Mwanasheria wa Kenya, Dola Indidis
Mwanasheria wa Kenya ameanzisha mchakato wa kupinga mateso na
hukumu ya kifo kwa Yesu Kristo, akisema kwamba ilikuwa kinyume cha
sheria na kwamba Israel na baadhi ya mataifa yanatakiwa kuwajibika.
Mwanasheria huyo, Dola Indidis (pichani) ambaye
aliwahi kuwa msemaji wa Mahakama nchini Kenya amesema kwamba amefikisha
shauri hilo kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), International
Court of Justice, iliyopo The Hague, Uholanzi.
Indidis katika mashtaka yake anahoji kesi isiyo ya haki dhidi ya Yesu, kifungo, adhabu na kifo chake.
Agosti 2007 alifungua kesi hiyo kwenye Mahakama
Kuu ya Nairobi kwa niaba ya ‘Marafiki wa Yesu.’ Hata hivyo mahakama
mwaka 2011 ilitoa uamuzi kwa kusema haina mamlaka na kumwomba mtoa
maombi kwenda ICJ.
Indidis anataka ifahamike ni uhalifu gani alifanya
Yesu hadi kufikia hatua ya kushtakiwa, na anaitaka mahakama itamke kuwa
‘mwenendo wa mashtaka dhidi ya Yesu haukufuata taratibu za kisheria kwa
wakati huo na hata sasa.’
“Mahakama (ICJ) imewasiliana na mimi. Sasa nasubiri tarehe ya kwenda Uholanzi kusikiliza kesi hiyo,” alisema Indidis.
Indidis aliendelea kusema: “Nimefungua kesi hii
kwa sababu ni jukumu langu kuenzi heshima ya Yesu na nimekwenda ICJ
kutafuta haki kwa ajili ya mtu kutoka Nazareth. “Kesi hii siyo kwa
masuala ya kilokole. Ni kuhusu sheria na ni jukumu la mahakama kusadia
maendeleo ya sheria,” alisema Indidis.
Alisema amekwenda ICJ kuhoji hukumu aliyopewa Yesu, kwamba alihukumiwa kwa makosa na alituhumiwa bila kufanya kosa lolote.
Indidis alisema japokuwa walalamikiwa wengi kwa
sasa ni marehemu, bado anaona uzito wa kesi na kwamba itaweka utaratubu
kwa siku za baadaye.
Kesi hiyo kwa mara ya kwanza ilifikishwa Mahakama
Kuu ya Kenya chini ya kifungu namba 65 na 67 cha Katiba ya Kenya (ambayo
sasa imerekebishwa).
Walalamikaji katika kesi hiyo ni Marafiki wa Yesu
kupitia kwa Dola Indidis, ambao wanawashtaki mtawala wa Roma Tiberius,
Pontius Pilate (Pilato) ambaye ni Gavana wa Judea, Annas, Padri Mkuu wa
Wayahudi, kiongozi wa Wayahudi, Walimu wa sheria wa Kiyahudi, Mfalme
Herod, Jamhuri ya Italia na Taifa la Israel.
Kwenye kesi hiyo taasisi ya kiraia ya kutetea haki
ya Kenya na Humprey Odanga Achala, wameorodheshwa katika sehemu ya watu
wenye masilahi na kesi hiyo. Alisema ametumia kifungu cha Marafiki wa
Yesu kwenye Agano Jipya kufungua kesi hiyo.
Walalamikaji wamezitaja nchi za Italia na Israel kwakuwa nchi
hizo hata baada ya uhuru zimeendelea kutumia sheria za Utawala wa Roma
na zile zilitotumika kumsulubu msalabani Yesu.
Padri Mkuu wa Wayahudi Caiaphas anatuhumiwa
kumkamata Yesu, kumshtaki kwenye mahakama isiyo halali (Kangaroo Court),
na kumtia hatiani kwa mashtaka ya kidini yaliyoangukia kwenye adhabu ya
kifo na hakutaka Yesu ahoji mamlaka yake.
Alidai Pilato hakumtia hatiani Yesu, lakini alitoa hukumu ya kumuua ili kuleta amani.
“Haikuwa sahihi Pilato kushuhudia mtuhumiwa
akipigwa,” alisema Indidis na kuongeza kuwa, “Jaji lazima alisimamie
haki za watu wote na aina zote za ukiukwaji wa sheria.”
“Miongoni mwa waliokuwepo walimshambulia usoni,
walimtemea mate, walimzaba vibao, walimdhihaki, na kumwona kuwa mtu
anayestahili kifo,” alisema.
Mlalamikaji pia alihoji mfumo wa maswali
yaliyotumika wakati wa kesi, uchunguzi, wakati kesi ikisilikizwa na
hukumu kwa Yesu Kristo, adhabu alizokuwa akipewa wakati kesi ikiendelea
na ukweli wa taarifa zilizotumika kumtia hatiani. Alisema kilichofanyika
ni uvunjaji wa haki za binadamu. “Yesu alikuja duniani kama binadamu.
Sasa hakupewa fursa ya kusikilizwa na hakuna aliyezungumza kwa niaba
yake.”
Indidis alisema ametumia miaka 10 kuifanyia kazi
kesi hiyo, ikiwamo kukusanya ushahidi kutoka kwenye Biblia. “Ushahidi
wote umo kwenye kumbukumbu za Biblia, huwezi kuidharau Biblia,”
aliongeza Indidis.
Alisisitiza kwamba hata baada ya Yesu kufa,
haikutolewa nafasi yoyote kusikilizwa kwa rufaa ya aina yoyote, hivyo
yeye ameamua kufanya hivyo akiwa kama ‘rafiki’.
Alizungumza kuhusu kesi hiyo, mmoja wa maofisa wa
ICJ alisema mahakama hiyo haina mamlaka kuhusiana na kesi ya aina hiyo
kwa sasa kwa kuwa inajihusisha zaidi na kesi baina ya nchi na nchi,
hivyo ni vigumu kuishughulikia kesi ya aina hiyo.
Mwananchi
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment