Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Freeman Mbowe
LICHA ya serikali kuyapiga marufuku maandamano yaliyoratibiwa na
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kuishinikiza kumwajibisha
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Naibu wake wajiuzulu kutokana
na matokeo mabaya ya mtihani wa kidato cha nne 2012, chama hicho
kimesema yapo pale pale.
Chama hicho kimewaomba wananchi wote waliochoshwa na kufelishwa kwa
watoto wao, kunyimwa elimu bora wajitokeze kuandamana kwa nguvu zote, na
wanafunzi wote waliofeli pia wajitokeze kudai elimu bora kwani ni haki
yao.
Akizungumza kwa simu na gazeti hili jana na kutoa msimamo huo,
Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe alisema “wananchi wajitokeze kwa
wingi ili kilio chao kisikike duniani kote.”
Alisisitiza kuwa maandamano hayo yatafanyika mbele ya ugeni wa Rais wa
China, Xi Jinping ili kufikisha kilio hicho na kamwe haikubaliani na
sababu ya serikali kuyazuia kwa sababu ya ugeni huo.
Alisema maandamano hayo yatasaidia kupuuza kunakofanywa na Serikali ya
CCM kuonwe na dunia nzima maana vyombo vyote vya habari vitafuatilia
tukio hilo.
Mbowe aliongeza kuwa, “Watanzania waliochoshwa na ubabaishaji katika
elimu wajitokeze, kulaani kitendo cha Waziri Dk. Shukuru Kawambwa na
Naibu wake, Philipo Mulugo kulindwa na serikali, badala ya kuwajibishwa
kwa matokeo mabaya ya watoto wa Kitanzania.”
Alipoulizwa itakuwaje maana kutakuwa na ugeni wa Rais wa China nchini,
sababu ambayo hata serikali imeitumia ili kuyazuia maandamano hayo,
Mbowe alijibu: “Kilio chetu hakikuja na Rais wa China, kama Serikali ya
CCM wanaona aibu kumwajibisha waziri mmoja na naibu wake, basi wasubiri
aibu ya dunia kuona jinsi Tanzania inavyoendeshwa kibabe, ikiwa haina
elimu bora.
“Tumetangaza maandamano wiki tatu zilizopita, hatukuwa na taarifa na
ujio wa Rais wa China, lakini jinsi Mungu alivyo upande wetu amemleta
Rais wa China, kweli Mungu ni mwema, hakuna tena nafasi ya kusubiri
kuficha ubovu katika sekta ya elimu nchini, ndani ya siku ambayo CHADEMA
waliandaa maandamano ili dunia nzima isikie kilio cha Watanzania kuhusu
elimu.
“Sababu kuwa CCM nao wameandaa maandamano kupinga maandamano ya
CHADEMA hazina msingi ni kutowajibika kwa Jeshi la Polisi. Hatukatazi
maandamano, polisi wapange ratiba siku tofauti, sisi tutaandamana
kumpinga waziri ili kama CCM wataandamana kumpongeza waziri wao
wapangiwe siku yao, ila sisi tulitangaza mapema na barua tulipeleka kwa
mujibu wa sheria za nchi yetu.”
Alipoulizwa kwanini asisubiri Tume ya Waziri Mkuu itoe majibu, Mbowe
alisema: “Hatuna shida na Tume ya Waziri Mkuu, matatizo ya elimu katika
nchi yetu yapo wazi, tukizungumza bungeni wanatuchakachua, na sasa huku
nje wanatukejeli, tunataka ifike mahali wajue kuwa nchi hii ni yetu
sote, na Watanzania wanapaswa kusikilizwa kilio chao.”
Kwa mujibu wa Mbowe, maandalizi ya maandamano hayo yanayotarajiwa
kufanyika katika mikoa ya Mbeya, Mwanza, Arusha na Dar es Salaam,
yamekamilika.
Jana, Idara ya Habari (Maelezo) ilitoa barua iliyosainiwa na
mkurugenzi wake, Assah Mwambene kuzuia maandamano yaliyokuwa yafanyike
Jumatatu ijayo katika mikoa ya Mbeya na Arusha tu.
Taarifa hiyo haikuzungumzia maandamano yaliyopangwa kufanyika jijini Dar es Salaam wala Mwanza.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, serikali ilisema kuwa
maandamano ya CHADEMA yalipangwa kuhusisha wananchama kutoka mikoa ya
Mbeya, Iringa, Njombe na Ruvuma, na kuongeza kuwa CCM ilipanga kufanya
maandamanno yake mkoani Arusha kupinga kusudio la CHADEMA kuandamana,
wakieleza kwamba wana imani na tume maalumu ya Waziri Mkuu inayochunguza
tatizo la kufanya vibaya wanafunzi wa kidato cha nne.
Awali CHADEMA walitangaza maandamano yatakayofanyika katika kanda nne.
Kanda ya Kusini yatafanyika Mbeya; Kanda ya Ziwa yatafanyika Mwanza;
Kanda ya Kaskazini yatafanyika Arusha, na Kanda ya Mashariki yatafanyika
Dar es Salaam.
Tanzania Daima ilipomuuliza Mkurugenzi wa Maelezo imekuwaje yeye akawa
msemaji wa jambo hili, alijibu: “Mimi ni msemaji wa serikali, hata
Ikulu naisemea, hivyo usiulize kwanini naisemea polisi.”
Sababu nyingine iliyotolewa na serikali kupitia Maelezo ilisema ni kwa
sababu siku hiyo ni muhimu kwa Watanzania kumpokea Rais mpya wa China
ambaye atakuwa na ziara ya siku mbili nchini.
Februari 19 mwaka huu akiwa jijini Mwanza, Mbowe alitoa siku 14 kwa
Waziri Kawambwa kujiuzulu kutokana na matokeo mabaya ya mtihani wa
kidato cha nne.
Kauli hiyo ilitolewa siku moja baada ya Baraza la Mitihani la Taifa
(NECTA) kutangaza matokeo ya kidato cha nne mwaka 2012 ambapo asilimia
sitini ya wanafunzi wote waliofanya mtihani wamefeli.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment