Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe akiwaonesha wananchi kitabu kinachoonesha matukio mbalimbali waliyofanyiwa Wanachadema alipokuwa akihutubia umati wa wananchi mjini Songea juzi.

VYAMA vikubwa viwili hasimu hapa nchini, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) vimeingia katika ‘vita’ mpya.

Wakati CCM ikituhumiwa kutumia dola na msajili wa vyama vya siasa ‘kukishikisha’ adabu CHADEMA, likiwamo tamko zito la kutaka kukifuta kwa madai ya kuhatarisha amani nchini, chama hicho pinzani kimeapa kupambana na yeyote kwa gharama zozote dhidi ya kile walichokiita dhuluma, uonevu na ukandamizaji wa haki za binadamu kunakofanywa na serikali.

Akihutubia katika mji wa Songea kwa mara ya kwanza tangu kuachiwa kwa dhamana makao makuu ya polisi na kunusurika kwa bomu katika mkutano wa kufunga kampeni jijini Arusha hivi karibuni, Mwenyekiti wa taifa wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alisema sasa chama hicho kitaongeza kasi ya mapambano bila kumwogopa yeyote.

“Sitamuogopa rais, lakini nitamheshimu, sitaogopa polisi lakini nitawaheshimu, sitaogopa Jeshi lakini nitaheshimu Jeshi.

“Kuanzia sasa sitamheshimu mtu yeyote asiyeheshimu ubinadamu wa mtu mwingine. Uchaguzi wa juzi wa kata, tumeshinda kwa mapambano ya damu. Watu wetu wamepigwa kila mahali, wamekatwa mapanga na mashoka na vijana wa CCM, Green Guard.

“Katika hali kama hiyo siwezi kucheka na polisi, ndiyo maana juzi tumetangaza kuwapatia vijana wetu mafunzo ya ukakamavu ili tujilinde na vitendo hivi. Hatujaanzisha jeshi, tulichokisema na kukisimamia ni hiki.

“Wananchi wa Songea, huu ni mkutano wangu wa kwanza kuhutubia hadharani tangu nilipokoswa koswa kuuawa kwa bomu, risasi za SMG na risasi za bastola kwenye tukio la Soweto, Arusha siku ya kuhitimisha kampeni.

“Lakini napenda niwaambie kitu kimoja, miye kama kamanda wenu mkuu, sitaingiwa hofu. Sasa tuna usongo zaidi na wametuongeza charge (nguvu) ya kuing’oa CCM katika chaguzi zijazo, maana tunajua tunasimamia haki, ukweli na matumaini ya Watanzania wote,” alisema.

Huku akiwatoa machozi baadhi ya waliohudhuria mkutano huo wa juzi, baada ya kuona kitabu kimojawapo chenye picha za watu waliouawa na kuteswa na vijana wa Green Guard ya CCM, Mbowe aliuita ushindi wa kata nne za jijini Arusha kuwa ni wa damu zilizomwagika za wanachama wake.

“Kama kuna mtu alifikiri kuwa kumuua au kutaka kumuua Mbowe atamtia hofu...huyo mtu ameshindwa. Kwa kweli siku ile mimi na wengine tuliokuwa walengwa kabisa wa lile tukio tulinusurika kwa mipango ya Mungu tu. Ni kwa sababu tunaongozwa na Mwenyezi Mungu, tutaendelea kupigania haki hadi kieleweke.

“Huko Serengeti, kwenye Kata ya Machila, watu wetu wake kwa waume wametekwa nyara, wakapelekwa na kufichwa kwenye nyumba ya CCM, wengine wamebakwa, wengine wamewekewa chupa sehemu za siri, kwa sababu tu ya CHADEMA,” alisema.

Mbowe alidai kuwa amesikitishwa na upotoshaji mkubwa unaofanywa kwa makusudi na CCM na serikali kwamba chama chake kimeanzisha jeshi, kiasi cha kuvisukuma vyombo vya dola kuanza kuwakamata viongozi wa juu wa chama hicho.

“Hatuwezi wala hatuna mpango wa kuanzisha jeshi kama ambavyo polisi wanataka kupotosha kwa kusoma habari zinazoandikwa na magazeti ya CCM na kutangazwa na TBC.

“Nani hajui kuwa CCM wana kikundi kinaitwa Green Guard ambacho kiko nchi nzima, kinapiga wananchi, kinaumiza wapinzani na ushahidi tunao wa kutosha, kinapewa mafunzo ya kijeshi na ushahidi tunao.

“CHADEMA tumeshalalamika na kulia mara chungu nzima kuwa si sahihi vitendo hivi kuendelezwa, hakuna anayetusikiliza, si polisi wala si serikali. Wote wamekaa kimya. Wakati mwingine vitendo hivi vinafanywa mbele ya usimamizi au macho ya polisi, kila siku wanaoumizwa ni CHADEMA. Sasa tukasema basi, kuendelea kulialia ni uendawazimu,” alisema.

Mbowe alisema walichokiamua ni kufanya ulinzi shirikishi au ulinzi jamii kama ambavyo polisi wamekuwa wakiasa na kusihi kila siku.
“Tulichokisema wala si kitu kipya kabisa. Kimo ndani ya katiba yetu. Naomba mtu yeyote hapa anayeweza kusoma apande hapa juu asome hii katiba ya chama hapa, inazungumzia Red Brigade. 

Tunachofanya sasa hivi ni kuwapatia vijana ukakamavu. Hatuanzishi  jeshi, wala hatutakuwa na mabomu, wala bunduki, shoka, wala mapanga kama walivyo wenzetu, lakini kama ni mchaka mchaka au karate tutapiga.

“Mtu yeyote mwenye nia mbaya na nchi yake hawezi kutangaza hadharani, na sisi kwa kuwa nia yetu ni njema na yenye lengo la kujilinda ndiyo maana tulitangaza mchana kweupe,” alisema Mbowe.

Onyo kwa Tendwa
Kadhalika, CHADEMA kimemwonya Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, asijaribu wala kuthubutu kukifuta chama hicho na kudai kuwa hatua hiyo itasababisha maafa nchini.

Mbowe alisema tamko la Tendwa linadhihirisha kile alichokiita ulevi wa madaraka na kama angelikuwa chini ya uongozi makini alipaswa kufukuzwa kazi mara moja kwa kauli zake zinazohatarisha demokrasia na amani ya nchi.

“Kauli za Tendwa zinazidi kuiponza serikali. Hazitawasaidia hata kidogo. Sasa kauli ya Mbowe ambayo naomba imfikie Tendwa ni hii, ajaribu kufuta CHADEMA aone moto wake.

“Unajua anaposema atafuta CHADEMA, maana yake ni kwamba anafuta Kambi ya Upinzani Bungeni, anafuta wabunge wote, hivyo uitishwe uchaguzi. Anafuta madiwani 600 na zaidi nchi nzima, hivyo uchaguzi urudiwe; anafuta wenyeviti wa vijiji, mitaa, vitongoji na wajumbe wao...huyu mtu amelewa madaraka, ajaribu aone moto,” alisema Mbowe.

Upotoshaji wa amani
Mbowe alisema kuwa kuna propaganda ambazo ama zinafanywa kwa makusudi au kwa kutokujua, zikipotosha maana nzima ya amani ambayo kila Mtanzania hana budi kuipigania.

Akimnukuu Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, kwenye moja ya hotuba yake aliyowahi kuitoa mwaka 1986, Ukumbi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Dar es Salaam, Mbowe alisema kama jamii haina wala haioni matumaini kwa viongozi wao huku haki zikiminywa, amani haiwezi kudumu.

“Suala la amani linafanyiwa upotoshaji mkubwa siku hizi. Ukisikiliza baadhi ya redio siku hizi unasikia wamerekodi sauti sijui ya kiongozi au mtu mashuhuri katika nchi, wanazungumzia amani, amani, amani, utafikiri amani inapatikana kwa kuimbwa kama ngonjera. Amani ina misingi yake. Misingi hiyo ikiwekwa au ikitekelezwa amani itadumu tu.

“Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliwahi kuhutubia akisema kuwa wakati anang’atuka madarakani aliacha nchi ikiwa na amani, si kwa sababu watu hawakuwa maskini, umaskini ulikuwepo, lakini kulikuwa na amani. Alisema ni kwa sababu watu...wananchi walikuwa na amani na serikali yao. Walikuwa na matumaini na viongozi wao, walikuwa wana amini katika Azimio la Arusha, walikuwa wana matumaini ya haki katika nchi yao.

“Mwalimu anasema wananchi walikuwa maskini, lakini walikuwa na matumaini kwa sababu serikali yake ilikuwa imejenga usawa kwa binadamu, kulikuwa na heshima kwa mkubwa na mdogo, mdogo na mkubwa. Ilikuwa imeweka misingi ya haki na matumaini, ndiyo ilikuwa ikibeba na kulea amani yetu wakati ule. Sasa vitu hivyo havipo.

“Wananchi wakipoteza vitu hivyo, vikikosekana, amani inayodaiwa kuwepo inakuwa sawa na volkano inayotikisika chini ya ardhi, inaweza kulipuka wakati wowote. Sasa tunawaambia watawala wasiende majukwaani tu kuhubiri amani...waweke miundombinu ya matumaini na haki kwa wananchi wote, bila kujali dini zao, makabila yao, rangi zao, wala maeneo wanayotoka.

Alisema wananchi wanahitaji kuona matumaini katika elimu yao, elimu ya watoto wao, wananchi wanasumbuliwa na gharama za maisha zinazopanda kila kukicha, tofauti za kipato zinazidi kuwa kubwa, wanataka wakienda mahakamani watendewe haki, vinginevyo amani inayohubiriwa kwa maneno tu bila miundombinu ya matumaini na haki, itakuwa ni amani ya muda mfupi tu,” alisema Mbowe.

Katiba mpya
CHADEMA pia imeisuta CCM kwa kukataa masuala mengi ya msingi yaliyopendekezwa na Tume ya Jaji Joseph Warioba.
“Bahati mbaya sana, mambo yote haya manne ambayo kwa kweli ni muhimu sana yakawemo kwenye Katiba mpya ya Watanzania, CCM wanayapinga. Kwanza, kuna suala la maadili na miiko ya viongozi, pili kuna suala la tunu za taifa, tatu haki za binadamu na nne ni serikali tatu.

“Haya ni kati ya mambo ya muhimu sana ambayo sisi CHADEMA tunaona ni vema yakatajwa na kuzingatiwa kwenye Katiba mpya, lakini jamaa hawa (CCM) hawayataki au mengine eti wanataka yasitajwe kwenye Katiba mpya bali yaundiwe sheria.

“Yaani jamaa hawa wanahofu, hawataki mambo ya tunu za taifa kama vile uwazi, ili mikataba hii mibovu iliyopo kila mahali iwe mwisho, wanapinga hata haki za binadamu, serikali tatu ndiyo balaa kabisa, wanajua wameondoka,” alisema.

Aliongeza kuwa chama hicho kitazunguka nchi nzima kuunda mabaraza yake ya katiba ambayo siku nzima wananchi wa eneo husika watajadili rasimu ya Katiba mpya wakitoa maoni yao.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top