MKOA wa Mjini Magharibi unakabiliwa na changamoto kubwa ya kuwepo kwa ongezeko la wakazi lisilolingana na ongezeko la mahitaji ya huduma kwa wakazi hao.
 
Akizungumza na viongozi na watendaji wa Serikali katika ukumbi mikutano Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo mara baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji majukumu ya Mkoa, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa ongezeko hilo linaongeza uzito wa majukumu kwa uongozi wa mkoa.
 
“Mkoa unakabiliwa na mtihani mkubwa katika kuwahudumia wananchi hawa wanaoongezeka mwaka hadi mwaka kutoka watu 391,002 mwaka 2002 hadi watu 506,907 hivi sasa kwa mujibu wa makadirio ya wataalamu wa takwimu”alifafanua.
 
Dk. Shein aliongeza kuwa huduma nyingi katika mkoa huo kama vile maji na umeme hazitoshelezi lakini alibainisha kuwa kumekuwepo na jitihada mbalimbali kukabiliana na matatizo hayo na kutolea mfano miradi ya maji na umeme inayoendelea hivi sasa katika mkoa huo na sehemu nyingine za Unguja na Pemba.
 
Rais wa Zanzibar ambaye yuko katika ziara ya siku mbili katika mkoa mjini Magharibi ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kutembelea mikoa yote ya Zanzibar pia, alikagua mradi wa uchimbaji visima huko Chumbuni pamoja na mradi wa Umeme Welezo.
 
Akiwa katika mradi wa maji wa uchimbaji visima huko Chumbuni Wilaya Mjini Dk. Shein aliutaka uongozi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kuhakikisha usalama wa vyanzo na miradi ya maji ikiwemo kufanya jitihada za kuwaelimisha wananchi kulinda vyanzo na vifaa vya miradi.
 
“Tuilinde vizuri sehemu hii (visima vya maji) ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha wananchi ili washiriki katika kulinda miundo mbinu hii ya maji”aliagiza
 
Nae Mkurugenzi Mkuu wa ZAWA Dk. Mustafa Ali Garu alimueleza Rais na ujumbe wake kuwa mradi wa visima tisa unatekelezwa kukabiliana na tatizo la kupungua kwa kiasi kikubwa wa uzalishaji maji katika chemchem mbili kuu za Mwanyanya na Mtoni.
 
“Tangu kuanza utekelezaji wa mradi huu mwezi Agosti mwaka 2011 visima vitano vimeshachimbwa katika maeneo ya Chumbuni na Saateni na kwamba uzinduzi unatarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu”alieleza Dk. Garu.
 
Akijibu swali la Rais kuhusu uwezo wa visima hivyo kutoa maji Dk. Garu alieleza kuwa visima hivyo vinatarajiwa kutoa maji kwa kiwango chake kwa muda wa miaka thelathini (30).
 
Wakati huo huo, Dk. Shein alitembelea Mradi wa uimarishaji huduma za umeme huko Welezo, Wilaya ya Mjini na kuona hatua za mradi zilizofikiwa za mradi huo.
 
Dk. Shein alipongeza hatua hizo zilizofikiwa hali ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa kutoa huduma ya uhakika ya umeme kwa wananchi pale mara tu mradi huo utakapoanza rasmi kufanya kazi.
 
Kituo hicho ni miongoni mwa vituo vitatu ambacho tayari kimeshaharimu Tsh. Bilioni 7.
 
Kwa Maelezo ya Meneja wa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), Bwana Hassan Salum alisema kuwa kituo hicho kitasaidia kutoa huduma ya umeme kwa maeneo ya Kilimahewa na maeneo ya kusini yakiwemo Mwera, Bambi, Koani na mengineyo. TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top