrika haitochoka
kudai haki ya kufanyika kwa mageuzi ya msingi ndani ya Baraza la Usalama
la Umoja wa Mataifa (UNSC), ili kuliwezesha bara hilo lenye idadi kubwa
zaidi ya wanachama kwenye Umoja wa Mataifa (UN) kuwa na uwakilishi wa
kudumu.
Katika hotuba yake ya dakika 15, Rais Kikwete
alisema ni jambo lisiloelezeka kuwa dunia ya leo inaendelea kushuhudia
umasikini wakati kuna raslimali na utajiri wa kutosha wa kumaliza tatizo
hilo ikiwa kuna utashi wa kisiasa kumaliza tatizo hilo.
Rais Kikwete alikiambia kikao hicho ambacho mada
yake kuu ilikuwa `Mjadala Kuhusu Ajenda ya Maendeleo Duniani baada ya
mwaka 2015' kuwa pamoja na kwamba umasikini mkali zaidi duniani
umepunguzwa kwa nusu katika kipindi cha utekelezaji wa MDG, bado zaidi
ya watu bilioni 1.2 wanaishi katika mtego wa umasikini mkubwa.
Alisema kuwa mbali na watu hao, bado kiasi cha
watoto wanaokadiriwa kufikia 19,000 chini ya umri wa miaka mitano na
wanawake 800 hupoteza maisha kila siku kwa magonjwa ambayo yanaweza
kuzuilika na kutibika.
“Hili ni jambo ambalo halikubaliki kabisa katika
dunia iliyojaa neema ya kila aina tunamoishi leo ambako kuna maendeleo
ambayo hayajapata kuonekana katika historia ya binadamu ya sayansi na
teknolojia ambayo yanaweza kutumika kumaliza changamoto zote za
maendeleo zinazokabili jamii ya binadamu sasa.
“Katika dunia ambako kuna chakula cha kutosha
kumlisha kila mtu, hakuna sababu ya mtu yeyote kulala na njaa na
kukabiliwa na ukosefu wa lishe. Katika dunia yenye utajiri mkubwa kama
wa sasa, hakuna sababu kwa nini umasikini, njaa na dhiki viendelee
kuleta dhiki na kusababisha shida kubwa kwa watu wengi kiasi hiki.”
Rais Kikwete alisisitiza: “Katika hali hiyo, ni
jambo lisiloingia akilini kwa nini Malengo ya Milenia hayakufanikiwa kwa
kiwango cha juu kabisa.
“Kama nchi tajiri na zilizoendelea duniani
zingekuwa zimetoa fedha na rasilimali za kutosha kama ilivyokuwa
imekubaliwa chini ya lengo la nane kwa mipango hiyo kwa mujibu wa
makubaliano na ahadi zao katika mikutano ya nchi tajiri duniani ya G8 na
G20, tungefanikiwa kutekeleza mipango hiyo,” alisema Rais Kikwete na
kuongeza:
“Kwa maana hiyo, litakuwa ni jambo la kujidanganya
kama tulijadili nini tufanye kuhusu Malengo ya Maendeleo ya Milenia
Baada ya 2015 bila kujadili na kukubaliana kuhusu jambo la msingi la
jinsi ya kugharimia mipango hii.”
Mapema leo, Rais Kikwete amekutana na kufanya
mazungumzo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon na baadaye
alikutana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani (anayeshughulikia
siasa), Wendy R Sherman.
Mwananchi
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment