WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki 

 WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki amesema kuwa mgogoro wa ardhi kwa wakazi wa Loliondo unachochewa na maslahi binafsi ya wawekezaji.

Balozi Kagasheki alimtaja mmiliki wa mtandao wa Shirika la Kimataifa la Utetezi wa Mazingira (AVAAZ) kutoka Uingereza kuwa anazitumia baadhi ya asasi nchini kwa maslahi binafsi ili kushinikiza kampuni ya kiarabu ya Otterlo Business Corporation Ltd (OBC) iliyomilikishwa eneo kihalali mwaka 1974 inyang’anywe.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kufafanua juu ya mgogoro wa ardhi unaofukuta Loliondo kati ya serikali na wafugaji wa jamii ya Kimaasai, Kagasheki alisema AVAAZ kupitia baadhi ya asasi na wanasiasa wamekuwa wakieneza uongo kwa wananchi hao.

Waziri alifichua kuwa aliwahi kupigiwa simu na mmiliki wa mtandao huo kutoka Uingereza akimtaka kufanikisha kumfukuza mmiliki wa Kampuni ya OBC na kumuahidi kuwa endapo akifanikiwa, yeye atawekeza eneno lote la ardhi.

“Mimi nilishangaa huyu anayejiita mmliki wa mtandao wa AVAAZ alithubutu kunipigia simu, kunilazimisha kumfukuza mwekezaji huyo mwenye asili ya Kiarabu, akasema endapo nitafanikiwa atahakikisha anawekeza eneo lote yeye kwa kuwa wana tofauti zao,” alisema.

Kagasheki aliongeza kuwa wakati akiendelea kumshawishi alimuuliza kuwa; “kama ningekuwa Waziri wa Maliasili nchini mwako ungeweza kuniuliza swali kama hilo?”

Alisema kuwa alimuuliza kama aliwahi kufika Tanzania na anaifahamu Loliondo, lakini alijibu “hapana”, akaona ni chuki tu ambazo anawatumia Watanzania katika kuvuruga amani Loliondo.

Waziri Kagasheki alisema mkanganyiko unaotokea hivi sasa ni kutokana na Waziri wa Ardhi aliyekuwepo mwaka 1994 kugawa hati juu ya hati.

Alisema hata hivyo wananchi wanatakiwa kufahamu kuwa ardhi wanayoimiliki ni mali ya rais, hivyo hakuna mtu yeyote ambaye anaweza kumuendesha wala kuiendesha serikali.

“Nasema na endapo serikali itakaa kimya na kuwanyamazia watu kuingia katika maeneo tengefu yenye vyanzo vya maji, mazalia ya wanyama na njia ya wanyama basi katika kipindi cha miaka 20 ijayo hakutakuwa na kitu cha kujidaia,” alisema.

Aliongeza kuwa kila sehemu ina sheria yake na serikali haiwezi ikatoa uamuzi kwa ajili ya kugandamiza wananchi wake, hivyo kama kutakuwa na upindishaji wa sheria yeye atakuwa tayari hata kwenda mahakamani na kwamba anafanya hivyo si kwa shinikizo au kuogopa yeyote.

Kuhusu kauli ya Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Mwigulu Nchemba kuwa serikali ilikosea kumega eneo hilo, Kagasheki alisema chama hakikumtuma kwenda kutoa uamuzi.
Alisema kuwa Nchemba alitumwa na chama kwenda kuangalia hali ya wanachama wake wamepokeaje msimamo wa serikali.

Waziri alifafanua kuwa hata hivyo hafikirii kama Nchemba angekwenda kule na kutoa uamuzi wowote.

“Nchemba hakutumwa kutoa maamuzi yoyote, ninachofahamu chama kama chama kimemtuma kwenda kuona wanachama wamepokeaje msimamo wa serikali na kukusanya maoni yao. Kauli yoyote aliyoitoa ni yake binafsi si ya chama,” alisema.

Kagasheki pia alizungumzia historia ya Loliondo ambapo alisema mwaka 1974 serikali kupitia Wizara yake ya Maliasili na Utalii kwa kupitia Tangazo la Serikali No 269, na kwa kuzingatia sera yake ya uhifadhi inayosifika duniani kote, ilitangaza kwamba kilomita za mraba 4,000 katika eneo la Loliondo litakuwa pori tengefu.

Hivi karibuni serikali ilifanya uamuzi wa kuliondoa eneo la kilomita za mraba 2,500 kutoka pori tengefu la Loliondo na kuwapatia wananchi ili walimiliki kisheria na kuitumia ardhi hiyo kwa hiyari yao kwa ajili ya kuwaletea maendeleo.

Hata hivyo, alisema kuwa serikali itaangalia namna ya kuwawezesha wafugaji hao kuanzisha WMA ambazo zitawasaidia katika kujiinua kiuchumi.

Pia alishangazwa na kasi za kuongezeka kwa NGO’s ambazo kwa sasa zimefikia 37 huku akieleza kuwa hata Wamaasai ambao ni wafugaji, wengi wao wametokea Kenya si Watanzania.
Chanzo: Tanzania Daima
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top