MATUKIO ya wasanii na vijana mbalimbali wa Kitanzania kukamatwa
na dawa za kulevya ndani na nje ya nchi, yameendelea kutikisa huku
kukikosekana jawabu la hatima yake.
Katika siku za nyuma, matukio haya yalikuwa kama uvumi tu, lakini kwa
sasa si siri tena na majina yamekuwa yakitajwa waziwazi, huku mengine
yakihusishwa na mizigo ya dawa yenye uzito na gharama kubwa sana, kiasi
cha kutia shaka juu ya walioko nyuma ya biashara hizi.
Inatia shaka, kutokana na ukweli kwamba si rahisi kwa wasanii hawa
kujitwisha mizigo hii ya mabilioni na kuanza kuzunguka nayo pande
mbalimbali za dunia, bila kuwa na mkono mnene unaowatetea na kuwapa
uhakika wa usalama wao.
Kama alivyosikika akisema Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni za IPP,
Reginald Mengi, hivi karibuni, ni wazi biashara hii imezungukwa na
vigogo wakubwa, ambao kutokana na ushawishi wao, imekuwa ni rahisi
kuwaingiza wasanii na vijana wengi katika mtego huu.
Akizungumzia hivi karibuni nchini China, wakati wa ugeni wa Katibu
Mkuu wa CCM, Abdulhaman Kinana na ujumbe wake, Balozi wa Tanzania nchini
humo aliyehamishiwa Ujerumani kwa sasa, Philip Marmo, anasema kwamba
kuna vijana zaidi ya 100 wa Kitanzania waliomo kwenye magereza
mbalimbali nchini China kutokana na biashara hii haramu.
Anaongeza kwamba, wengi wa vijana hawa, tayari wamekwisha kuhukumiwa
kunyongwa, ingawa kutokana na uhusiano wa kidiplomasia uliopo kati ya
Tanzania na China, wengi wamebadilishiwa vifungo vyao na kuwa vya
maisha, huku vikiambatana na kazi ngumu.
Ripoti za aina hii haziko katika nchi ya China tu, bali mataifa
mbalimbali duniani na kumekuwa na ripoti nyingine za kimataifa zikiitaja
Tanzania kama lango kuu la biashara hii haramu ya dawa za kulevya.
Ni bahati mbaya kwamba, katikati ya wingu zito la dawa hizi za
kulevya, wasanii wa Kitanzania wamejikuta kwenye mzingo tata wa kubebwa
na kokoro hili.
Wasanii wamebebwa na kokoro hili katika mazingira mawili, kwanza wao
wenyewe kuhusika moja kwa moja katika matumizi yake na pili kuyabeba
kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa ajili ya kuyauza.
Orodha ya wasanii ambao wamekuwa wakihusishwa na matumizi ya dawa za
kulevya, huku wengine vifo vyao vikihusishwa na kadhia hii ni ndefu
sana.
Hili pia haliwaachi wale ambao wanatajwa kuyasafirisha kutoka eneo moja hadi jingne.
Majina ya wasanii kama Albert Mangweha ‘Ngwair’ na Langa Kileo
waliotutoka hivi karibuni na wale waliokamatwa wakibeba dawa hizo kama
Agnes Gerald ‘Masogange’, Binti Kiziwi na wengine ni ushahidi tosha wa
hili.
Itoshe kusema kwamba, katika kasi ya biashara hii ya dawa za kulevya
inayoendelea sasa, wasanii wamejikuta wako katikati ya muhimili wa
kuathirika na kwa kweli, baadhi wako katika wakati mgumu kwa sasa.
Hata hivyo, maswali yanayobaki kuwa magumu katika vichwa vya wengi ni
kwa nini kwa sasa majina ya wasanii na vijana maarufu (celebrities),
ndiyo yamekuwa yakigonga vichwa vya habari katika biashara hii haramu?
Je, ni kwa kuwa wanaweza kutumia umaarufu wa majina yao kuaminika na
kupita katika vizingiti na vizuizi mbalimbali? Au ni kwa kuwa wana
uhitaji mkubwa sana wa fedha kuliko watu wengine?
Lakini, maswali mengine magumu ya kujiuliza katika hili ni je, wasanii
wetu hawawezi kabisa kuishi kwa kutegemea kazi zao za sanaa bila
kuingia kwenye mitego ya dawa hizi haramu? Je, ni kwa kuwa wanataka
kuishi maisha ya mafanikio kwa njia za mkato?
Maswali haya yanakosa majibu ya moja kwa moja, lakini kwa hakika
yanahitaji kupatiwa majibu ya kina ili kuweza kutibu tatizo hili, ambalo
kwa sasa linaonekana kuwa sugu na kutishia mustakabali wa vijana wengi
nchini.
Hata hivyo ukweli mchungu ambao mtu yeyote akiunganisha nukta kadhaa
na kufanya utafiti mdogo anaweza kupata majibu ni kwamba, wasanii wengi
na hata vijana wameingiwa na tamaa ya kutaka mafanikio ya haraka pasipo
kusota wala kufanya kazi kwa bidii.
Hata wale wanaofanya kazi, wanataka mafanikio ya haraka sana na
yasiyolingana na mikakati (input), wanayoweka hali ambayo inawafanya
waingie kwenye mikakati ya ‘njia za panya’ ambayo mwisho wa siku,
wengine wanajikuta kwenye mzinga wa dawa hizi za kulevya.
Kunaweza kuwa na sababu nyingine nyingi, kama umaskini wa kipato na
ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana, lakini kwa wasanii ambao tayari
wana kazi zinazoweza kuwaingizia kipato, hili la kuishi maisha ya
kuigiza na yasiyo na uhalisia wa vipao vyao linaweza kuwa sababu kuu.
Nilishawahi kueleza katika moja ya makala zangu kwamba, kati ya wajibu
mkuu walionao wasanii kwa sasa ni kuhakikisha kila fedha wanayoipata
kupitia kazi zao inazaa fedha nyingine.
Nilieleza kwamba, inawezekana kabisa kutokana na mazingira yaliyopo
sasa, kazi za sanaa zikawa zinaingiza kipato kisicholingana na kazi zao.
Hata hivyo, hicho kidogo kinachopatikana kama kikiwekezwa katika
miradi mingine, kinatosha kabisa kubadili hali iliyopo na kuwa bora
zaidi.
Nilitoa mifano ya baadhi ya wasanii wakubwa wa Marekani na baadhi wa
hapa nchini, ambao wamekuwa wakijiingiza katika fani nyingine kama za
uigizaji filamu, uuzaji wa mavazi yao, kufungua maduka na kadhalika
katika kutanua mianya ya mapato.
Nilihitimisha kwa kutoa wito kwa wasanii kwamba kwa sasa wengi wao
fedha wanazozipata zimeongezeka tofauti na ilivyokuwa zamani. Malipo ya
maonesho na kazi zao yameongezeka. Urasimishaji wa sekta ya sanaa
umeanza rasmi hivyo hawana budi kuwa chachu ya uchumi wao na wa taifa
kwa ujumla.
Hata hivyo, ni vema nikatanua mjadala sasa kwa kuangalia tatizo
jingine sugu linalozunguka vipato vya wasanii, hivyo kuwafanya kuingia
kwenye vishawishi vya kufanya shughuli haramu za kuwaingizia vipato,
hasa zile za kusafirisha dawa za kulevya, nalo si jingine bali lile la
kuishi maisha yasiyorandana na vipato vyao halisi.
Ni wazi, wasanii wote wa Tanzania hawatoki mbinguni, bali wanapatikana
miongoni mwa familia za kati au duni kabisa, ambazo nyingi
zinawategemea katika kupata mkate wa kila siku na kuendesha maisha.
Kwa maana hiyo, hata maisha ya kila siku wanayoishi, lazima yafanane
na vipato vyao na zaidi familia zao zilivyo. Kinyume chake ni lazima
kusaka vyanzo vingine vya mapato ambavyo vinaweza kuwa halali au
vinginevyo.
Hapa, ndipo huwa kunaleta shaka na utata, hasa wengi wetu tunapotazama
kazi za wasanii na maisha yao ya kila siku wanayoishi. Tunafikia hatua
ya kuhoji ni kwa vipi hasa wanaweza kuweka mizania halisi ya mapato yao
na matumzi yao?
Si vema kuhoji mapato na matumizi ya mtu binasfsi, lakini inapofikia
hatua lawama za kundi la wasanii za kupata mapato kidogo zikiongezeka
huku wakionekana kila uchwao kwenye starehe za gharama sambamba na
kuwepo kwa taarifa za wao kuingia kwenye shughuli haramu kama za dawa za
kulevya, lazima tuanze kuhoji ili kupata majibu sahihi ya nini
kinaendelea.
Tunalazimika kuhoji, maana kuna tatizo kubwa hapa linalohitaji kuwekwa sawa na lisipowekwa sawa ni maafa zaidi mbele ambalo ni la wasanii kuwa na matumizi makubwa yasiyooana na vipato vyao.
Ni tatizo hili la wasanii kuishi maisha yasiyorandana na uhalisia wao,
ndilo limewalazimisha baadhi yao kutumia kila mbinu, kuhakikisha
wanaweza kuishi ‘kimaigizo-igizo’. Mbinu hizi ndizo zimewafikisha
kumezwa na lindi la dawa za kulevya.
Kama nilivyoeleza awali, wasanii wanaingia kwenye lindi la dawa za
kulevya katika njia mbili. Kwanza, ni matumizi yake na pili ni
usafirishaji wake kutoka kona moja hadi nyingine ili kupata fedha za
haraka, kutoka kwa wafanyabiashara wa ‘dili’ hizi haramu.
Ukweli ni kuwa, katika hali ya kawaida, binadamu yeyote anahitaji
kupata mahitaji yote ya muhimu katika maisha. Wanasayansi wanayataja
mahitaji hayo kuwa yanaangukia kwenye mavazi, nyumba, chakula, mapenzi
na kadhalika.
Hata hivyo, upatikanaji wa mahitaji haya na yale mengine ambayo
yamepewa jina la anasa (ziada), hutegemea zaidi uwezo binafsi wa
binadamu husika, vinginevyo kama kipato ni kidogo, hakuna jinsi, unaweza
kuyapata labda kwa kutumia njia za panya na haramu.
Kwa vijana na wasanii wengi suala la kutaka maisha ya gharama kubwa
kuanzia vyombo vya usafiri, mavazi, mitoko ya usiku, vifaa wanavyotumia
na kadhalika ni jambo la kawaida sana.
Haishangazi kwa vijana na wasanii wengi kukesha maeneo mbalimbali ya
klabu za usiku kwa matumizi makubwa ya fedha huku wengine wakiishi
katika ufahari ambao kwa mazingira ya kawaida ya Tanzania si rahisi
kuyamudu na kuyaishi kwa muda mrefu.
Suala hapa si kuvipata vitu hivyo vya gharama, suala ni je, uwezo wa
kuvipata vitu hivyo unatoka wapi? Utadumu kwa muda gani? Na kwa vipi mtu
ataweza kuishi maisha yasiyorandana na jamii inayomzunguka?
Maswali haya ndiyo yanapaswa kuwa dira kwa wasanii na vijana wa
kisasa, ambao ndoto ya kutaka kuishi maisha ya juu na yasiyofanana na
vipato vyao halisi, ndiyo yanayosababisha kuangukia kwenye shughuli
haramu na za kutisha.
Kwa ujumla, kuwa maarufu ni jambo moja lakini kuweza kuumiliki na
kuuishi umaarufu ni jambo jingine tofauti. Hapa ndipo tatizo lipo kwa
vijana na wasanii wetu wengi.
Maana, wanaamini umaarufu ni kuwa tofauti na wengine na kuishi maisha
ya gharama kuzidi wengine. Haiwezekani, maana tuko Tanzania hii hii na
kipato chetu ni hiki hiki.
Wasanii na vijana wakifika mahali wakatambua kwamba hakuna jinsi
wanaweza kuishi maisha yasiyooana na vipato vyao na zaidi jamii
inayowazunguka, wataweza kuepuka mitego ya kuingizwa kwenye wimbi la
dawa za kulevya.
Via Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment