Waombolezaji wakipiga mayowe kando ya gali liliokuwa limebeba maiti ya polisi aliyeuawa kwenye ghasia.

Waziri mkuu mpya wa Misri, Hazem al-Beblawi anaanza kibarua cha kuteua baraza la mawaziri , wiki moja baada ya kuondolewa mamlakani kwa rais Mohammed Morsi.

Hii ni katika hatua ya kujaribu kuleta maridhiano na Hazem El Beblawi amesema atatoa viti vya uwaziri kwa vuguvugu la Muslim Brotherhood linaloongozwa na aliyekuwa rais wa taifa hilo Mohammed Morsi.
Hata hivyo mmoja wa viongozi wakuu wa vuguvugu hilo ameiambia BBC kwamba hawatashiriki katika serikali yoyote hadi pale kiongozi wao Mohammed Morsi atakaporejeshwa mamlakani.

Taarifa hiyo inajiri wakati ambapo Jeshi la Misri limeonya dhidi ya jaribio lolote la kuvuruga kipindi hicho cha mpito.

Bwana Beblawi anatarajiwa kutoa nafasi za kazi za uwaziri kwa vuguvugu hilo licha ya kusema kuwa haliko tayari kushiriki katika serikali ya mpito kufuatiua hatua wanayosema ni ya jeshi kumpindua Morsi.

Brotherhood wamesema hawataunga mkono mpango wa serikali hiyo kuandaa uchaguzi mpya hadi pale mageuzi yatakapofanyika.

Marekani imesema inaunga mkono ingawa kwa makini hatua ya kupendekeza mageuzi.

Ratiba iliyotolewa ya maandalizi ya uchaguzi mpya, ilitangazwa na rais wa muda, Adly Mansour siku ya Jumatatu masaa kadhaa baada ya angalau watu 51 kuuawa wengi wao wakiwa wa chama cha Muslim Brotherhood. Waliuawa wakiwa nje ya kambi ya jeshi wanakoamini kuwa Morsi anazuiliwa.

Amri ya rais wa mpito inalenga kubuni jopo maalum litakalofanyia marekebisho  katiba katika kipindi cha wiki mbili.

Huku watu wakiendelea kuvutana, hofu nayo inaongezeka sio tu kuhusu kuokoa mapinduzi bali nchi nzima.
Chanzo: BBC Swahili
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top