Dk. Salim Ahmed Salim
WAZIRI Mkuu mstaafu Dk. Salim Ahmed Salim, amevionya vyombo vya
dola kuwa matumizi ya nguvu dhidi ya wananchi ni kiashiria cha
uvunjifu wa amani.
Dk. Salim ameeleza masikitiko yake kuhusu uwepo wa viashiria vya
uvunjifu wa amani, zikiwemo kauli za viongozi na kuitaka jamii
kupambana navyo kwa kudumisha misingi ya amani ambayo ni upendo,
kuheshimiana na kuvumiliana.
Mwanadiplomasia huyo wa kimataifa alisema hayo Dar es Salaam jana
alipozungumza na Tanzania Daima Jumatano wakati wa kongamano la
kutafakari amani ya nchi lililoandaliwa na Kituo cha Demokrasia
Tanzania (TCD).
Kauli ya kiongozi huyo mashuhuri Afrika ilikuja baada ya kutakiwa
kutoa maoni yake kuhusu kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliyoitoa
hivi karibuni bungeni, akiwaruhusu askari polisi kuwapiga wananchi
aliodai wanavunja sheria.
Pinda alitoa kauli hiyo siku chache baada ya bomu kutupwa kwenye
mkutano wa CHADEMA wa kumalizia kampeni za uchaguzi mdogo wa madiwani
mjini Arusha kwenye Uwanja wa Soweto.
“Mimi nadhani nguvu ya dola siku zote itumike kwa maslahi ya
wananchi… wakati mwingine mazingira yanakuwa magumu mtu anaudhika,
lakini kitu muhimu popote pale duniani nguvu ya dola isipotumika kwa
maslahi ya wananchi itavuruga amani.
“Tujifunze kwamba bila amani, bila utulivu hakuna kinachofanyika.
Vurugu katika jamii ni mbaya, hebu tujifunze kwa nchi za wenzetu
zinavyovurugana… amani ni kitu muhimu kwa familia zetu, watoto wetu na
jamii nzima.
“Lazima tuheshimiane, tumefika kama kisiwa cha amani kwa
kuheshimiana, tusibaguane, tupambane na viashiria vya uvunjifu wa
amani,” alisisitiza Dk. Salim aliyepata kuwa balozi wa Tanzania kwenye
nchi mbalimbali.
Aidha, alionya matumizi ya nyumba za ibada yanayofanywa na baadhi ya
wanasiasa nchini na kusema si vema kupeleka siasa, huku akitaka
viongozi wa dini na wanasiasa watimize wajibu wao kila mmoja kwa nafasi
yake bila kuingiliana.
Naye Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana wa Wizara ya Habari, Utamaduni
na Michezo, Profesa Elisante ole Gabriel aliwataka viongozi wa dini
kutoshabikia siasa na kuwaonya viongozi wanaopeleka siasa kwenye nyumba
za ibada.
“Viongozi wa dini watambue nafasi yao katika kudumisha amani bila
kushabikia,” alisema mkurugenzi huyo na kuongeza kwamba wanapofanya
hivyo wanaashiria uvunjifu wa amani kwa sababu dini na siasa ni mambo
tofauti.
Gabriel alishauri kuwepo na mafunzo maalumu kwa wanasiasa ya jinsi ya
kuzungumza jukwaani huku akisisitiza kwamba yanayotokea Tanzania na
Afrika nzima ni matokeo ya kuingia kwenye mfumo wa vyama vingi bila
kujiandaa kisaikolojia.
Alivitaja viashiria vya uvunjifu wa amani kuwa ni kutoaminiana kwa
viongozi, wananchi na wanasiasa jambo linalowafanya kila mmoja
kumlalamikia mwenzake.
“Tusibaguane ingawa kwa sasa ubaguzi upo kwenye siasa. Ipo siku
tutabaguana dhahiri, naamini tofauti za kisiasa ni njia rahisi ya
kupoteza amani yetu. Ubaguzi wa kidini na kikabila utatupeleka pabaya,”
alisema.
Alishauri TCD iendelee kuwezeshwa kwa gharama yeyote ili kiwe chombo
cha kuwakutanisha wanasiasa na serikali katika kuimarisha umoja,
mshikamano na kuaminiana kwa mustakabali wa amani ya Tanzania.
Alichagiza kwamba upo uwezekano wa chama kingine kuingia madarakani,
lakini sio kwa kukidharau chama kinachotawala huku akisisitiza kwamba
uwezekano wa chama kimoja kukaa madarakani muda mrefu upo ila sio
kutawala milele.
Naye Mwenyekiti wa TCD, James Mbatia, aliwataka wanasiasa wasijione
muhimu zaidi kuliko Watanzania wengine, hivyo kila wanachokifanya
lazima kiwe kwa maslahi ya wote.
Mbatia alisisitiza kwamba viongozi wa dini hawapendi kuona polisi
wakiwalinda wakati wanawafundisha neno la Mungu waamini wao, hivyo
kuwataka wanasiasa wasiwe chanzo cha vurugu nchini.
Naibu Katibu Mkuu Bara wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro,
alisema iwapo mifumo thabiti ya utoaji haki haijengwa na haki
ikaonekana kutendeka, bado amani ya nchi itaendelea kuwa shakani.
“Hata TCD wakiitisha makongamano kama haya mara 10,000 wakajadili
amani, kama viongozi wa serikali hawapo tayari kuiweka mifumo thabiti
ya kuifanya haki itendeke na ionekane, hayo makongamano hayatafanikiwa.
“Watawala wanataka kuiendesha nchi kwa kubahatisha, jambo ambalo ni
hatari kwa amani ya nchi badala yake wawe radhi kuweka mifumo imara ya
kumwezesha kila mmoja kupata haki kwa wakati,” alisisitiza Mtatiro.
Kongamano hilo la siku mbili litamalizika leo.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment