Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba.

 JINAMIZI la kashfa za ufisadi limeendelea kuwaandama Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye sasa ni Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM), kuwa ndio waliouza nchi katika utawala wao.

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, ndiye aliyewataja viongozi hao kuuza nchi kwa wageni wanaochimba madini yanayowanufaisha zaidi wageni kuliko Watanzania.

Profesa Lipumba alitoa kauli hiyo jana jijini Mwanza alipokuwa akijibu swali la mwandishi wa Tanzania Daima Jumapili, muda mfupi baada ya kuahirishwa kwa muda mkutano wa kujadili na kuchangia mawazo juu ya maendeleo kwa wote katika Mkoa wa Mwanza.

“Kizazi hiki na kijacho viwatupie lawama Mkapa na Chenge, hawa wameliingiza taifa kwenye mikataba ya unyonyaji ya sekta ya madini inayowaneemesha zaidi Wazungu wanaojua thamani na umuhimu wa dhababu kuliko Watanzania wenye ardhi inayotoa madini husika,” alisema.

Alibainisha kuwa Tanzania inatafunwa na saratani mbaya ya mikataba mibovu ya madini iliyoasisiwa na Mkapa kwa kushirikiana na Chenge katika utawala wa Awamu ya Tatu iliyosifika kwa sera ya ubinafsishaji wa mali za umma zilizokabidhiwa kwa wawekezaji wengi wao kutoka nje ya nchi.

“Kimsingi, huwezi kuishtaki kampuni katika sheria za kimataifa, maana serikali ndiyo iliyosaini mikataba hiyo ya kinyonyaji na kampuni kwa niaba ya wananchi wake. Uzalendo haupo kwa viongozi wetu.”

“Mkapa na Chenge, hawa watu ndio walioiuza nchi kwa kusaini mikataba yenye utata ambayo nchi inapewa mrabaha wa asilimia tatu huku asilimia zilizobaki zikienda kwa wawekezaji,” alisema.

Profesa Lipumba aliwataka Watanzania kukomesha unyonyaji na udhalimu wa rasilimali zao kwa kuweka vipengele kwenye Katiba mpya vitakavyofuta mikataba yoyote ile itakayobainika kuingiwa kwa lengo la kunufaisha watu wachache.

Alibainisha kuwa anashangazwa na kitendo cha baadhi ya kampuni za uchimbaji madini kudai mara kwa mara kwamba zinajiendesha kwa hasara lakini haziondoki nchini.

Profesa Lipumba alisema unyonyaji wa rasilimali za taifa hasa katika sekta ya madini unaofanywa na wageni unatokana na baraka ya serikali ya CCM iliyokaa madarakani kwa muda mrefu.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, licha ya madini kuwa na soko kubwa nje ya nchi Tanzania bado haijanufaika vya kutosha na rasilimali hiyo.

Awali, akitoa mada yake kwenye mkutano huo ulioandaliwa na CUF kwa kushirikiana na Chama rafiki cha Redikale Venstre cha nchini Denmark, Profesa Lipumba alisema katika sekta ya madini hapa nchini, dhahabu ndiyo inayoongoza kwa mauzo makubwa nje ya nchi.

Baadhi ya washiriki wa mkutano huo waliituhumu serikali ya CCM, kwa kuonekana kushindwa kuweka mfumo mzuri wa kulinda rasilimali za nchi, badala yake Tanzania imegeuzwa kama shamba la bibi.

Mmoja wa washiriki hao, Said Tembo, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Muungano wa Machinga jijini Mwanza, alisema misingi ya kulinda na kutunza rasilimali za nchi iliyoachwa na Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere imetelekezwa na watawala wa sasa.

Tembo aliongeza kwamba: “Wakati Nyerere akitafuta uhuru wa nchi hii alitaka wananchi wajitawale na wamiliki uchumi wao mzuri kwa faida. Lakini kwa sasa watawala wetu wana mwelekeo wao...uadilifu na uzalendo haupo kwa viongozi wetu.”
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top