Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Freeman Mbowe.
Sehemu ya Hotuba ya M/kiti wa Taifa ailiyoitoa leo katika Mkutano wake na Waandishi wa Habari kuhusu maazimio ya Kamati Kuu iliyokutana tarehe 06-07/07/2013 Blue Pearl Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam.

Ndugu Waandishi wa Habari,
Kila tukionewa tunalia, kila tukionewa tunatoa matamko, lakini kila tukienda kwenye vyombo vya dola kuomba msaada tunakamatwa sisi; Tunaoshambuliwa ni sisi, tunaopigwa ni sisi, tunaoshitakiwa ni sisi, tumejaa Mahakama mbalimbali katika Taifa hili, Idadi ya Viongozi na Wanachama wa CHADEMA wanaokabiliwa na kesi mbalimbali katika nchi hii mpaka sasa hivi ni zaidi ya 2000, wako katika hatua mbalimbali za mashtaka ya kubambikiziwa.

Sasa tunasema tunaendelea kupigwa tu, ushahidi tunao, wanaendelea kutupiga tu, na Polisi inalinda wapigaji, lazima na sisi sasa kama Chama tutafute na sisi njia ya kujilinda. 

Kama M/kiti wa Chama mimi naweza kushambuliwa kwenye mkutano wa hadhara kwa mabomu, na risasi za SMG, na risasi za Bastola, na bado mpaka leo hajakamatwa mtu hata mmoja!! Waliokamatwa sanasana ni vijana wa CHADEMA waliokuwa wanapiga picha jukwaani ili waweze kutoa ushahidi, Tunasema tutakuwa ni Wajinga kama tutaendelea kusubiri, kupiga magoti na kulia.
 
Waziri Mkuu anazungumza Bungeni, PIGENI! Anawapa mamlaka Jeshi la Polisi, Waziri Mkuu anavunja Katiba! Anavunja sheria Rais hamkemei! Makamu wa Rais hamkemei! Jamii inalalamika, Watanzania wanalalamika, Taasisi za kiserikali, Taasisi zisizo za kiserikali wanalalamika, Wanasheria wanalalalmika, Waandishi wa Habari wameandika, Serikali imeweka Pamba masikioni, Waziri Mkuu anapeta mtaani na Mawaziri wenzake wanamuunga mkono kwamba tutaendelea kupiga. 

Tunasema wataweza kupiga vilevile lakini na wao vilevile kufikiria kwamba wataweza kupiga milele kuna siku na wao watajikuta katika mazingira ya kupigwa. Aidha watapigwa na Mahakama au watapigwa na sheria zilezile wanazozivunja.

Lakini tunawaambia vijana wetu sasa hivi na ni wajibu kabisa wa Chama kutafuta njia ya kujilinda, Tulindwe na nani!!?? Hatulindwi na Polisi, hatulindwi na Usalama wa Taifa, hatulindwi na Jeshi la Wananchi, TUNAPIGWA NA KILA MTU!! Watu wetu wanaumizwa, wanauwawa!! Ni lazima sasa tujue tuna uwezo wa kujilinda kwa sababu tukienda Polisi hatutapata hiyo haki Polisi.

Kwa hiyo sisi kama Chama kama Kamati Kuu ya Chama tumesema ili kukabiliana na fujo zinazofanywa na vijana wa Chama cha Mapinduzi nchi nzima, na sisi tuna kikosi chetu cha Vijana wa RED BRIGADE, ambacho ni kikosi kilichoundwa kwa mujibu wa Katiba ya Chama, ambacho kina wajibu Mkubwa wa kulinda Chama na mali zake. 

Labda pengine kikosi chetu kimekuwa legelege sana au kimekuwa cha upole sana kiasi kwamba wale wanaona wana nguvu za kupiga kiasi wanavyotaka, Sisi kama Kamati Kuu tunasema kwamba tutafanya mafunzo maalum kwa ajili ya vijana wetu ya namna ya KUJILINDA nchi nzima, na sisi tutaweka Makambi kama ambavyo Chama Cha Mapinduzi kinaweka makambi ya kuwafundisha vijana wake kwa ajili ya kushambulia ila sisi tutafundisha namna ya kujilinda. 

Kama wao wanaweka makambi ya kuwafundisha vijana wao namna ya kushambulia sisi tutaweka Makambi ya kuwafundisha vijana wetu ukakamavu kwa sababu hatuna mlinzi na hatuwezi kuwa Kondoo wa Kafara.
FB 
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top