Na Isaac
Mwangi, EANA
Arusha, Machi 6, 2013 (EANA) – Waangalizi wa Kanda katika uchaguzi mkuu
wa Kenya wameonyesha kuukubali mwenendo wa upigaji kura Jumatatu kuwa ulikwenda
sawia na kutaka hali hiyo iendelee katika hatua nyingine zilizobaki za uchaguzi
huo.
Taarifa hiyo imetolewa na Timu ya Pamoja ya Waangalizi wa Kanda kutoka
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Soko la Pamoja la Nchi za Mashariki na
Kusini mwa Afrika (COMESA) na Mamlaka ya Maendeleo Afrika (IGAD), Shirika Huru
la Habari la Afrika Mashariki (EANA) limeripoti.
‘’Ingawa kulikuwepo na changamoto kadhaa kuhusu uhakiki wa wapiga kura, timu
hiyo imehitimisha kwamba uchaguzi mkuu wa 2013 umefikia viwango vya kanda, bara
na vya kimataifa kuwa ni wa kuaminika na uwazi,’’ ilieleza taarifa iliyotolewa
Jumanne.
Taarifa ya awali ya
waangalizi imetathmini hali ya kisiasa kuelekea kwenye uchaguzi,uteuzi wa
wagombea uliofanywa na vyama vya siasa, kampeni na nafasi ya wapiga kura na
vyombo vya habari kwenye mchakato mzima wa uchaguzi huo.
Timu hiyo katika taarifa
yake imeleza pia kwamba ilitathmini siku ya upigaji kura yenyewe ikiwa ni
pamoja na idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura,mwenendo wa upigaji
kura,wasimamizi,masuala ya usalama,waangalizi na mawakala wa vyama vya siasa.
Taarifa hiyo ya Timu, iliipongeza Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC)
kwa kusimamia uchaguzi huo kwa weledi, pia iliwapongeza maafisa usalama kwa
kuhakikisha kwamba sheria na taratibu zinafuatwa katika kipindi chote cha
mchakato wa upigaji kura.
‘’Matukio machache ya ghasia hayakuweza kufunika mwendendo mzima wa
amani katika uchaguzi huo,’’ taarifa ilisisitiza.
Taarifa hiyo ya waangalizi
pia iliguswa na idadi kubwa ya kura zilizoharibika ambazo zinaweza kuleta
athari katika matokeo. Ilisema hiyo inawezekana imetokana na wapiga kura
kutoelewa sawia taratibu za upigaji kura.
Taarifa hiyo ilisomwa na
Kiongozi wa Timu ya Waangalizi wa Uchaguzi ya Kanda, Abdulrahman Kinana
aliyefuatana na viongozi wenzake wa timu za waangalizi za COMESA, EAC na IGAD.
Kinana ambaye ni Spika wa
zamani wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) alitoa wito kwa wagombea kuyakubali
matokeo ya uchaguzi huo au kama wana malalamiko watumie njia inayokubalika ya
kuyafikisha mahakamani.
Makundi hayo matatu ya kanda yalikuwa na jumla ya waangalizi 78
waliosambazwa katika kaunti 40 kati ya 47 zilizopo nchini Kenya.
IM/LC/NI
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment