MWALIMU Mkuu wa Shule ya Msingi Chalinze Mzee, wilayani
Bagamoyo, Mkoa wa Pwani, Elias Kapama, yuko katika wakati mgumu baada
ya kuhamishia ofisi yake kwenye vyoo vya wanafunzi kutokana na jengo la
ofisi yake kuharibika vibaya.
Hatua ya kuhamia chooni ilitokana na mkuu huyo kutawaliwa na hofu ya
ubovu wa ofisi yake, hivyo kushindwa kufanya kazi zake kwa ufasaha
unapotokea upepo au mvua.
Novemba 2012, Kapama alihamishia ofisi yake katika jengo la vyoo vya
wanafunzi ambavyo havijaanza kutumika tangu ujenzi wake ukamilike mwaka
2011.
Akizungumzia hali hiyo, Kapama alisema kuwa anajisikia vibaya kutumia
chumba maalumu cha kubadilishia nguo cha wavulana katika choo hicho
kutokana na kukosa msaada kutoka halmashauri ya wilaya hiyo.
Alisema kuwa ni miezi tisa sasa tangu ahamishie ofisi yake chooni na
hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na ngazi ya wilaya pamoja na
kufahamu mazingira hayo, hali aliyodai kuwa inamweka katika wakati
mgumu.
“Sina ofisi, nimelazimika kuomba kwa wafadhili waliotujengea vyoo kwa
ajili ya wanafunzi niweze kutumia chumba hiki cha kubadilishia nguo kama
ofisi yangu hadi pale tutakapojenga ama kufanyia ukarabati ofisi ya
zamani,” alisema.
Vyoo hivyo ambavyo vimejengwa kwa ufadhili wa Taasisi ya Ebenezer
Spritual Center ya mjini Chalinze, vimegharimu kiasi cha sh milioni 70
hadi kukamilika.
Mkuu huyo aliongeza kuwa kwa sasa walimu wanatumia tundu moja la choo
huku wanafunzi 450 wakitumia matundu saba, matatu kwa wanawake na manne
kwa wavulana.
Hata hivyo Tanzania Daima ilishuhudia choo hicho kinachotumika sasa kikiwa hakina hadhi na usalama kwa watumiaji.
Aliuomba uongozi wa wilaya pamoja na wizara ambao umetembelea shule
hiyo na kushuhudia mazingira hayo magumu kufanyia utekelezaji wa ujenzi
wa ofisi hiyo haraka ili aweze kuhama kutoka chooni.
0 comments:
Post a Comment