Serikali kupitia wizara ya maji imepania kuondoa vibali vinavyotolewa na Wizara hiyo katika kupata Wakandarasi, Wataalam, Washauri na kupitisha taarifa za usanifu ili kutekeleza kwa haraka miradi mbalimbali ya maji nchini.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Nurdin Ndimbe kutoka Wizara ya Maji wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es salaam.

Aidha Nurdin alisema ili kuboresha mfumo wa ufuatiliaji wizara imeunda chombo cha ufuatiliaji kinachoitwa Ministerial Delivery Bureau kikiwa na dhumuni la kuboresha na kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa na Wizara hiyo inatekelezeka ndani ya mda uliopangwa.

Naye Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Rasilimali Maji kutoka Wizara hiyo Naumia Rupime amewataka wananchi kuacha kuchimba visima kiholela badala yake wafuate taratibu  na sheria zilizowekwa ili kuondoa kero mbalimbali zinazoweza kujitokeza.

Amesema wananchi wamekuwa wakichimba visima kiholela na kuuza maji bila kufuata taratibu ikiwa ni kwenda kwa msajili wa mabonde katika eneo husika au bila ya kupeleka sampuli ya maji yaliyochimbwa katika Maabara ili kuthibitisha usalama wa maji hayo

Jumla ya miradi ya maji kwenye vijiji 682 ikiwa ni wastani wa vijiji 5 kwa kila Halmashauri vipo katika hatua mbalimbali ya utekelezaji. Ifikapo mwezi Septemba 2013 ujenzi wa miundombinu ya maji utakuwa umekamilika  ambapo jumla ya watu milion 1.7 wanatarajiwa kupata huduma ya maji
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top